Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takriban watu 3, 000 wamekufa na 10,000 hawajulikani waliko kufuatia mafuriko Libya:WMO/WHO/IOM/IFRC

Mafuriko yamekumba maeneo ya kaskazini mashariki mwa Libya.
© National Meteorological Centre, Libya
Mafuriko yamekumba maeneo ya kaskazini mashariki mwa Libya.

Takriban watu 3, 000 wamekufa na 10,000 hawajulikani waliko kufuatia mafuriko Libya:WMO/WHO/IOM/IFRC

Msaada wa Kibinadamu

Mafuriko makubwa yaliyoikumba Libya tarehe 10 September yamesababisha maafa ikiwemo vifo vya takriban watu 3,000 na wengine zaidi ya 10,000 kutojulikana waliko Mashariki mwa nchi hiyo  kwa mujibu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na shirikisho la kimataifa la chama cha msalaba mwekundu IFRC na mwezi mwekundu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswis hii leo mkuu wa ujumbe wa IFRC nchini Libya Tamer Ramadan amesema “Kimbunga Daniel kilipiga Mashariki mwa Libya siku mbili zilizopita  na kuathiri maelfu kwa maelfu ya watu kuanzia kwenye vifo, kuachwa bila makazi na wengine kupotea wakati wa kimbunga hicho. Tunachukua hatua katika maeneo yaliyoathirika kwa kushirikiana na wadau wetu Shirika la mwezi mwekundu la Libya. Timu zilipelekwa mara moja wakati kimbunga hicho kilipopika katika miji mitano.”

Hali halisi ya kimbunga hicho

Kwa mujibu wa shirika la utabiri wa hali ya hewa la Umoja wa mataifa WMO, mabwawa mawili yalipasua matawi yake na kusababisha mafuriko makubwa yaliyosoma maeneo ya karibu hadi baharini.

Kimbunga hicho pia kilisababisha kukatika kwa mawasiliano, kuanguka kwa nguzo za umeme na mitin a mafuriko kusambaa pia katika miji mingine.

Maeneo yote ya mji wa Derna Mashariki mwa nchi hiyo yamemezwa na maji sambamba na wakazi wa maeneo hayo na kufanya hali kuwa ya taharuki, janga kubwa lisilohimiliwa.

Bwana Ramadhan amesema “Mahitaji ya kibinadamu na mengi kuliko uwezxo wa shirika la mwezi mwekundu la Libya na zaidi ya uwezo wa serikali ndio maana serikali katika eneo la Mashariki imetoa ombi la msaada wa kimataifa.

Ni janga kubwa kushuhudiwa:WHO

Kwa upande wake msemaji wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO, Margaret Harris ameyaelezea mafuriko hayo kuwa ni zahma kubwa, kimbunga ambachoi hakijawahi kushuhudiwa katika ukanda huo katika kumbukumbu ya Maisha ya sasa, hivyo ni mshangao mkubwa. WHO imepeka msaada katika maeneo yaliyoathirika.”

Msemaji huyo ameongeza kuwa “Mafuriko hayo yameathiri watu angalau milioni 1.5 hadi milioni 1.8. Pia yameathiri na kuharibu hospitali, yamesambaratisha kabisa baadhi ya hospital na kuziacha zingine zikishindwa kufanya kazi. Hivyo kazi kubwa kwa sasa ni kuhakikisha msaada unafika, lakini kwa bahati mbaya baadhi ya msaada huyo ni mifuko ya kufungia maiti na vifaa vya kusaidia waliopata kiwewe.”

Serikali ya Libya imetangaza siku tatu za maombolezo katika maeneo yote yaliyoathirika.

Wahudumu wa dharura, wafanyakazi wa serikali na wakaazi wamekuwa kwakifukua kifusi ili kusaka manusura.

Bi. Harris amesema kipaumbele cha pili cha WHO ni “Kuangalia watu waliotawanywa. Tayari imeelezwa kwamba kuna idadi kubwa ya watu waliotawanywa wanaoishi katika mazingira magumu. Na inabidi tuangalie ni aina gani za hospitali zinaweza kuwekwa kwa muda katika maeneo yaliyoathirika  na aina gani za kliniki zinazotembea. Hivyo kuna kazi kubwa ya kufanya na inafanyaka sasa.”

Lybya ni mdau mkubwa kwa wahamiaji:IOM

Libya imekuwa chachu muhimu kwa wahamiaji wanaoelekea Ulaya kutoka zaidi ya mataifa 44 ambao kuna uwezekano mkubwa pia wameathiriwa vibaya na mafuriko.

"Kuna takriban wahamiaji 600,000 nchini Libya kwa wakati huu na tunafahamu kwamba katika baadhi ya maeneo yaliyoathirika kuna idadi ya wahamiaji lakini katika hatua hii ya awali na masuala mengi ya changamoto za ufikiaji waathirika ambazo sisi na watoa huduma za kibinadamu tunakabiliwa nayo, ni vigumu kutambua na kupata picha kamili ya jinsi ambavyo wameathiriwa vibaya”, amesema Paul Dillon, msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji (IOM). 

Ameongeza kuwa "Lakini kama sehemu ya idadi ya watu kwa ujumla, ungetarajia athari zile zile ambazo wakazi wa eneo hilo wamepata katika muda wa saa 24 zilizopita na bila shaka itaathiri wahamiaji wanaoishi huko pia."

Libya, nchi ya jangwani yenye utajiri mkubwa wa mafuta na imekuwa katika machafuko ya kisiasa tangu mtawala wa muda mrefu Muammar Gaddafi alipopinduliwa na kuuawa mwaka 2011 na kuifanya nchi hiyo kugawanyika na kuongozwa na serikali ya mpito, inayotambulika kimataifa inayofanya kazi kutoka mji mkuu, Tripoli, na nyingine katika eneo la Mashariki.

Tangu mwaka 2014, Libya imegawanyika katika makundi yanayoshindana ya kisiasa na kijeshi yenye makao yake makuu katika maeneo tofauti ya nchi hiyo. Pande hizo mbili zilitia saini makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano mwaka 2020, lakini mizozo ya kisiasa inaendelea.