Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya UN yanasaidia mamilioni ya walioathirika na Mafuriko Pakistan

Kijiji kilichoathirika ma mafuriko huko Matiari, katika mkoa wa Sindh wa Pakistani.
© UNICEF/Asad Zaidi
Kijiji kilichoathirika ma mafuriko huko Matiari, katika mkoa wa Sindh wa Pakistani.

Mashirika ya UN yanasaidia mamilioni ya walioathirika na Mafuriko Pakistan

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanafanya kila juhudi kuhakikisha yanasaidia zaidi ya watu milioni 33 walioathirika na mafuriko nchini Pakistan baada ya mvua za monsoon kunyeesha kwa kiwango kikubwa sana na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 1200 na kuharibu kabisa miundo mbinu mingine. Leah Mushi anatujuza nini mashirika ya UN yanafanya. 

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto ulimwenguni UNICEF ambalo katika taarifa yake limeeleza kusikitishwa na mafuriko ya Pakistan yaliyosababisha vifo zaidi ya 1200 na kati ya hivyo watoto ni takriban 400.

Taarifa ya shirika hilo kutoka Islamabad Pakistan na Geneva Uswisi imeeleza kwa masikitiko kuwa miongoni mwa miundombinu iliyoharibiwa au kusambaratishwa kabisa na mafuriko hayo ni mamilioni ya nyumba, vituo vya afya na shule  takriba 18,000 ama zimesombwa na maji au zime haribiwa vibaya na mafuriko.

Watoto milioni 16 wameathirika na Mafuriko haya, watoto milioni 3.4 wana uhitaji mkubwa wa misaada ya kibinadamu na ufikishaji wa misaada umekuwa mgumu kuwafikia watoto hawa kwani madaraja zaidi ya 160 na zaidi ya kilometa 5000 za barabara zimeharibiwa.

Hata hivyo mwakilishi wa UNICEF nchini Pakistan Abdullah Fadil anasema juhudi za kuokoa maisha na kusambaza misaada ni za lazima, na UNICEF inasambaza vifaa vya kibinadamu katika majimbo yote yaliyoathirika.

Watu waliokimbia makazi yao wakichota maji kutoka kwa tanki la maji lililowekwa na UNICEF baada ya mafuriko makubwa nchini Pakistan.
© UNICEF/Asad Zaidi
Watu waliokimbia makazi yao wakichota maji kutoka kwa tanki la maji lililowekwa na UNICEF baada ya mafuriko makubwa nchini Pakistan.

“Tayari UNICEF tumeshatoa huduma za dharura na vifaa vya dharura vyenye thamani ya zaidi ya Dola milioni 2, ikiwa ni pamoja na maji ya kunywa, tembe za kusafisha maji, vifaa vya usafi, dawa, chanjo, chakula cha matibabu kwa watoto, wajawazito na wanaonyonyesha na vyandarua. 

Shirika jingine la Umoja wa Mataifa ni lile la kuhudumia wakimbizi UNHCR kwani Pakistan ni mwenyeji wa mamilioni ya wakimbizi kutoka mataifa jirani mathalani nchi hiyo imesajili wakimbizi kutoka Afghanistan zaidi ya milioni 1.3 kwa miongo minne sasa.

Kwakutambua taabu zinazowakabili wakimbizi na jamii za wenyeji msemaji wa UNHCR Matthew Saltmarsh amesema “ Tunafanya kazi na mamlaka ya usimamizi wa maafa ya Pakistan, UNHCR imetoa msaada wa haraka mahema, karatasi za plastiki, ndoo na vifaa vingine vya nyumbani katika mikoa iliyoathiriwa vibaya ya Khyber Pakhtunkwa na Balochistan, ambapo tumesambaza mahema 10,000 na vifaa vingine vya msaada. 

Ameongeza kuwa msaada pia unakimbizwa katika maeneo yaliyokumbwa na mafuriko kusini mwa mkoa wa Sindh.

“Tunapanga kusaidia kaya 50,000 hivi katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi  kwa kuwafikishia misaada zaidi ya milioni moja.”

Watoto walioathirika na mafuriko nchini Pakistan wakipimwa na wataalam wa afya
© UNICEF/UN0691112/Sami Malik
Watoto walioathirika na mafuriko nchini Pakistan wakipimwa na wataalam wa afya

Makazi, maji safi ya kunywa na chakula ni miongoni mwa vitu vinavyohitajika kwa haraka baada ya mafuriko. Na Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO limesema lina wasiwasi mkubwa kwani tayari zimeanza kutolewa ripoti za wagonjwa wa Kuharisha, matatizo ya ngozi, mifumo ya kupumua, Malaria na Ndengue. 

Kutokana na ripoti hizo ndio maana WHO imeongeza mwitikio wake kwa kutibu waliojeruhiwa, kupeleka vifaa kwenye vituo vya usaidizi vinavyotoa huduma za afya, na kuzuia kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza, na inatuma timu ya upasuaji ya wataalamu wa afya ya umma kutoka ofisi ya Kanda ya WHO hadi Pakistan kusaidia wenye uhitaji.