Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuriko yafurusha makwao zaidi ya watu 700,000 nchini Sudan Kusini

Nyumba zilizofurika kando ya kingo za mto wa Akobo huko Sudani Kusini.
© WFP/Theresa Piorr
Nyumba zilizofurika kando ya kingo za mto wa Akobo huko Sudani Kusini.

Mafuriko yafurusha makwao zaidi ya watu 700,000 nchini Sudan Kusini

Msaada wa Kibinadamu

Mvua kubwa zilizonyesha katika kipindi cha miezi 6 iliyopita nchini Sudani Kusini zimeathiri miundombinu ya barabara, madaraja na viwanja vya ndege huku zaidi ya wakazi  700,000 wa kaunti ya Maban jimboni Jonglei wakisalia wakiiishi bila kupata msaada wowote kutokana na eneo lote kujaa maji.

Wafanyakazi wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi UNHCR kwa kutumia helipokta wameweza kufika eneo hilo ili kujionea athari za mafuriko

Video iliyopigwa na UNHCR kutokea angani inaonesha namna mvua kubwa zilivyoathiri kaunti ya Maban.
Ukungu wa kijani umetapakaa katika eneo kubwa la kaunti hii na wananchi ili waweze kutoka eneo moja kwenda jingine, mizigo inabebwa kichwani na wanalazimika kunyanyua nguo zao juu kwakuwa maji namepita usawa wa magoti.
 
Athari zilizoletwa na mafuriko hayo ni pamoja na nyumba kadhaa kusombwa na maji, mashamba kuharibiwa kabisa wale wenye mifugo wamelazimika kuihamishia maeneo ya juu katika miji Jirani, na kuwaacha wakazi wa hapa wakihitaji si makazi pekee bali chakula, maji na huduma za usafi wa mazingira.

Mwakilishi wa UNHCR nchini Sudani Kusini Arafat Jamal wakati akifanya tathmini, wakazi wa eneo hili wakawa na ombi kama asemavyo mwakilishi wao Amer Diing.

"Ombi letu kwa serikali na mashirika, watupatie plastiki za kujifunika kwa sababu iwapo maji hayataingia kwenye nyumba zetu, tunaweza kutengeneza mifereji midogo ya kuzunguka nyumba zetu. Lakini ikiwa mvua inaendelea, kuna umuhimu wa kuwa na plastiki hizo kutufunika. Hofu yetu kuu ni kwa watoto ambao kwa kuwa hatua kitu cha kuwafunika wanaweza kuugua kutokana ubaridi unaosababishwa na maji ya mvua.”

Na ndipo mwakilishi wa UNHCR akasema,

"Mabadiliko ya tabianchi hayalazimishi kukata tamaa kwa sababu kuna suluhisho, suluhisho ni pamoja na kusukuma maji kwa kutumia bomba, kutenganesha mifereji na mipango mizuri. Tunachopenda kufanya ni kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wananchi pamoja na serikali kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kuona jinsi ya kufanya maisha ya watu kuwa bora na yenye matumaini zaidi. "