Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu waliokufa kwa COVID-19 mwaka 2022 wafikia milioni 1: WHO

Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus akizungumza katika moja ya taarifa za WHO kuhusu janga la COVID-19
UN Photo/Evan Schneider
Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus akizungumza katika moja ya taarifa za WHO kuhusu janga la COVID-19

Watu waliokufa kwa COVID-19 mwaka 2022 wafikia milioni 1: WHO

Afya

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema watu hawapaswi kujisahau wala kuchukulia kama janga la COVID-19 limeisha duniani kwani bado lipo na linaendelea kuuawa mamilioni ya watu.

Akizungumza na waandishi wa Habari jijini Geneva Uswisi Dkt Tedros amesema “Hatuwezi kusema tunajifunza kuishi na COVID-19 wakati watu milioni moja wamekufa na COVID-19 mwaka huu pekee.”

Amewaambia waandishi wa habari kuwa miaka miwili na nusu ya janga la COVID-19 duniani “tuna nyenzo zote tunazohitaji za kuzuia vifo vitokanavyo na janga hili.”

Ametoa wito kwa serikali zote ulimwenguni kuoimarisha juhudi zao za kutoa chanjo kwa wahudumu wote wa afya, wazee, na wengine walio katika hatari kubwa zaidi, mbinu hii ikiwa ni moja katika njia za kuweza kufikia utoaji wa chanjo ya COVID-19 kwa asilimia 70 kwa watu wote.

Chanjo kwa jamii zinazohifadhi wakimbizi Uganda.
© UNICEF/Maria Wamala
Chanjo kwa jamii zinazohifadhi wakimbizi Uganda.

Hongera Afrika kwa kasi ya utoaji chanjo 

Akipongeza juhudi za kuendelea kutoa chanjo Mkuu huyo wa WHO ameseme “Inafurahisha kuona kwamba baadhi ya nchi zilizokuwa na viwango vya chini zaidi vya chanjo sasa zinainuka hususan barani Afrika.”

Akaongeza kuwa "Inafurahisha sana kuona kwamba utoaji chanjo unazingatia makundi yanayohitajika kupewa kipaumbele huku nchi nyingi zikipiga hatua ya kuvutia katika kutoa chanjo kwa asilimia 100 ya wafanyakazi wa afya na asilimia 100 ya wazee.”

Hata hivyo Dkt. Tedros amesema bado mengi zaidi yanahitajika kufanywa ili kutokomeza janga hilo la Afya ulimwenguni.