Kupata chanjo ya tatu na nne kunaweza kuleta balaa kwa wananchi na nchi- WHO
Shirika la Umoja wa Matiafa la afya ulimwenguni WHO limeonya juu ya kile kinachoonekana kuwa baadhi ya watu wanataka kuanza kuchanganya chanjo za ugonjwa wa Corona au COVID-19 na kueleza tabia hiyo inaweza kuwa na madhara kwa watu hao na pia kwa nchi zao.
Janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 likiwa lina miezi 18 sasa duniani, idadi kubwa ya watu katika nchi zilizoendelea tayari wamepata chanjo dhidi ya ugonjwa huo huku wengine wakiwaza na kuwazua iwapo chanjo hiyo bado ni muhimu kwao au la.
Upatikanaji wa chanjo katika nchi hizo zilizoendelea umekuwa ni rahisi ambapo baadhi ya watu waliokwishakupata chanjo iwe ile ya dozi mbili kama Pfizer au Moderna au chanjo moja ya Johnson and Johnson wanaripotiwa kufikiria kwenda kupata chanjo ya ziada jambo ambalo WHO inasema kitendo hicho kinaweza kuwa tatizo.

Dkt. Soumya Swaminathan, mwanasayansi mkuu wa WHO anasema,“sasa kuna tabia ya watu katika nchi zenye chanjo za kutosha kwa hiari yao kuanza kufikira kuongeza dozi. Wengine wanafikiria kuchanganya na kulinganisha, tumeona maswali mengi ya watu waliopata aina moja ya chanjo na wanapanga kuchukua aina nyingine ya chajo. Hii kidogo ni hatari kwa watu wanaowaza kufanya hivi. eneo hili kuna takwimu chache juu ya kuchanganya na kulinganisha chanjo. Kuna utafiti mdogo bado unaendelea juu ya kuchanganya chanjo. Lazima tusubiri matokeo ya utafiti yatoke ndio itakuwa njia nzuri zaidi, lakini kwa sasa tuna takwimu za chanjo ya AstraZenica, ikifuatiwa na Pfizer. Itakuwa balaa kwa hizi nchi kama wananchi wake wataanza kujiamulia muda gani na nani anapaswa kuchukua chanjo ya pili, ya tatu na ya nne.”
Kuhusu suala la kuwa na kichocheo cha nguvu ya chanjo kwa kiingereza BOOSTER kwa wale waliopata chanjo, Mkuu wa Programu ya chanjo WHO Dkt. Ann Lindstrand amesema bado hakuna takwimu za kuthibitisha uhitaji wa kuongeza nguvu kwenye chanjo watu walizopatiwa.
Dkt. Lindstrand anasema, “jopo letu la wataalamu wa ushauri na mikakati wanaendelea kuangalia iwapo kuna uhitaji wa kutumia dozi ya kuongeza nguvu kwenye chanjo ambazo watu wameshapatiwa. Lakini kwa wakati huu hakuna takwimu za kutosha kuongeza dozi hizi, hasa kwa kuzingatia usambazaji wa chanjo ambao bado upo katika kiwango cha chini sana duniani badala ya kufikiria kupata chanjo ya nyongeza ni vyema kufikira kusambaza kwenye nchi ambazo hata bado hazijaanza kutoa chanjo kwa watoa huduma wake wa vituo vya afya”
WHO imesema Corona bado ni janga kwa ulimwengu hivyo nchi zinapaswa kuwahimiza wananchi wake wajilinde na kulinda wale walio katika hatari zaidi ya kupata maambukizi katika jamii zao kwa kuwa wasipofanya hivyo hospitali zitazidiwa tena uwezo na nchi hazitakuwa na namna zaidi ya kurejea kuweka vikwazo zaidi ili kudhibiti maambukizi.