Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wagonjwa wa COVID19 na Monkeypox waongezeka duniani

Mwanamke akichomwa chanjo ya pili ya dozi ya COVID19 katika kituo cha afya huko Obassin , Burkina Faso
© UNICEF/Frank Dejongh
Mwanamke akichomwa chanjo ya pili ya dozi ya COVID19 katika kituo cha afya huko Obassin , Burkina Faso

Wagonjwa wa COVID19 na Monkeypox waongezeka duniani

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO limehimiza nchi wanachama kuhakikisha zinaendelea  kujikinga na janga la COVID19 kwakuwa janga hilo lingalipo na takwimu za wiki mbili zilizopita zinaonesha kuongezeka kwa wagonjwa kwa takriban asilimia 30.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus akiongea na waandishi wa habari hii leo jijini Geneva Uswisi amesema katika kanda sita za WHO kanda nne zimeripoti kuongezeka kwa wagonjwa wa COVID19.

Dkt Ghebreyesus ametaja changamoto zinazosababisha kuongezeka kwa wagonjwa wa COVID-19 pamoja na kuibuka kwa aina mpya za virusi huko nchini India, Barani ulaya na Amerika na kusema sababu za kuongezeka huko ni:-

Mosi, upimaji umepungua kwa kiasi kikubwa sana, na hii inathibitika na kuibuka kwa virusi vinavyo badilika kila mara hali inayozidisha mzigo wa ugonjwa huo ulimwenguni. Lakini pia ikionesha matibabu hayapewi umuhimu wa kutosha kuzuia ugonjwa huo pamoja na vifo.

“Pili matibabu mapya ambayo ni dawa za kunywa bado hayajawafikia hususan nchi za kupato cha chini na cha kati na hivyo wale wenye uhitaji kukosa” amesema Mkuu huyo wa WHO

 

Chanjo kwa jamii zinazohifadhi wakimbizi Uganda.
© UNICEF/Maria Wamala
Chanjo kwa jamii zinazohifadhi wakimbizi Uganda.

Mengine aliyoeleza ni pamoja na virusi kubadilika, kinga ya mwili kupungua na hivyo kuhitajika kuongezewa dozi za chanjo za COVID19 huku wimbi la virusi likiacha watu wengi zaidi katika hali ya kuw ana COVID19 kwa muda mrefu wakati wanaugua na hata baada ya kuugua.

“Changamoto hizi zinahitaji hatua kuchukuliwa katika ngazi ya kimataifa, kitaifa na ngazi ya chini kabisa ya kila eneo. Serikali, wanasayansi, watengenezaji dawa na chanjo, WHO pamoja na wananchi wenyewe wote wana sehemu yao ya kutekeleza.” Amesema Dkt Tedros na kutaja hatua muhimu za kuchukua ni pamoja na “kutoa chanja hususa kwa wale walio katika hatari zaidi. Hii ni pamoja na wazee, watu walio na magonjwa sugu, wasio na kinga na wafanyakazi kwenye sekta ya afya.”

Amehimiza kila nchi kuhakikisha zinajenga  kinga kwa watu wote pamoja na kuwapatia dawa mpya za kumeza za kuzuia virusi na matibabu mengine yanayopatikana kwa wote.

Vidonda vya Monkeypox mara nyingi huonekana kwenye mikono ya mikono.
© CDC
Vidonda vya Monkeypox mara nyingi huonekana kwenye mikono ya mikono.

Monkeypox yaenea nchi 58

Akizungumzia ugonjwa wa ndui ya nyani au Monkeypox Dkt. Tedros amesema ugonjwa huo unazidi kusambaa katika mataifa mbalimbali duniani na WHO ina wasiwasi na kusambaa huku kwa wagonjwa na kuenea kwa virusi

“Ulimwenguni kote, sasa kumekuwa na zaidi ya wagonjwa 6000 wakirekodiwa katika nchi 58.Upimaji unasalia kuwa changamoto na kuna uwezekano mkubwa kuwa kuna idadi kubwa ya watu wanaougua ugonjwa wa Monkeypox lakini bado hawaja tambulika.”

Ametaja bara la Ulaya ndio kitovu cha sasa cha mlipuko huo, kukiwa na rekodi zaidi ya asilimia 80 ya wagonjwa wote duniani.

Barani Afrika, tayari kuna rekodi za wagonjwa ambao wametambulika kutoka nchi ambazo hazikuwahi kuathiriwa hapo awali na rekodi za wagonjwa kutoka atika maeneo ambayo hapo awali yamewahi kuwa na wagonjwa wa Monkeypox.

“Timu zangu inafuatilia kwa karibu takwimu hizi, ninapanga kuwakutanisha tena Kamati ya dharura ili yupate masahihisho mapya kuhusu magonjwa na mabadiliko ya sasa ya mlipuko huo, na utekelezaji wa hatua za kukabiliana nazo.” Amesema mkuu huyo wa WHO ambaye amesema timu hiyo inatarajia kukutana tarehe 18 Julai 2022 au mapema zaidi ya hapo iwapo watahitajika kufanya hivyo.

Chanjo ya Monkeypox

WHO imeelza infanya kazi kwa karibu na nchi na watengenezaji chanjo ili kuratibu ugawaji wa chanjo, ambayo kwa sasa ni adimu na inahitaji kupatikana kwa watu walio hatarini zaidi.

WHO pia inafanya kazi kwa karibu na mashirika ya kiraia na jumuiya ya watu wanaoshirki mapenzi ya jinsia moja LGBTIQ+, hasa kusaidia kuondokana na unyanyapaa na ili kuelimisha jamii taarifa za jamii ziweze kujilinda badala ya kunyooshea mkono wale wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja pekee.

“Ninapenda kuwapongeza hasa wale ambao wanashiriki kutoa video mtandaoni kupitia chaneli za mitandao ya kijamii wakizungumza kuhusu dalili na uzoefu wao wa Monkeypox, hii ni njia chanya ya kuondoa unyanyapaa kuhusu virusi ambavyo vinaweza kuathiri mtu yeyote.” Alihitimisha Mkuu huyo wa WHO.