Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vifo vya waafrika 23 katika mpaka wa Melilla wataalamu wa UN wataka uwajibikaji

Melilla karibu na mpaka wa Hispania na Morocco
Unsplash/Christelle Hayek
Melilla karibu na mpaka wa Hispania na Morocco

Vifo vya waafrika 23 katika mpaka wa Melilla wataalamu wa UN wataka uwajibikaji

Wahamiaji na Wakimbizi

Wataalamu huru wa Umoja wa Mataifa hii leo wameyataka mataifa ya Morocco na Hispania kuhakikisha uchunguzi huru unafanyika na hatua kuchukuliwa kwa wale waliohusika na vifo vya waafrika 23 waliokuwa wakijaribu kuvuka mpaka wa Melilla unaotenganisha nchi hizo mbili wakitaka kwenda ulaya. 

Taarifa iliyotolewa leo kutoka Geneva Uswisi na wataalamu watatu wa Umoja wa Mataifa wa mfumo huru wa Kimataifa IIEM ambao ni Justice Yvonne Mokgoro, Dkt.Tracie Keesee na Profesa Juan Mendez imesema vifo hivyo vilitokea wakati ambapo takribani watu 2000 walijaribu kuvuka uzio mrefu huko kaskazini mwa Afrika. 

“Matumizi yoyote ya nguvu yanayotumiwa na maafisa wa polisi yanapaswa pia kuongozwa na kutekeleza sheria na kanuni za uhalali, tahadhari, umuhimu, uwiano, uwajibikaji na bila ubaguzi,” walisema wataalamu hao waliopewa jukumu la kuhakikisha wanaangalia masuala ya mamlaka kuendeleza haki na usawa bila ubaguzi wa rangi wakati wa utekelezaji wa sheria na pia wataalamu hawa ni kikosi Kazi cha Wataalam wa Umoja wa Mataifa kuhusu watu wenye asili ya Kiafrika.

IIEM imekusanya taarifa ya tukio hilo kutoka kwa serikali za Hispania na Morocco hususan kuhusu maendeleo ya uchunguzi unaoendelea. 

“Tutaendelea kufuatilia na kushirikiana na mamlaka za Hispania na Morocco. Tuko tayari kutoa mwongozo na mapendekezo kwa Mataifa na wadau wote husika ili kuhakikisha waathiriwa na familia zao wanapata haki.”

Wataalamu hao wamezitaka serikali zote mbili kutoa taarifa juu ya udhibiti wa ndani wa matumizi ya nguvu na hatua zinazochukuliwa ili kuhakikisha tukio kama hilo halijirudii tena. 

“Tunatambua kuwa uchunguzi umeshaanza na tunatoa wito kwa Hispania na Morocco kuchukua hatua zote muhimu kwakushirikiana na Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika ili kuhakikisha kuna uwajibikaji wa haraka, kuwalipa fidia waathirika na kuzuia tukio la namna hii la vifo likitokea.” Wameongeza wataalamu hao. 

Wamesema kutokana na taarifa zilizokusanywa, pia watafanya tathmini ya sheria na taratibu za utekelezaji wa sheria katika nchi zote mbili kinyume na viwango vinavyotumika vya haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na Kanuni za Msingi za Umoja wa Mataifa kuhusu Matumizi ya Nguvu na Silaha za moto kwa wasimamizi wa sheria, na miongozo ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, pia wataangalia mwongozo juu ya silaha zisizo na hatari katika utekelezaji wa Sheria.

“Tunataka kutoa mapendekezo madhubuti kwa serikali zote mbili kukomesha mzunguko huu wa matukio hatari ya Waafrika wanapotekeleza sheria,” alisema Jaji Mokgoro, Mwenyekiti wa IIEM.

Wataalamu hao walikumbusha mapendekezo waliyotoa kwenye ziara yao mwaka 2018 nchini Hispania  (https://undocs.org/en/A/HRC/39/69/Add.2.) ambapo walionesha wasiwasi juu ya  namna waofikia katika mipaka ya Hispania ya Ceuta na Melilla wanavyorudishwa nyuma .