Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahamiaji sita wauawa mahabusu Tripoli IOM yashutumu 

Wahamiaji katika kituo cha kuzuiliwa cha mji wa Zawiya nchini Libya
Photo: Mathieu Galtier/IRIN
Wahamiaji katika kituo cha kuzuiliwa cha mji wa Zawiya nchini Libya

Wahamiaji sita wauawa mahabusu Tripoli IOM yashutumu 

Wahamiaji na Wakimbizi

Wahamiaji sita wameuawa na wengine 24 wamejeruhiwa katika kituo cha mahabusu walikokuwa wakishikiliwa cha Mabani huko mjini Tripoli nchini Libya wakati walinzi wenye silaha walipoanza kufyatua risasi kufuatia ghasia na jaribio la kutoroka, limesema leo shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM.

Shirika hilo linalaani vikali mauaji hayo ya ya kikatili yaliyotokea Ijumaa na matumizi ya risasi za moto dhidi ya wahamiaji wanaopinga hali mbaya katika kizuizini. 

Kabla ya ufyatuaji risasi, zaidi ya wahamiaji 3,400, wakiwemo wanawake 356 na watoto 144, walizuiliwa katika kituo hicho kilichojaa watu cha Mabani. 

Wengi walikuwa wamekamatwa wakati wa msako wiki iliyopita katika kitongoji cha Gergaresh na walikuwa walizuiliwa kiholela.

Mkuu wa IOM nchini Libya Federico Soda amesema “Matumizi ya nguvu kupita kiasi na machafuko ambayo mara nyingi husababisha vifo ni kitu kinachotokea mara kwa mara katika vituo vinavyoshikilia watu nchini Libya.”

Ameongeza kuwa “Baadhi ya wafanyikazi wetu walioshuhudia tukio hili wanaelezea kuwa wahamiaji waliojeruhiwa walikuwa wamelala kwenye dimbwi la damu. Tumeumizwa sana na upoteaji huu mbaya wa maisha.”

Daktari mmoja na muuguzi aliyepewa kandarasi na IOM walikuwa katika kituo hicho cha mahabusu wakitoa huduma ya upimaji mara kwa mara, matibabu na msaada wakati ghasia zilipozuka na wahamiaji kadhaa wakijaribu kutoroka.

Timu za IOM zilichukua wahamiaji wanne waliojeruhiwa vibaya hadi kliniki ya kibinafsi na wengine 11 kwenye hospitali ya eneo hilo. 

Madaktari hao bado wako Mabani wakitoa msaada wa dharura wa matibabu.

Wahamiaji zaidi ya 1,000 katika kituo hicho cha mahabusu walikuwa wameomba msaada wa huduma ya IOM ya kurejeshwa nyumbani kwa hiyari na wamekuwa wakingojea kwa miezi kadhaa kufuatia uamuzi wa upande mmoja na usio wa haki wa kurugenzi ya kupambana na uhamiaji haramu (DCIM) wa kusimamisha safari za ndege za kibinadamu kutoka nchini humo.

IOM inatoa wito kwa viongozi wa Libya kuacha kutumia nguvu kupita kiasi, kumaliza vitendo vya kuzuia watu kiholela na kuanza tena safari za ndege ili kuwaruhusu wahamiaji kuondoka.

Karibu wanaume, wanawake na watoto 10,000 wamekwama katika hali mbaya kwenye vituo hivyo rasmi vya kizuizini ambavyo vimepunguza na mara nyingi havinafursa ya kufikiwa na wahudumu wa kibinadamu.