Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Algeria acheni kuwatimua kwa pamoja wahamiaji:UN

Wakimbizi nchini Algeria. Picha:WFP/Algeria

Algeria acheni kuwatimua kwa pamoja wahamiaji:UN

Haki za binadamu

Umoja wa Mataifa leo umetoa wito kwa serikali ya Algeria kusitisha vitendo vya kuwafukuza kwa pamoja wahamiaji hususani kutoka Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Ingawa idadi kamili ya waliotimuliwa haijajulikana inaaminika ni maelfu ya wahamiaji.

Kwa mujibu wa timu ya ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa iliyozuru Niamey, Argadez na Arlit nchini Niger ambako waliwahoji wahamiaji 25 miongoni mwa waliotimuliwa kutoka Algeria pamoja na wengine waliopitia hali kama hiyo walichokisikia ni kwamba, malaka ya Algeria mara kwa mara inawakusanya wahamiaji kutoka nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara katika sehemu mbalimbali za Algeria na kuwafukuza.

Lakini pia inafanya msako katika maeneo ya ujenzi mjini Algiers na viunga vyake ambako kunajulikana kuwa na wahamiaji wengi na wengine wamekuwa wakisimamishwa mitaani na kuswekwa rumande. Ravina Shamdasan ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu Geneva Uswis, “Kinachotia wasiwasi hasa ni kwamba wengi wa watu tuliozungumza nao wamesema hawakufanyiwa tathmini binafsi, na hawakuelezwa sababu za kufungwa kwao, wala hawakuruhusiwa kuchukua vitu vyao, hati za kusafiria au fedha kabla ya kufukuzwa. Wengi waliacha kila kitu walichokuwanacho.

Ameongeza kuwa wakati wengine walipelekwa haraka Niamey ,waliosalia wanashikiliwa katika vituo vya kijeshi vya Blida na Zeralda nje kidogo ya Algers, kisha wanapelekwa Tamanrasasset Kusini kwa Algeria ambako wahamiaji kutoka Nigeria wanawekwa kwenye mabasi na kusafirishwa hadi Agadez Niger, na wahamiaji wengine wanarundikwa kwenye malori na kwenda kutelekezwa kwenye mpaka wa Nigeria ambako wanalazimika kutembea jangwani kwa mwendo mrefu ili kufika mpaka wa Niger.

 

Image
UN Photo/Evan Schneider
Wakimbizi wa Sahrawi kambini Smara nje ya Tindouf, Algeria.

Ofisi ya haki za binadamu inasema hali katika rumande ni mbaya sana na ya kuwadhalilisha wahamiaji hao, na kitendo cha kuwatimua Waafrika kinatia hofu ya ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya Waafrika kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Pia kuwafukuza wahamiaji hao bila kuwafanyia tathimini ni inasikitisha na ni kinyume cha sheria za kimataifa za haki za binadamu na mikataba ya kimataifa ya kuwalinda wakimbizi na wahamiaji.

Kwa muktadha huo imeitaka Algeria kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa na  kamati ya wafanyakazi wahamiaji mwezi Aprili ambayo yanakataza kuwafukuza watu kwa pamoja, lakini pia yanataka kuanzishwa kwa mkakati wa kuhakikisha kwamba  wanazingatia viwango vya kimataifa vinavyotakiwa wanapoamua kuwatimua wafanyakazi wahamiaji.