Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huduma za maji safi ya kunywa shuleni yasalia ndoto kwa watoto wengi duniani

Mukasa Herbert mwanafunzi katika Shule ya Nakivubo Settlement Nursery na Primary School nchini Uganda ananawa mikono siku ya kwanza ya kufungua tena shule, Januari 10, 2022.
© UNICEF/Maria Wamala
Mukasa Herbert mwanafunzi katika Shule ya Nakivubo Settlement Nursery na Primary School nchini Uganda ananawa mikono siku ya kwanza ya kufungua tena shule, Januari 10, 2022.

Huduma za maji safi ya kunywa shuleni yasalia ndoto kwa watoto wengi duniani

Afya

Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa hii leo yamesema kuwa ingawa idadi ya shule zisizo na huduma za msingi za maji na kujisafi, WASH zimepungua bado kuna pengo kubwa la huduma hizo ndani ya nchi n ahata baina ya nchi.

Taarifa ya mashirika hayo, lile la afya duniani, WHO na la kuhudumia watoto, UNICEF iliyotolewa leo katika miji ya Geneva, Uswisi na New York, Marekani inasema hali ni tete zaidi kwa shule zilizo katika nchi zinazoendelea, LDCs na zaidi ya yote, “ni shule chache zenye huduma za maji na kujisafi kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu.” “Watoto wengi wanakwenda shuleni bila huduma ya maji safi na salama, vyoo visafi na sabuni ya kunawa mikono na hii husababisha suala la kujifunza kuwa ni gumu,” amesema Kelly Ann Naylor, Mkurugenzi wa UNICEF akihusika na Maji, Kujisafi, Tabianchi, Mazingira, Nishati na Upunguzaji wa athari za majanga. Amesema janga la COVID-19 limeibua umuhimu wa kuweka mazingira ya kujifunza yenye afya na jumuishi. Kulinda elimu ya watoto wakati huu wa kujikwamua kutoka janga la COVID-19 ni lazima kupatia shule huduma za msingi ili kupambana na magonjwa ya kuambukiza kwa sasa na siku za usoni.” Takwimu zinaonesha hali tete • Duniani kote, asilimia 29 ya shule bado hazina huduma za maji safi na salama ya kunywa na hivyo kuathiri wanafunzi milioni 546. Asilimia 28 ya shule hazina huduma za kujisafi hivyo kuathiri watoto milioni 539 • Theluthi moja ya watoto wasio na huduma za msingi shuleni kwao wanaishi katika nchi zinazoendelea, LDCs na nusu yao mazingira wanamoishi ni duni. • Nchi za Afika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara pamoja na zile za Oceania ndio maeneo ambako huduma za kujisafi shuleni ziko chini ya asilimia 50. Halikadhalika huduma za maji safi na salama la kunywa shuleni bado ni tete Afrika, Kusini mwa jangwa la Sahara. “Kupata maji safi na salama, huduma za kujisafi na vyoo siyo tu ni muhimu kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya magonjwa, bali pia ni muhimu kwa afya na ustawi wa mtoto,” amesema Dkt .Maria Neira Mkurugenzi wa WHO, Idara ya Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Afya. Amesema shule lazima ziwe mazingira ambamo watoto wanastawi na kuchanua badala ya kuwa eneo la machungu na magumu kutokana na ukosefu wa miundombinu ya msingi.