Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maji safi na salama yasalia anasa kwa robo ya wakazi wa dunia, ripoti ya UN yatoa mapendekezo

Mtoto akijaza maji kwenye dumu katika makazi ya wakimbizi ya Mendruzi huko nchiini Msumbiji (2019)
© UNICEF/Karel Prinsloo
Mtoto akijaza maji kwenye dumu katika makazi ya wakimbizi ya Mendruzi huko nchiini Msumbiji (2019)

Maji safi na salama yasalia anasa kwa robo ya wakazi wa dunia, ripoti ya UN yatoa mapendekezo

Afya

Serikali lazima ziwekeze zaidi kwenye ujenzi wa mifumo yam aji safi na salama ya kunywa ili kuhakikisha kila mtu anapata huduma hiyo lakini pia kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi, imesema ripoti mpya iliyotolewa leo na mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la afya ulimwenguni, WHO, la kuhudumia watoto, UNICEF na Benki ya Dunia.

Wito wa ripoti hiyo inazingatia lengo namba 6 la Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs ambalo pamoja na mambo mengine linataka huduma ya maji safi na salama pamoja na huduma za kujisafi zipatikane kwa watu wote ifikapo mwaka 2030, malengo ambayo nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa ziliridhia mwaka 2015.

Ikiwa imesalia miaka 8 kufikia ukomo huo, ripoti inafichau kuwa ingawa zaidi ya watu bilioni mbili wamepata huduma ya maji safi katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili iliyopitam robo ya wakazi wa dunia hivi sasa bado hawana huduma hiyo.

Mtoto akijaza maji safi kwenye dumu katika kambi ya wakimbizi karibu na Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC
© UNICEF/Olivier Asselin
Mtoto akijaza maji safi kwenye dumu katika kambi ya wakimbizi karibu na Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC

Haki ya msingi ya binadamu

Wakati huo huo, mabadiliko ya tabianchi yanaongeza viwango na vipindi vingi zaidi vya ukame na mafuriko, na hivyo kuchochea uhaba wa maji halikadhalika kuvuruga usambazaji wa huduma hiyo.

Kasi kubwa ya kukua kwa miji pia kunafanya hali inakuwa ngumu zaidi kwa miji kusambaza maji kwa mamilioni ya wakazi wake wanaoishi kwenye maeneo yasiyo rasmi au maeneo ya mabanda.

“Kufikisha huduma ya maji safi na salama kumeokoa watu wengi hususan uhai wa watoto. Lakini mabadiliko ya tabianchi yanavuruga mafanikio hayo,” amesema Dkt. Maria Neira, Mkurugenzi wa WHO, Idara ya Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Afya.

“Tunaongeza juhudi zetu ili kuhakikisha kila mtu ana fursa ya kupata maji safi na salama ya kunywa, kitu ambacho ni haki ya binadamu na si anasa.”

© UNICEF/Delil Souleiman
Mtoto akiwa kwenye kambi ya muda huko Ain Issa nchini Syria. (3 Juni 2019)
© UNICEF/Delil Souleiman

Uwekezaji Muhimu

Ripoti inachunguza uhusiano aina ya maji, afya na maendeleo.

Inatoa pia mapendekezo ya hatua ambazo serikali na wadau wanapaswa kuchukua ili kuongeza uwekezaji kwenye mifumo salama ya maji safi na salama, kuimarisha mipango, kuratibu na kusimamia utoaji wa huduma.

Mifano inaonesha ni kwa vipi nchi zinachangia katika kufanikisha malengo madogo ya lengo namba 6 la SDGs.

“Kuwekeza kwenye maji na huduma za kujisafi ni muhimu kwa afya, ukuaji wa uchumi na mazingira. Watoto wenye afya bora zaidi watakuwa watu wazima wenye afya zaidi na kuchangia zaidi kwenye uchumi na jamii,” amesema Sajor Kumar Jha, ambaye ni Mkurugenzi wa Water Global Practice kutoka Benki ya Dunia.

Watoto wawe salama

Wadau hao wametoa wito kwa serikali na sekta binafsi kuongeza kwa kiasi kikubwa ahadi zao za kisiasa kwenye masuala ya maji safi na salama ya kunywa na uwekezaji huo uongezwe mara nne zaidi.

“Hakuna mtoto ambaye anapaswa kuwa na fursa ya kuchagua kunywa maji machafu ambayo yanaongoza kwa kusababisha vifo vya watoto, au fursa ya kutembea safari ndefu na hatari kufuata maji na hivyo kukosa shule,” amenukuliwa Aidan Cronin, Kaimu Mkuu wa Idara ya UNICEF inayohusika na huduma za maji na kujisafi, WASH na tabianchi, mazingira, nishati na udhibiti wa athari za majanga, CEED.

Ameongeza kuwa kupata maji na kwa uhakika ni suala la msingi la kuhakikisha watoto wanasalia na afya, wanasoma na wanastawi.

Mtoto akiwa amebeba maji huko Cox's Bazar nchini Bangladesh (10 Julai 2019)
© UNICEF/Patrick Brown
Mtoto akiwa amebeba maji huko Cox's Bazar nchini Bangladesh (10 Julai 2019)

Hatua za serikali

Ripoti inatoa pia mapendekezo ya kina kwenye uboreshaji wa masuala ya usimamizi, ufadhili, ujengeaji uwezo, data, taarifa na ugunduzi.

Mathalani, kuimarisha taasisi zilizoko; mfano kwa kuanzisha mazingira bora ya usimamizi wa rasilimali maji, kuweka sheria na kanuni za huduma bora na kuhakikisha zinasimamiwa.

Halikadhalika fedha ziongezwe, na watoaji huduma ya maji watoe huduma hiyo kwa ufanisi na serikali ziweke mazingira ya uwazi ya utawala na usimamizi kisera.

Na hatimaye ni ubunifu ambao ripoti inasema unapaswa kupatiwa hamasa ili kusaidia serikali katika sera na kanuni.