Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maji ya kunawa mikono majumbani bado ni shida kwa mabilioni ya watu duniani

Kijana akiwa maji kutoka katika mtandao mpya wa mfumo wa maji katika kambi ya Zaa'tari huko Jordan
© UNICEF/Christopher Herwig
Kijana akiwa maji kutoka katika mtandao mpya wa mfumo wa maji katika kambi ya Zaa'tari huko Jordan

Maji ya kunawa mikono majumbani bado ni shida kwa mabilioni ya watu duniani

Afya

Takwimu mpya zinaonesha kuwa watu 3 kati ya 10 duniani kote hawakuweza kuosha mikono yao kwa maji na sabuni wakiwa nyumbani wakati wa janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19.
 

Taarifa hizo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya pamoja ya mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la afya, WHO na lile la kuhudumia watoto,  UNICEF ambapo ripoti inasema kama mwelekeo ndio huo, “mabilioni ya watu watakuwa hawana maji safi na salama na huduma za kujisafi ifikapo mwaka 2030, ukomo wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Ripoti ikipatiwa jina Maendeleo ya kaya katika kuwa na maji safi na salama ya kunywa, huduma za kujisafi na usafi mwaka 2000 hadi 2020, inawasilisha makadirio ya uwezo wa kaya kupata maji safi na salama na huduma za kujisafi katika kipindi cha miaka mitano na mwelekeo wa kufanikisha lengo namba 6 la SDGs la kuhakikisha upatikanaji na usimamizi wa maji safi na salama kwa wote ifikapo mwaka 2030.

Mwaka 2020 mtu 1 kati ya 4 hakuwa na uwezo wa kuwa na maji safi na salama nyumbani, na takribani nusu ya wakazi wa dunia hawakuwa na huduma za kujisafi.COVID-19 imeangazia umuhimu wa kuchukua hatua za dharura kuhakikisha kilamtu anaweza kunawa mikono. Janga la Corona lilipoanza mtu 1 kati ya 3 hakuweza kunawa mikono nyumbani kwake kwa kutumia maji na sabuni.”

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema kunawa mikono ni moja ya njia fanisi zaidi za kuzuia kuenea kwa COVID-19 na magonjwa mengine ya kuambukiza, “lakini bado mamilioni ya watu duniani kote hawana fursa ya kupata maji safi na salama tena kwa uhakika. Uwekezaji katika sekta ya maji na huduma za kujisafi ni lazima uwe kipaumbele iwapo tunataka kutokomeza janga hili na kujenga mifumo ya afya yenye mnepo zaidi.

Kuna mafanikio lakini bado hayatoshi

Ripoti imeonesha mafanikio katika upatikanaji wa maji safi na salama, huduma za usafi na kujisafi kwa wote, WASH.

Kati ya mwaka 2016 na 2020, idadi ya watu duniani yenye huduma hizo za maji safi na salama iliongezeka kutoka asilimia 70 hadi asilimia 74, huku ile ya huduma za kujisafi ikiongezeka kutoka asilimia 47 hadi 54 na uwezo wa kunawa mikono kwa maji na sabuni ikaongezeka kutoka asilimia 67 hadi 71.

Kwa mara ya kwanza mwaka 2020, watu wengi zaidi walitumia huduma bora za kujisafi, kama vile vyoo vya shimo na mashimo ya kuhifadhia majitaka, mfumo ambao unaweza kudhibiti taka za chooni, badala ya ile ya kuunganishwa kwenye mifereji ya majitaka. 

Ripoti inataka serikali zihakikishe kuna usadizi wa kutosha wa kusimamia huduma za majitaka katika makazi ya watu.