Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tishio la migogoro inayohusiana na maji linahatarisha maisha ya watoto milioni 190: UNICEF

Msichana mdogo nchini Zimbabwe anakunywa maji safi na salama kutoka kwenye kisima kilichorekebishwa kwa msaada wa Umoja wa Mataifa.
© UNICEF/Karin Schermbrucker
Msichana mdogo nchini Zimbabwe anakunywa maji safi na salama kutoka kwenye kisima kilichorekebishwa kwa msaada wa Umoja wa Mataifa.

Tishio la migogoro inayohusiana na maji linahatarisha maisha ya watoto milioni 190: UNICEF

Afya

Wakati viongozi wa dunia wakijiandaa kuhudhuria mkutano wa kihistoria wa maji wa Umoja wa Mataifa, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF llimetoa wito wa uwekezaji wa haraka katika huduma za maji, usafi na usafi wa mazingira (WASH) zilizo na mnepo ili kuwalinda watoto. 

Kulingana na tathimini mpya ya UNICEF “Watoto milioni 190 katika nchi 10 za Afrika wako katika hatari kubwa zaidi kutokana na mchanganyiko wa matishio matatu yanayohusiana na maji ambayo ni ukosefu wa maji ya kutosha, hudumza za usafi na usafi wa mazingira (WASH),  magonjwa yanayohusiana na maji na hatari za mabadiliko ya tabianchi.”

Shirika hilo limeongeza kuwa tishio hilo la mara tatu limegundulika kuwa baya zaidi katika nchi za Benin, Burkina Faso, Cameroon, Chad, Côte d'Ivoire, Guinea, Mali, Niger, Nigeria na Somalia, na kuifanya Afrika Magharibi na Kati kuwa miongoni mwa nchi zenye uhaba mkubwa wa maji na changamoto za mabadiliko ya tabianchi duniani.

Nchi nyingi zilizoathiriwa zaidi, hasa katika Sahel, pia zinakabiliwa na ukosefu wa amani na migogoro ya silaha, ambayo inazidisha changamotpo ya upatikanaji wa maji safi na vyoo kwa watoto.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa program wa UNICEF Sanjay Wijesekera "Afrika inakabiliwa na janga la maji. Wakati mabadiliko ya tabianchi na majanga yanayohusiana na maji yanaongezeka duniani kote, hakuna mahali popote duniani ambapo hatari zinazidi kuwa mbaya kwa Watoto kama afrika. Dhoruba, mafuriko ya kihistoria na ukame tayari vinaharibu vifaa na nyumba, yanachafua vyanzo vya maji, kunasababisha njaa na kueneza magonjwa. Lakini kwa jinsi hali ya sasa ilivyo changamoto, bila hatua za haraka, siku zijazo zinaweza kuwa mbaya zaidi."

Uchambuzi huu wa kimataifa ambao umetathimini katika ngazi ya kaya fursa za huduma za WASH, mzigo wa vifo vinavyotokana na ukosefu wa huduma za WASH miongoni mwa watoto wa chini ya umri wa miaka mitano, na kukabiliwa na hatari za mabadiliko ya tabianchi na mazingira unaonyesha ni wapi watoto wanakabiliwa na tishio kubwa na ambapo uwekezaji katika suluhu unahitajika sana ili kuzuia ulazima wa vifo zaidi.

Katika maeneo 10 yaliyo hatari zaidi, karibu theluthi moja ya watoto hawana japo huduma ya maji ya msingi nyumbani, na theluthi mbili hawana huduma za msingi za usafi wa mazingira.

Robo ya watoto hawana chaguo ila kujisaidia haja kubwa katika maeneo ya wazi. Usafi wa mikono pia ni mdogo, ambapo robo tatu ya watoto hawawezi kunawa mikono kwa sababu ya ukosefu wa maji na sabuni nyumbani.

Tathimini hiyoi inasema “Kutokana na hali hiyo, nchi hizi pia hubeba mzigo mkubwa zaidi wa vifo vya watoto kutokana na magonjwa yanayosababishwa na huduma zisizotosheleza za WASH, kama vile magonjwa ya kuhara. Kwa mfano watoto  6 kati ya 10 wamekabiliwa na milipuko ya kipindupindu katika mwaka uliopita. Ulimwenguni, zaidi ya watoto 1,000 wa chini ya miaka mitano hufa kila siku kutokana na magonjwa yanayohusiana na huduma za WASH, na karibu  Watoto 2 kati ya 5 wapo katika nchi hizi 10 pekee.”

Uchambuzi huo mpya umekuja kabla ya mkutano wa maji wa Umoja wa Mataifa wa 2023 utakaofanyika New York Marekani kuanzia tarehe 22-24 Machi. Viongozi wa dunia, mashirika husika na washiriki wengine watakutana kwa mara ya kwanza baada ya miaka 46 kukagua maendeleo ya kuhakikisha upatikanaji wa maji na usafi wa mazingira kwa wote.