Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukiona watoto wenye utapiamlo pembe ya Afrika utalia 

Ibrahim mtoto wa miezi 8 anayeugua utapiamlo akifanyiwa vipimo katika hospitali ya Moghadishu Somalia
© UNICEF/Omid Fazel
Ibrahim mtoto wa miezi 8 anayeugua utapiamlo akifanyiwa vipimo katika hospitali ya Moghadishu Somalia

Ukiona watoto wenye utapiamlo pembe ya Afrika utalia 

Msaada wa Kibinadamu

Mwaka 2011 dunia ilitangaziwa kuwepo kwa baa la njaa nchini Somalia ambapo zaidi ya watoto laki 340,000 walikuwa na utapiamlo, na ingawa mwaka huu bado baa la njaa halijatangazwa rasmi nchini humo lakini Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limesema hali ni tete na watoto zaidi ya laki 380,000 wana utapiamlo mkali ambapo hata ukiwaona watoto hao machozi yatakutoka.

Ni Rania Dagash huyo, Naibu mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF katika mahojiano maalum na Umoja wa Mataifa baada ya kukamilisha ziara yake katika pembe ya Afrika ziara ambayo anaeleza katika zaidi ya miaka 22 aliyofanya kazi hajawahi kuona Watoto wakiwa na hali mbaya kama sasa.

Dagasha anasema miaka yote ya ufanyaji kazi kusaidia watoto hajawa kulia akiwa eneo katika kituo cha kuwasaidia wahitaji lakini katika ziara hii alijikuta akilia kila sehemu aliyoenda. 

“Niliona watoto wachanga wa chini ya umri wa miezi sita ambao walikuwa wamebebwa na mama zao ambao bila shaka walikuwa wanaenda kupoteza maisha, na walikuwa wametembea nao zaidi ya kilometa 100 na huku wakiwa wamezika watoto wengine wakiwa njiani na wengine walizika Watoto wao baada ya kufika kambini. Nilimuona bibi akiwa amembeba mjukuu wa chini ya miezi sita ambaye alikuwa na utapiamlo mkali na alivimba, yani kiufupi mtoto hakuwa na uhai ndani yake na hakuweza kumpeleka kituo cha afya kupata matibabu”

Bi. Dagash anasema pamoja na kuwa hali ni mbaya kutokana na ukame ambao haujawahi kushuhudiwa sio tu nchini Somalia pekee bali katika Pembe nzima ya Afrika lakini anaamini lipo linaloweza kufanyika.

“ Tumeshawahi kufanyia kazi suala kama hili hapo awali, na tumewahi kugeuza kabisa hali iliyokuwepo ya ukame na hata sasa tunaweza kufanya hivyo iwapo tutapata rasilimali na usaidizi wakushughulikia suala hili kwa pamoja kama jumuiya ya kibinadamu na hapa namaanisha Umoja wa Mataifa na asasi za kimataifa na kitaifa ambazo ni asilimia 75 ya wadau wetu.

UNICEF inasema iwapo ulimwengu hautafungua macho na kuchukua hatua mara moja, basi kutakuwa na mlipuko wa vifo vya watoto kutokea katika Pembe ya Afrika.