Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunahitaji msaada zaidi kukabiliana na njaa hususan Vijijini Somalia: FAO

Wanawake na watoto katika kambi ya ADC ambako wakimbizi wapya wamefika Baidoa, Somalia.
UN Photo/Fardosa Hussein
Wanawake na watoto katika kambi ya ADC ambako wakimbizi wapya wamefika Baidoa, Somalia.

Tunahitaji msaada zaidi kukabiliana na njaa hususan Vijijini Somalia: FAO

Msaada wa Kibinadamu

Ingawa Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa baa la njaa limeweza kuepukwa kwa sasa nchini Somalia, Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo duniani, FAO limesema bado kuna muda wa kufanya mageuzi zaidi kuepusha kabisa baa la njaa kwa kushughulikia mahitaji ya haraka ya jamii za vijijini ambazo ni miongoni mwa walio hatarini zaidi. 

Mwakilishi wa FAO nchini Somalia Etienne Peterschmitt akizungumza na waandishi wa habari mjini Rome Italia amesema "Hali nchini Somalia bado ni mbaya. Viwango vya sasa vya usaidizi wa kibinadamu vinasaidia kuzuia matokeo mabaya zaidi, lakini havitoshi kukomesha tishio la njaa zaidi. 

Peterschmitt ameongea kuwa “Ikiwa tunataka kuzuia na sio tu kuchelewesha njaa, viwango endelevu vya usaidizi wa viwango vitahitajika hadi katikati mwa mwishoni mwa 2023 ikiwa tutazuia, sio tu kuchelewesha njaa,"

Makadirio ya waathirika mwaka 2023

Hali ya muda mrefu ya ukame isiyo na kifani imesababisha jamii za wafugaji na wakulima kushindwa kustahimili.

 Kulingana na uchambuzi uliofanywa hivi karibuni na FAO wa makadirio kati ya Mwezi Januari na Machi 2023, watu milioni 1.9 wanatarajiwa kuwa katika ngazi ya nne ya udharura wa uhitaji wa upatikanaji wa chakula IPC na idadi hiyo inatarajiwa kuongeza na kufikia watu milioni 2.7 kati ya Aprili na Juni.

Kiujumla makadirio ni takriban watu 727,000 wanaweza kukabiliwa na janga la uhaba wa chakula ifikapo Juni 2023, ikimaanisha njaa na kifo.

Jamii walio kimbia makazi yao kutokana na ukame huko Baidoa, nchini Somalia, wakusanyika karibu na Katibu Mkuu António Guterres (kofia nyeupe), ambaye yuko katika eneo hilo akiomba hatua zichukuliwe kuwasaidia.
Picha: UNSOM
Jamii walio kimbia makazi yao kutokana na ukame huko Baidoa, nchini Somalia, wakusanyika karibu na Katibu Mkuu António Guterres (kofia nyeupe), ambaye yuko katika eneo hilo akiomba hatua zichukuliwe kuwasaidia.

Waathirika wengi wako vijijini

Wanajamii ambao ni wakulima na wafugaji wa vijijini, pamoja na jamii zilizofurushwa kutoka maeneo ya vijijini, ni miongoni mwa walio katika hatari kubwa ya njaa.

FAO wameeleza watu hawa kuishi kwao kunategemea maisha ya mifugo yao na uwezo wa kupata mazoa ambayo sasa hayapo kutokana na ukame wa muda mrefu. Lishe ya watoto wao nayo imekuwa na changamoto kutokana na Wanyama kushindwa kutoa maziwa na wengine kufa kwa kiwango cha kushangaza tangu mwaka jana 2021.

“Ni muhimu kuokoa mifugo na kuwahifadhi na kuwa na afya njema kwani ndio chanzo pekee cha chakula na mapato kwa jamii nyingi za vijijini. Matokeo ya awali kutokana na utafiti katika Pembe ya Afrika yanaonesha kuwa kulisha mifugo kulipunguza hatari ya utapiamlo mkali kwa hadi 11% na ya watoto kudumaa kwa hadi 8% katika jamii za wafugaji.” Amesema Mwakilishi huyo wa FAO nchini Somalia.

Amesema msaada wa haraka ukipatikana itasaidia kupunguza gharaam kwani akitolea mfano wa mbuzi ambaye kumuhudumia ni dola 0.40 kwa kila mbuzi ikilinganishwa na dola 40 kununua mbuzi mwingine.

FAO pia imesema itaendelea kutoa chakula na chanjo kwa wanyama na kurejesha visima vya maji, sambamba na usaidizi wa fedha kusaidia watu kukidhi mahitaji yao ya kimsingi.