Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto zaidi ya milioni 1.5 wako hatarini Bangladesh kutokana na mafuriko:UNICEF 

Mvua kubwa zimepelekea miji, vijiji na miundombinu kuoshwa.
© UNICEF
Mvua kubwa zimepelekea miji, vijiji na miundombinu kuoshwa.

Watoto zaidi ya milioni 1.5 wako hatarini Bangladesh kutokana na mafuriko:UNICEF 

Msaada wa Kibinadamu

Zaidi ya watoto milioni 1.5 wako katika hatari kubwa ya magonjwa yatokanayo na maji, kuzama na utapiamlo kutokana na mafuriko makubwa yaliyolikumba eneo la Kaskazini-Mashariki mwa Bangladesh imeonya taarifa iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.  

Shirika hilo limesema liko tayari kushirikiana na Serikali na wadau wengine wasio wa serikali kuchukua hatiua kukidhi mahitaji ya dharura ya usalama, afya, lishe, maji safi na elimu kwa watoto na familia zao. 

Zaidi ya watu milioni nne katika wilaya tano za Kaskazini Mashariki mwa Bangladesh za Sylhet, Sunamganj, Habiganj, Netrokona na Maulvibazar wameathiriwa na mafuriko makubwa.  

Sylhet na Sunamganj zimeathirika zaidi, huku maji yakitiririka juu ya viwango vya hatari.  

Ardhi ya kilimo na miundombinu muhimu, ikijumuisha vituo vya umeme na shule, vimezama. 

Hatari ya magonjwa ya mlipuko 

Zaidi ya watu milioni 4 Kaskazinimashariki mwa Bangladesh wameathiriwa na mafuriko.
© UNICEF
Zaidi ya watu milioni 4 Kaskazinimashariki mwa Bangladesh wameathiriwa na mafuriko.

Kwa mujibu wa UNICEF visa vya kuhara, maambukizo ya magonjwa ya kupumua, na magonjwa ya ngozi tayari vimeripotiwa.  

Takriban watoto watatu wameshafariki dunia baada ya kupigwa na radi. 

Mamia ya shule zimefungwa na hivyo kuhatarisha zaidi elimu ya watoto. Baada ya miezi 18 ya kufungwa kwa shule kutokana na janga la COVID-19 katika miaka michache iliyopita, na sasa watoto wanakosa tena elimu. 

"Uharibifu wa maisha, nyumba na shule ni wa kusikitisha. Katika janga hili, kama ilivyo kwa wengine wengi, watoto ndio walio hatarini zaidi. UNICEF iko tayari kulinda watoto na kukidhi mahitaji yao ya dharura, kusaidia Serikali na kufanya kazi kwa karibu na washirika wetu wa ndani,” amesema Bwana. Sheldon Yett, mwakilishi wa UNICEF nchini Bangladesh. 

 Ameongeza kuwa UNICEF inasaidia serikali ya Bangladesh kukabiliana na mafuriko kwa kusambaza maji safi, vifaa vya usafi, maziwa kwa ajili ya matibabu ya lishe na vifaa vya kujifunzia.  

UNICEF pia inafanya kazi kwa karibu na idara ya huduma za jamii ili kuhakikisha kuwa wafanyikazi wa kijamii wanasimama tayari kulinda uhai na usalama wa watoto.  

Pia suala la kuelimisha jamii kuhusu hatari ya Watoto kuzama linapewa kipaumbele katika hatua za msaada zinazoendelea.