Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto milioni 3.5 wanahitaji haraka maji ya kunywa kufuatia mafuriko Bangladesh:UNICEF

Watu milioni nne wakiwemo watoto milioni 1.6 wamekwama kutokana na mafuriko nchini Bangladesh na sasa wanahitaij msaada wa dharura
© UNICEF/Mukut
Watu milioni nne wakiwemo watoto milioni 1.6 wamekwama kutokana na mafuriko nchini Bangladesh na sasa wanahitaij msaada wa dharura

Watoto milioni 3.5 wanahitaji haraka maji ya kunywa kufuatia mafuriko Bangladesh:UNICEF

Msaada wa Kibinadamu

 Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF limesema leo kwamba mafuriko yaliyolikumba eneo la Kaskazini mashariki mwa Bangladesh yameongeza zahma wiki iliyopita katika hali ya watoto ambayo tayari ilikuwa mbaya. 

 

Shirika hilo katika taarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis linasema kwa wakati huu, watoto milioni 3.5 wanahitaji haraka majisafi na  salama ya kunywa. 

"Hiyo ni idadi kubwa ya watoto ikiwa ni milioni mbili zaidi ya siku chache zilizopita. Sehemu kubwa za eneo hilo ziko chini ya maji kabisa na hazijaunganishwa na mfumo wa maji safi na salama ya kunywa na mahitaji muhimu ya chakula. Watoto wanahitaji msaada haraka hivi sasa,” amesema Sheldon Yett, mwakilishi wa UNICEF nchini Bangladesh. 

Ameongeza kuwa hatua za kuzuia magonjwa yatokanayo na maji ni jambo muhimu sana kwani “Watoto wako katika hatari kubwa katika hali hii ya kukata tamaa. Visa vya kuhara na magonjwa mengine hatari vinaongezeka kwa kasi huku visa 2,700 vimerekodiwa kufikia Jumanne wiki hii.” 

Kwa mujibu wa UNICEF asilimia 90 ya vituo vya afya katika tarafa ya Sylhet vimefurika, na huduma za chanjo ya watoto zimekatizwa, huku zaidi ya shule 5,000 na vituo vya kujifunzia vikizama. 

Pia amesema miundombinu mingine ya msingi kama barabara imebomolewa au kusambaratishwa na mafuriko hayo na hivyo kuongeza hofu ya changamoto kwa juamii ambazo nyingi tayari zimekuwa zikiishi kwa kutegemea msaada kama vile jamii za wakimbizi na wenyeji wanaowahifadhi.