Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya Gaza ni zahma juu ya zahma: Mashirika ya UN

Msichana mdogo amelazwa katika hospitali ya Al-Quds huko Gaza.
© UNICEF/Eyad El Baba
Msichana mdogo amelazwa katika hospitali ya Al-Quds huko Gaza.

Hali ya Gaza ni zahma juu ya zahma: Mashirika ya UN

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa leo yameeielezea hali inayoendelea Gaza siku 105 baada ya kuzuka vita mpya baina ya wapiganaji wa Hamas na vikosi vya Israel, kuwa ni zahma juu ya zahma. Watu zaidi ya milioni 1.7 wametawanywa huku hofu ya milipuko ya magonjwa, janga la njaa na vifo zaidi likitawala.

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO linaonya juu ya mlipuko wa magonjwa ya kuambukiza Gaza watu zaidi ya milioni 1.7 waliotawanywa hivi sasa wanaishi katika makazi ya dharura yaliyofurika pomoni na kwa wastani watu 500 wanatumia choo kimoja huku watu zaidi ya 2000 wakitumia bafu moja kuoga na wakati mwingine kwenye baadhi ya makazi ya dharura hakuna choo kabisa.

Msichana mwenye umri wa miaka 11 ameketi kwenye vifusi vya nyumba huko Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.
© UNICEF/Eyad El Baba
Msichana mwenye umri wa miaka 11 ameketi kwenye vifusi vya nyumba huko Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Kusambaa kwa magonjwa 

Hivyo shirika hilo linasema ukosefu wa vyoo na huduma za usafi vimewalazimisha watu kujisaidia haja kubwa kwenye maeneo ya wazi na kuongeza hatari kubwa ya kusambaa kwa magonjwa ya kuambukiza. 

Tangu katikati ya kwezi Oktoba mwaka jana WHO inasema kumekuwa na makali ya wagonjwa wa kuhara, matatizo ya njia ya mfumo wa hewa, chawa, upele, tetekuanga, homa ya manjano na hata homa ya ini aina ya E.

"Sehemu kubwa ya wakazi wa Gaza  watu ambao wamejeruhiwa na kushambuliwa kwa mabomu wanahitaji msaada wa haraka wa matibabu," amesema afisa wa WHO akibainisha kuwa kituo cha matibabu cha Nasser Medical Complex huko Khan Younis kina madaktari wawili tu waliobaki katika idara yake ya dharura ikilinganishwa na madaktari 24 kabla ya vita na kuna vitanda 14 pekee vya wagonjwa mahututi leo, idadi ikipungua kutoka vitanda 45 na kuna wauguzi wanne pekee waliopatikana kutoka 20 waliokuwa hapo awali.

Karibu watu 25,000 wameuawa tangu kuanza kwa mzozo

Ikiunga mkono hofu ya hali ya Gaza, ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, imeonyesha wasiwasi mkubwa kutokana na ripoti kwamba karibu watu 25,000 wameripotiwa kuuawa, kulingana na wizara ya afya ya Gaza. Asilimia 70 kati ya hao wanaaminika kuwa wanawake na watoto na angalau wengine 61,500 wamejeruhiwa, huku "maelfu kadhaa zaidi wamefukiwa chini ya vifusi, wengi wakidhaniwa kuwa wamekufa".

OHCHR inasema ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaendelea katika ukanda huo na mkuu wa ofisi ya haki za binadamu kwenye eneo linalokaliwa la Gaza Ajith Sunghay mbaye yuko Gaza tangu Jumatatu anasema “Nimewaona wanaume na watoto wakifukua vifusi kupata matofali ya kujengea mahema ya mifuko ya plastiki, huli ni janga kubwa la haki za binadamu na janga kubwa lililosababishwa na binadamu. Gaza inahitaji ongezeko la misaada ya kibinadamu ikiwemo ulinzi.”

Ameongeza kuwa kukatika kwa mawasiliano ya simu kwa siku nyingi kumeendelea, hali ambayo "inaongeza mkanganyiko na hofu kwani inawazuia Wagaza kupata huduma na habari juu ya wapi wanapaswa kuhamia.

Wapiganaji wa ulinzi wa raia wa Palestina wakitafuta manusura katika vifusi vya jengo baada ya mashambulizi ya anga katika Ukanda wa Gaza. (Maktaba)
WHO
Wapiganaji wa ulinzi wa raia wa Palestina wakitafuta manusura katika vifusi vya jengo baada ya mashambulizi ya anga katika Ukanda wa Gaza. (Maktaba)

"Ni mazingira ya jiko linalochemka hapa, katikati ya machafuko makubwa, kutokana na hali mbaya ya kibinadamu, uhaba, na hofu iliyoenea na hasira", ameongeza afisa huyo wa OHCHR kabla ya kuelezea jinsi "mashambulio makubwa ya mabomu katika Gaza ya Kati na Khan Younis" yalivyokuwa akisema "inaonekana wazi na inasikika hasa kwa Rafah wakati wa usiku".

Baada ya kuwasili Gaza siku ya Jumatatu, Bwana Sunghay alisema kwamba walikuwa wakisikia mlipuko wa mabomu wakati mwingine mara kadhaa kwa saa. Wakati wa usiku ulikuwa "wakati wa kutisha zaidi, wakati wa mabomu, kwa watu wa Gaza” amebainisha, na kuongeza kwamba zaidi ya raia 100 bado wanashikiliwa mateka katika eneo hilo, ambao "hawaonekani na ambao kwa hakika husikia sauti sawa na kuhisi hofu sawa".

Hakuna mawasiliano Gaza

Katika tarifa yake ya hivi karibuni kuhusu mzozo huo, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura, OCHA imerejea kuelezea wasiwasi mkubwa kwamba operesheni salama na yenye ufanisi ya misaada "popote pale Gaza ni changamoto na imeathiriwa pakubwa na vikwazo vya Israel vya kuagiza vifaa muhimu, ikiwa ni pamoja na vifaa vya mawasiliano vinavyofaa".

Imeongeza kuwa leo ni siku ya tano mfululizo huduma za mawasiliano zimekatwa Gaza na hali hii inazuia maelfu ya watu kupata tarifa za kuokoa maisha, kukosa fursa ya kuwapigia wahudumu wa afya kupata msaada na inaendelea kuathiri usambasaji wa msaada wa kibinadamu unaohitajika sana.