Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu milioni 18 Sahel kukabiliwa na njaa kali miezi mitatu ijayo:OCHA/CERF 

Mkulima katika ukanda wa Sahel ikiwemo Chad wanachangamoto katika kilimo.
© WFP/Giulio d'Adamo
Mkulima katika ukanda wa Sahel ikiwemo Chad wanachangamoto katika kilimo.

Watu milioni 18 Sahel kukabiliwa na njaa kali miezi mitatu ijayo:OCHA/CERF 

Msaada wa Kibinadamu

Watu wapatao milioni 18 kwenye Ukanda wa Sahel barani Afrika watakumbwa na njaa kali na kutokuwa na uhakika wa chakula katika kipindi cha miezi mitatu ijayo ikiwa ni idadi kubwa zaidi tangu mwaka 2014 limeonya leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA. 

Taarifa ya shirika hilo iliyotolewa mjini Geneva Uswisi inasema kwenye ukanda wa Sahel, watoto milioni 7.7 walio chini ya umri wa miaka 5 wanatarajiwa kukumbwa na utapiamlo, kati yao milioni 1.8 wana utapiamlo mkali.  

“Na ikiwa shughuli za misaada hazitaongezwa, idadi hii inaweza kufikia milioni 2.4 ifikapo mwisho wa mwaka huu” limeonya shirika hilo. 

 “Familia zote katika Sahel ziko kwenye ukingo wa kutumbukia katika njaa. Mchanganyiko wa ghasia, ukosefu wa usalama, umaskini mkubwa na bei ya juu ya chakula vinazidisha utapiamlo na kuwafanya mamilioni ya watu kuishi maisha magumu. Ongezeko la hivi majuzi la bei za vyakula linalochochewa na mzozo kati ya Urusi na Ukraine linatishia kugeuza mgogoro wa uhakika wa chakula kuwa janga la kibinadamu. Tusipochukua hatua sasa, watu wataangamia.” Amesisitiza Martin Griffiths, mkuu wa OCHA

Wanawake wanachimba mabwawa ya katikati ya mwezi ili kuokoa maji nchini Niger.
©FAO/ Giulio Napolitano
Wanawake wanachimba mabwawa ya katikati ya mwezi ili kuokoa maji nchini Niger.

Hali ni ya kutisha 

Kwa mujibu wa OCHA hali imefikia viwango vya kutisha nchini Burkina Faso, Chad, Mali na Niger, ambapo karibu watu milioni 1.7 watakabiliwa na dharura ya uhaba wa chakula wakati wa msimu wa muambo kati ya Juni na Agosti.  

Kiwango cha dharura kitaalam kinachojulikana kama IPC daraja la 4  “ni hali ambapo kaya hupata pengo kubwa katika milo yake huku kukiwa na viwango vya juu vya utapiamlo na vifo vinavyohusiana na njaa na ambapo familia zinalazimika kuuza, kwa mfano, zana zao za kilimo na mali nyingine wanazohitaji ili kuendesha maisha na riziki zao.” 

Dola milioni 30 zimetolewa na CERF kusaidia 

Ili kusaidia kukidhi mahitaji ya dharura ya uhakika wa chakula na lishe ya watu, OCHA imetoa dola milioni 30 kutoka mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa  CERF kwa ajili ya kusaidia nchi hizo nne, zikiwemo dola milioni 6 kwa Burkina Faso na dola milioni 8 kila nchi ambazo ni Chad, Mali na Niger.  

CERF ni mfuko ambao hukusanya fedha kutoka kwa wafadhili mapema, ili fedha hizo ziruhusu mashirika ya kibinadamu kutoa msaada wa awali, wa kuokoa maisha popote pale matatizo yanapotokea huku wakingoja ufadhili wa ziada. 

Mchango huu wa hivi karibuni unafanya jumla ya karibu dola milioni 95 ya fedha za ufadhili zilizotolewa na CERF kwa Sahel tangu mwanzoni mwa mwaka huu ikijumuisha mgao wa hivi karibuni kwa nchi za Mauritania (dola milioni 4) na Nigeria (dola milioni 15). 

"Hakuna wakati wa kupoteza. Maisha yako hatarini, mchango huu wa fedha utasaidia mashirika ya kibinadamu kuongeza hatua za dharura ili kusaidia kuzuia janga kubwa. Sio mbadala, hata hivyo, kwa michango mikubwa zaidi ya wafadhili tunayohitaji itatusaidia kudumisha hatua zetu na kusaidia kujenga jamii zenye uthabiti.” Amesema Griffiths. 

Mapema mwaka huu, jumuiya ya kibinadamu ilizindua maombi sita ya kibinadamu katika Ukanda wa Sahel ya jumla ya dola bilioni 3.8 ili kutoa msaada katika kanda nzima kwa mwaka 2022.  

Hata hivyo, ikiwa karibu katikati ya mwaka, maombi hayo yamefadhiliwa chini ya asilimia 12 pekee.