Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chad yahitaji haraka dola Zaidi ya milioni 4.7 kunusru mamilioni ya watu:OCHA

Leo nchini Chad kuna takriban watu 657,000 waliofurushwa makwao asilimia 51 ni wanawake na wasichana.
OCHA/Naomi Frerotte
Leo nchini Chad kuna takriban watu 657,000 waliofurushwa makwao asilimia 51 ni wanawake na wasichana.

Chad yahitaji haraka dola Zaidi ya milioni 4.7 kunusru mamilioni ya watu:OCHA

Msaada wa Kibinadamu

Hali ya kibinadamu nchini Chad inasalia kuwa tete huku watu milioni 4.3 wakihitaji haraka msaada wa kibinadamu kuweza kunusuru maisha yao kutokana na njaa. 

Hayo ni kwa mujibu wa ripota iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA.

Taarifa hiyo inasema machafuko, watu kutawanywa na ukosefu wa huduma muhimu vimeathiri kwa kiasi kikubwa mnepo wa jamii ambazo tayari watu wake wako kwenye hatihati.

OCHA inasema mashirika ya misaada ya kibinadamu yanashirikiana na serikali ya CHAD kukabiliana na mgogoro uliopo na kuhakikisha watu wanaohitaji msaada wanafikiwa, lakini usalama mdogo na ukosefu wa fedha ndio changamoto kubwa.

Jumuiya ya kimataifa nchini Chad imetoa ombi la dola milioni 476.6 ili kuweza kuwafikia watu milioni 2 wanaohitaji msaada Zaidi wakati huu kukiwa na kiwango kikubwa cha kutokuwa na uhakika wa chakula, utapiamlo, watu kutawanywa na maradhi mengine.

OCHA inasema matatizo yote haya yakijumuishwa yameongeza zahma kwa mamilioni ya watu ambao tayari wanakabiliwa na maendeleo duni na umasikini unaoathiri mnepo wa jamii zao. Kwamujibu wa mratibu wa OCHA nchini Chad Stephen Tull “Usugu wa mgogoro wa kibinadamu Chasd unahitaji pia uimarishaji wa uwezo wa kukabiliana na hali na kuwekeza zaidi katika hatua za kuzuia na kudhibiti hatari na zahma nyingine kutokea.” Mpango huo unaenda sanjari na mkakati wa 2017-2019 ambao unaruhusu kufikia mahitaji ya haraka ya kibinadamu huku ukibaini na kutoa muongozo kwa pande husika katika kutanabahi miziz ya mahitaji ya kibinadamu ambayo yamewaweka hatarini watu Zaidi ya milioni 7.5.”

Ongezeko la mgogoro wa njaa

Ingawa hali ya kutokuwa na uhakika wa chakula imeongezeka kwa asilimia 18 mwaka 2019 , kutokana na msimu mzuri wa kilimo watu waliosalia bila uhakika wa chakula wanakadiriwa kuwa milioni 3.7 nchini Chad huku  milioni 2.2 wana utapiamlo ikiwa ni ongezeko la asilimia 29 ukilinganisha na mwaka jana kipindi kama hiki. Na inakadiriwa kuwa watu milioni 3.7 hawatakuwa na uhakika wa chakula Chad wakati wa msimu wa muambo (Juni-Agosti 2019) na miongoni mwa watu hao zaidi ya 519,000 watakabiliwa na tatizo kubwa la kutokuwa na uhakika wa chakula.

OCHA inasema changamoto ya utapiamlo ni kubwa kwani linawakabili Watoto 350,000 ambao ni ongezeko la asilimia 59 ukilinganisha na mwaka jana.

 

Janga la kibinadamu inasalia kuwa tete huku watu milioni 4.3 wakihitaji msaada wa kibinadamu
OCHA/Naomi Frerotte
Janga la kibinadamu inasalia kuwa tete huku watu milioni 4.3 wakihitaji msaada wa kibinadamu

Matarajio finyu kwa wanaotaka kurejea nyumbani

Kuna watu zaidi ya 665,000 waliotawanywa nchini Chad huku wengine wakiendelea kufungasha virago na kuhama makwao kwenye jimbo la Lac kutokana na vita vinavyoendelea.Zaidi yah apo matarajio ya wakimbizi wengi kurejea nyumbani kutokea Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR na Sudan yanasalia kuwa finyu kutokana na machafuko yanayoendelea na kutokuwepo kwa usalama katika nchi watokako. Hivi leo Chad kuna watu 657,000 waliotawanywa na asilimia 51 ni wanawake na wasichana. Kati yao 450,000 ni wakimbizi au waomba hifadhi na 124,000 ni wakimbizi wa ndani. Kati ya wakimbizi hao 51,000 wamerejea katika vijiji vyao na 81,000 ni raia wa Chad wanaorejea. Hali ya watu kutawanywa inaleta mzigo mkubwa kwa jamii zinazowahifadhi ambazo tayari zinahaha kuweza kuishi.

Idadi kubwa ya vifo duniani

Chad ndio nchi yenye idadi kubwa ya vifo duniani ikisababishwa na mchanganyiko wa mambo yakiwemo kutofanya kazi kwa mfumo wa afya ,maendeleo duni, umasikini uliotapakaa, kiwango kidogo cha watu kupata chanjo,kukosa huduma za afya kwa watu Zaidi ya milioni 2wakiwemo Watoto wa umri wa chini ya miaka mitano , wa mama wajawazito, wa mama wanaonyonyesha na wakimbizi wa ndani na wafugaji wa kuhamahama. Surua inaendelea kuathiri wilaya 39 kati ya 1117 nchini humo.

OCHA inasema licha ya Ushahidi wa mahitaji yote haya  mpango wa usaidizi wa mwaka jana umefadhiliwa chini ya asilimia 53 ya fedha zilizohitajika kukidhi mahitaji.