Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya watoto wenye utapiamlo Sahel imefurutu ada: UNICEF

Mama akiwa kando mwa mtoto wake alie lala akiwa na utapiamlo
UNICEF/UN055334/Tremeau
Mama akiwa kando mwa mtoto wake alie lala akiwa na utapiamlo

Idadi ya watoto wenye utapiamlo Sahel imefurutu ada: UNICEF

Msaada wa Kibinadamu

Zaidi ya watoto milioni moja kupokea matibabu ya dharura kutokana na utapiamlo kwa mwaka 2018, na wito wa uwekezaji kuepuka zahama hii mwaka 2019 umetolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Kwa mujibu wa UNICEF watoto zaidi ya milioni 1.3 wenye umri wa chini ya miaka mitano wanaohitaji matibabu ya dharura kutokana na utapiamlo uliokithiri katika nchi sita za Afrika zilizoko kwenye Ukanda wa Sahel, watapata huduma hiyo mwaka 2018. 

Shirika hilo linasema hii ni idadi kubwa zaidi kwa takribani muongo mmoja na ni ongezeko la asilimia 50 la idadi ya watoto walio na utapiamlo ikilinganishwa na mwaka 2017 nchini Burkina Faso, Chad, Mali, Mauritania, Niger na Senegal.

Katika mwanzo wa mwaka huu UNICEF ilikadiria kwamba hadi watoto milioni 1.6 katika nchi hizo sita za Sahel walikuwa hatarini kupata utapiamlo uliokithiri.

Katika kukabiliana na hali hiyo UNICEF imechukua hatua haraka za kufikisha misaada ya kuokoa maisha na madawa kwa ufadhili wa kitengo cha Muungano wa Ulaya cha ulinzi kwa raia na msaada wa operesheni za kibinadamu, ECHO na wadau wengine.

Akifafanua kuhusu ukubwa wa janga hilo mkurugenzi wa kanda ya Magharibi na Katikati mwa Afrika wa UNICEF, Marie-Pierre Poirier amesema“Utapiamlo ni jinamizi linalowazogoma watoto eneo zima la Sahel, na mwaka 2018 hali imekuwa mbaya zaidi, tumeweza kufikisha misaada na madawa kwa watoto wanaoihitaji zaidi kuweza kuishi, lakini umuhimu kama huo unahitajika katika uwekezaji hususani kwenye njia za kuzuia na kubaini mapema ili kuepusha watoto kuugua na kupoteza maisha, huu ndio mwelekeo tuliouchukua mwaka huu na umeanza kuzaa matunda.

Pia amesema UNICEF imekuwa ikichukua hatua ili kusaidia janga hili lisiongezeke zikiwemo kusaidia kubaini mapema maradhi hayo, kuwapima watoto wote walio chini ya umri wa miaka mitano wakati wa kampeni, kuwapa msadaa wa mazoezi ya kihisia na kimwili watoto walioko hospitali ili wapone haraka, kuhimiza kuingizwa sera za vita dhidi ya utapiamlo kwenye mkakati wa kitaifa wa afya ya umma na kuelimisha jamii.