Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa miji  Afrika umeanza Kisumu kuchagiza jukumu la miji katika kutimiza ajenda 2030:UNHABITAT 

Moja ya mitaa ya mji mkuu wa Rwanda, Kigali
UN/Rick Bajornas
Moja ya mitaa ya mji mkuu wa Rwanda, Kigali

Mkutano wa miji  Afrika umeanza Kisumu kuchagiza jukumu la miji katika kutimiza ajenda 2030:UNHABITAT 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mkutano wa 9 wa miji barani Afrika umeanza leo katika mji wa Kisumu nchini Kenya kwa lengo la kuchagiza umuhimu na jukumu la miji ya ukubwa wa kati barani humo. 

Mkutano huo wa siku tano unaofanyika kila baada ya miaka 3 kwenye miji tofauti Afrika umeandaliwa kwa ushirikiano wa shirika la makazi la Umoja wa Mataifa UN-HABITAT, serikali ya Kenya, baraza la magavana Kenya na kaunti ya Kisumu.  

Mkutano huo umewaleta pamoja viongozi wa serikali na miji mbalimbali kwa lengo la kuendeleza ugatuzi wa madaraka na utawala wa ndani pia kushughulikia maswali makubwa yanayotokana na utekelezaji wa dira ya 2063 ya Afrika na ajenda ya maendeleo endelevu ya mwaka 2030 katika upande wa ukuaji wa miji. 

Mkurugenzi mtendaji wa UN-HABITAT Maimunah Mohd Sharif atatoa hotuba katika ufunguzi wa mkutano huo akisisitiza  kuhusu umuhimu wa kutekeleza ajenda mpya ya miji barani Afrika na hitaji la hatua mahususi kama ilivyojadiliwa katika mkutano wa ngazi ya juu kuhusu ajenda mpya ya miji kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 28 Aprili 2022.  

Ameongeza kuwa “Kupitishwa kwa programu za makazi nafuu na mkakati wa miji kujikwamua baada ya maafa na mazingira ya migogoro inaweza kuharakisha maendeleo na kusaidia serikali kufikia malengo ya kimataifa yaliyowekwa na Ajenda ya 2030.” 

Huko Kisumu pia , UN-HABITAT inaandaa jukwaa la maonyesho ili kuonyesha umuhimu wake barani Afrika na kuwaalika washiriki kuendelea na majadiliano katika kikao kijacho cha Kumi na Moja  ambacho ni jukwaa la miji duniani linalotarajiwa kuanzia tarehe 26 hadi 30 Juni 2022 huko Katowice, Poland.