Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mataifa ya Kiafrika yanaongoza kwenye mageuzi ya mifumo ya chakula: Guterres

Mkimbizi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati anayeishi Cameroon akiwaandalia wateja wake chakula.
UN Women/Ryan Brown
Mkimbizi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati anayeishi Cameroon akiwaandalia wateja wake chakula.

Mataifa ya Kiafrika yanaongoza kwenye mageuzi ya mifumo ya chakula: Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Nchi za Kiafrika ziko katika msitari wa mbele kwenye mabadiliko muhimu ya mifumo ya chakula ili kushughulikia kwa wakati mmoja masuala ya uhakika wa chakula, lishe, ulinzi wa kijamii na mazingira yote hayo wakati zikijenga mnepo amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa leo Alhamisi. 

António Guterres ameasema hayo wakati akihutubia katika ufunguzi wa mdahalo wa ngazi ya juu wa sera kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani, ambao ni sehemu ya msururu wa mazungumzo kuhusu Afrika mwaka 2022, ulioitishwa ili kuimarisha uthabiti katika usambazaji wa chakula kwenye bara zima la afrika wakati ambapo miongo kadhaa ya maendeleo dhidi ya njaa yanabadilishwa. 

Muungano wa kina 

 

Guterres amesema kwa muda mrefu sana, lishe, uhakika wa chakula, migogoro, mabadiliko ya tabianchi, mifumo ya ikolojia na afya imekuwa ikichukuliwa kama changamoto tofauti, "lakini changamoto hizi za ulimwengu zina uhusiano mkubwa. Migogoro huleta njaa. Changamoto ya mabadiliko ya tabianchi inazidisha migogoro, na matatizo ya kimfumo yanazidi kuwa mabaya zaidi.” 

Amebainisha kuwa baada ya zaidi ya muongo mmoja wa maboresho, Mwafrika 1 kati ya 5 alikuwa na lishe duni mwaka 2020, huku watoto milioni 61 wa Afrika wakiathiriwa na udumavu. Wanawake na wasichana hubeba mzigo huo, na chakula kinapokuwa haba, “mara nyingi wao huwa wa mwisho kula na wa kwanza kufukuzwa shuleni na kulazimishwa kufanya kazi au kuingia kwenye ndoa.” 

Bwana Guterres amesema kuwa wasaidizi wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa na washirika wake wamekuwa wakifanya kila wawezalo ili kukidhi mahitaji ya Afrika huku kukiwa na mzozo, lakini misaada "haiwezi kushindana na vichochezi vya kimfumo vya njaa." 

Ameongeza kuwa "Mishtuko mingine ya nje imekuwa ikizidisha hali hiyo, kama vile kujikwamua kwa usawa kutoka kwenye janga la COVID-19 na vita nchini Ukraine, huku nchi za Kiafrika zikiwa kati ya zilizoathiriwa zaidi na uhaba wa nafaka na madeni yanayoongezeka.” 

Vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi 

 

Kujenga mbepo pia kunahitaji kushughulikia janga la mabadiliko ya tabianchi 

"Wakulima wa Kiafrika wako mstari wa mbele katika sayari yetu ambayo ina ongezeko la joto, kuanzia kuongezeka kwa joto hadi ukame na mafuriko," amesema Katibu Mkuu. 

Ameongeza kuwa "Afrika inahitaji kuimarishwa kwa kiasi kikubwa kwa usaidizi wa kiufundi na kifedha ili kukabiliana na athari za dharura za mabadiliko ya tabianchi na kutoa umeme mbadala katika bara zima." 

Ameendelea kusema kwamba nchi zilizoendelea lazima zitimize ahadi zao za ufadhili dhidi ya mabadiliko ya tabianchi wa dola bilioni 100 kwa nchi zinazoendelea, kwa msaada wa taasisi za kifedha za kimataifa, ili nchi za Kiafrika, haswa, ziwekeze katika ahueni ya kujikwamua kutoka kwenye janga la COVID-19, katika suala la nishati mbadala. 

Mifumo ya chakula, amesema Katibu Mkuu, "inaunganisha changamoto hizi zote", kama ilivyoangaziwa katika mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mifumo ya chakula uliofanyika mwezi Septemba mwaka uliopita. 

"Nchi nyingi wanachama wa Afrika ziliongoza wito wa mabadiliko ya kimsingi, kupitia njia za mageuzi shirikishi, ambazo zinalenga kushughulikia wakati huo huo uhakika wa chakula, lishe, ulinzi wa kijamii, uhifadhi wa mazingira na kujenga mnepo wa kuhimili mishtuko." 

Amekaribisha uamuzi wa Muungano wa Afrika (AU) wa kutenga mwaka 2022 kama mwaka wa lishe ahadi ya kufanyia kazi ahadi kubwa zilizotolewa katika mkutano huo. 

Utaalamu wa pamoja 

 

“Kupitia ushirikiano wa kitaifa, kikanda na kimataifa, ni lazima ttuendeleze yale tuliyojifunza na kutumia utaalamu wa pamoja. Kwa pamoja, lazima tufanikishe njia hizi”, amesisitiza Bwana Guterres. 

Jumuiya ya kimataifa lazima ichukue nafasi yake aesema akiongeza kwamba , “kupunguza msaada wakati mahitaji ni ya juu sana, hilo sio chaguo." 

Usaidizi rasmi wa maendeleo, au ODA, kulingana na asilimia ya fedha za umma zilizopo, ni muhimu zaidi kuliko hapo awali, amesema Katibu Mkuu. 

"Ninazihimiza nchi zote kuonyesha mshikamano, kuwekeza katika kujenga mnepo na kuzuia mzozo wa sasa usizidi kuongezeka." 

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema katika ziara yake ya hivi karibuni nchini Senegal, Niger na Nigeria, ametiwa moyo na ujasiri na azma ya watu aliokutana nao. 

"Wanawake na vijana haswa wamejitolea kupata suluhisho la kudumu, endelevu ambalo linawawezesha kuishi kwa amani na majirani zao na asili. Ikiwa tutafanya kazi pamoja, ikiwa tutaweka watu na sayari mbele ya faida, tunaweza kubadilisha mifumo ya chakula, kufikia Malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) na kutomwacha mtu nyuma." 

Katibu mkuu amehimiza kwamba malengo muhimu ya kumaliza njaa na utapiamlo ifikapo muda wa mwisho unaokaribia haraka wa mwaka 2030, ni ya kweli, na yanayoweza kufikiwa. 

Amemalizia kwa kuliambaia bara la Afrika kwamba "Umoja wa Mataifa uuko samabamba nayi katika, kila hatua."