Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza kuu la UNHABITAT laanza Nairobi likijikita na miji endelevu kwa ajili ya kutimiza SDGs

Bustani ya kijani kibichi katika miji inachagiza matokeo chanya kwa bioanuwai, hali ya hewa, ustawi na ubora wa hewa.
© Unsplash/Nerea Martí Sesarin
Bustani ya kijani kibichi katika miji inachagiza matokeo chanya kwa bioanuwai, hali ya hewa, ustawi na ubora wa hewa.

Baraza kuu la UNHABITAT laanza Nairobi likijikita na miji endelevu kwa ajili ya kutimiza SDGs

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mkutano wa pili wa Baraza Kuu la shirika la Umoja wa Mataifa la makazi UNHABITAT umeanza leo mjini Nairobi Kenya ukibeba maudhui “Mustakabali endelevu wa miji kupitia ujumuishwaji na na ufanisi wa ushirikiano wa kimataifa: kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu wakati wa majanga ya kimataifa.”

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Baraza hilo mkurugenzi mtendaji wa UNHABITAT Maimunah Mohd Sharif ametaja mada kuu zitakazojadiliwa katika mkutano wa Baraza hilo zitajikita katika mada zifuatazo

Fursa ya ufikiaji wa nyumba za bei nafuu kwa wote: Nchi Wanachama zinahimizwa kuchunguza mbinu za kufikia haki ya kimataifa ya makazi ya kutosha na kuelekea kwenye kuondoa vizuizi vilivyopo kwa nyumba zagharama nafuu.

Hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi mijini: Ili kufikia dhamira ya kimataifa ya kusalia ndani ya kikomo cha nyuzi joto 1.5˚C kwenye viwango vya joto vinavyoongezeka ifikapo mwaka wa 2030, nchi wanachama wa shirika hilo zinahimizwa kuchunguza njia halisi mijini kwa ajili ya kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Kujikwamua na changamoto za mijini: UNHABITAT inasema migogoro ya sasa inazidi kuongezeka mijini, na miji mara nyingi hutumika kama sehemu kuu za kuwasili kwa watu waliotawanywa.

Nchi wanachama zinahimizwa kuwezesha miji kukabiliana na changamoto za mijini na kuunga mkono juhudi za kitaifa za kujikwamua.

Ujanibishaji wa SDGs: Baraza hilo kuu pia litaangalia hatua za ndani zinazohitajika ili kuendeleza utekelezaji wa SDGs ili kufikia malengo ya ajenda ya maendeleo ya 2030.

Nchi Wanachama pia zitaalikwa kuchunguza mifumo ya kifedha ili kuhakikisha rasilimali zinaelekezwa kwenye maendeleo ya miji na kufikia viwango vya ndani.

Ustawi na fedha za ndani: ili kuharakisha kufikiwa kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs, kukabiliana na majanga ya mijini, kuendeleza hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi mijini, na kuhakikisha makazi ya kutosha na ya gharama nafuu kwa wote, miji inahitaji sera na rasilimali za kifedha.

Nchi wanachama pia zimealikwa kuchunguza sera na taratibu za soko ili kuhakikisha mtiririko wa fedha unaoelekezwa kwa maendeleo ya mijini na kufika katika ngazi ya mashinani.

Miji ni kiini cha hadithi ya ubinadamu

Katika ujumnbe wake wa video kwa mkutano wa Baraza hilo kuu la UNHABITAT Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema “Miji ni kitovu cha hadithi ya ubinadamu. Kupitia sehemu kubwa ya historia yetu, imesukuma maendeleo. Maamuzi yaliyochukuliwa ndani ya miji yameamua njia yetu, mawazo na ubunifu ulioanzia katika miji umeunda ulimwengu wetu na leo, jukumu lake ni muhimu zaidi kuliko wakati mwingine wowote.”

Ameongeza kuwa ni kwa sababu Baraza kuu la UNHABITAT linakutana wakati Dunia ikiwa imeghubikwa na majanga lukuki, ikiwemo “Kuongezeka kwa ukosefu wa usawa, viwango vya joto duniani na matokeo yake ni janga. Pia madeni yanadhoofisha uchumi wa nchi zinazoendelea hadi kikomo huku tukiwa nusu ya tarehe ya mwisho ya Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu, tunawaacha zaidi ya nusu ya ulimwengu nyuma. Na coronavirus">COVID-19 imeleta athari mbaya katika kupunguza umaskini.”

Zaidi ya watu bilioni 1 wanaishi katika ufukara

Katibu Mkuu ameendelea kusema kwamba hivi sasa zaidi ya watu bilioni moja bado wanaishi katika vitongoji duni wakisukumwa kwenda mijini si kwa sababu ya kazi na fursa, kama zamani, lakini ukosefu wa huduma mahali pengine.

Hata hivyo amesema “Bado kuna kuna fursa ya kubadili mwelekeo huu. Lakini ili kufanya hivyo lazima tupiganie mustakbali tunazotaka. Mustakabali unaotarajiwa katika SDGs, ajenda mpya ya mijini, na mkataba wa Paris.”

Kwani amesema “miji ni uwanja muhimu wa vita. Miji inazalisha asilimia 70 ya hewa chafu duniani, nusu ya binadamu wote duanini wanaishi mijini na kufikia mwaka 2050, zaidi ya watu bilioni mbili zaidi watapaita mijini nyumbani.”

Ajenda ya pamoja

Guterres amesema ripoti yake ya “Ajenda Yetu ya Pamoja,” inatoa wito wa kuimarishwa upya na umoja wa kimataifa zaidi,  kutambua jukumu muhimu la miji na mamlaka nyingine za mitaa katika kushughulikia changamoto zinazoikabili dunia hivi sasa.

Ushirikiano kama huo wa kimataifa amesema ni muhimu katika kusaidia miji kutekeleza jukumu lake

Ni muhimu kuhakikisha fedha, taarifa na usaidizi unapatikana ili kuwezesha miji kuwa na mnepo, jumuishi na endelevu.

Ushirikiano wa kimataifa lazima uunge mkono miji kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, kuendeleza upatikanaji wa nyumba za gharama nafuu, na kuweka mikakati ya ndani inayohitajika ili kufanya SDGs kuwa kweli.

“Nina hakika kwamba Baraza hili la Umoja wa Mataifa la makazi litaendeleza malengo haya, ikiwa ni pamoja na kupitia tamko lenu la mawaziri. Kwa pamoja, tunaweza kufikia mustakabali endelevu wa miji tunaohitaji ili kujenga ulimwengu wenye amani, ustawi na afya kwa wote.”

Baraza hili kuu hukutana kila baada ya miaka minne. Ni chombo cha juu zaidi duniani cha kufanya maamuzi juu ya ukuaji endelevu wa miji na makazi ya watu.