Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kituo cha ushirika wa miji kupambana na mabadiliko ya tabianchi chanzinduliwa:UNHABITAT 

Mkurugenzi mtendaji wa UN-HABITAT Maimunah Mohd Sharif akihutubia baraza la shirika la makazi la Umoja wa Mataifa UN-HABITAT jijini Nairobi Kenya.
Julius Mwelu/UN-Habitat
Mkurugenzi mtendaji wa UN-HABITAT Maimunah Mohd Sharif akihutubia baraza la shirika la makazi la Umoja wa Mataifa UN-HABITAT jijini Nairobi Kenya.

Kituo cha ushirika wa miji kupambana na mabadiliko ya tabianchi chanzinduliwa:UNHABITAT 

Tabianchi na mazingira

Shirika la makazi la Umoja wa Mataifa UNHABITAT na washirika kadhaa wa kitaifa na kimataifa wamezindua kituo cha kwanza cha ushirikiano wa miji cha UN-Habitat ili kusaidia uundaji wa miundo ya kujenga uwezo kwa mamlaka za mitaa, wasanifu majengo, watendaji na wajasiriamali. 

UNHABITAT inasema kituo hicho Urban Living Lab, kilichozinduliwa leo kwenye mkutano wa 9 wa miji barani Afrika utakaofunga pazia kesho Jumamosi Mei 21 mjini Kisumu Kenya kimeandaliwa kwa pamoja na taasisi ya teknolojia ya Massachusetts (MIT), Chuo kikuu cha ufundi cha Berlin (TUB) na taasisi ya Wuppertal, na kitakuza uwezo wa kisera na kupanga mipango miji, kuboresha uwezo wa mamlaka za miji kupata ufadhili na kusaidia mikakati ya ufadhili, kusaidia uchukuaji wa miundo bunifu ya biashara na makampuni na wmiradi inayochipukia katika maeneo ya washirika. 

Kituo hicho, kilichoanzishwa na mradi wa Urban Pathways unaofadhiliwa na mradi wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi wa Serikali ya Ujerumani (IKI), tayari kimeanza  kuweka maabara hizo hai kote ulimwenguni katika miji kama Nairobi Kenya, Belo Horizonte Brazili na Quito Ecuador. 

Maendeleo ya miji ni majaribio ya ubunifu 

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo hicho mkuu wa UNHABITAT Bi. Maimunah Mohd Sharif  amesema "Tunaelewa miji kama sehemu za majaribio kwa uvumbuzi. Miji huleta pamoja akili angavu, uongozi wa kisiasa na uchumi imara na wa ubunifu. Kupitia kutekeleza dhana ya Living Labs, tunatumai kuimarisha jukumu la miji ili iweze kutumia kikamilifu uwezekano wa ukuaji endelevu”. 

Amesisitiza kuwa “Tunafurahia sana fursa ya kuunda suluhu pamoja na washirika mbalimbali wanaohusika, kwa kuwa tunaamini kwamba Living Labs ni mahali pa majaribio katika mazingira halisi ya maisha, pale ambapo suluhisho zinapangwa na kutekelezwa.” 

Mkuu huyo wa shirika la makazi la Umoja wa Mataifa ameendelea kusema kwamba mabadiliko ya miji kuelekea maendeleo endelevu na shirikishi ni lengo kuu la ajenda mpya ya miji.  

“Kuna uwezekano mkubwa wa kuboresha ufikiaji wa mijini, ubora wa hewa, usalama na ubora wa maisha katika miji pamoja na kupunguza uzalishaji wa gesi ya kuharibu mazingira ikiwa mbinu jumuishi za sera zitatumika ambapo zitachanganya maeneo yote ya kuingilia kati kwa sera ya miji na kuhusisha wadau wengi wa umma na binafsi.” Ameongeza 

Kwa mujibu wa UNHABITAT kuunganisha sekta muhimu na watendaji ni hatua muhimu kuelekea mbinu jumuishi ambayo husaidia kuondoa mifumo ya hewa ukaa mijini na kuwa na miji ambayo watu wanaweza kuishi na kufikiwa na wote. Kujaribu suluhu za kibunifu katika maabara zilizo hai mijini kunaweza kuwa hatua muhimu limesema shirika hilo. 

Limeongeza kuwa mafunzo yanayopatikana kutokana na majaribio kama haya yanaweza hapo baadaye kuhamishiwa katika hatua za juu za sekta ya umma au ya kibinafsi, ambayo ni hatua muhimu kuelekea mabadiliko makubwa yanayohitajika.  

UNHABITAT inasema ushirikiano huo utaanza na miradi inayofadhiliwa na mpango wa kimataifa wa hali ya hewa (IKI) kama vile njia za mjini na fursa  kuharakisha upatikanaji wa suluhisho za usafiri wa miji kupitia  mbinu za kidijitali pamoja na miradi inayofadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya kama vile SOLUTIONSplus na Suluhu bora za nishati kwa Afrika (SESA). 

Na katikia hatua itakayofuata pia itawafikia wafadhili wengine muhimu ili kuongeza ushirikiano kati ya miradi na kukuza ufanisi katika jitihada za kuongeza hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kukuza maendeleo endelevu.