Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa mafunzo wa ILO wawainua wafanyabiashara Turkana magharibi, Kenya

Mmiliki wa duka akiwa dukani  katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya
Picha/UN-Habitat/Julius Mwelu
Mmiliki wa duka akiwa dukani katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya

Mradi wa mafunzo wa ILO wawainua wafanyabiashara Turkana magharibi, Kenya

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani, ILO limeendesha programu ya kutoa mafunzo ya stadi za kuendesha biashara kwa jamii zinazowahifadhi wakimbizi hususan wakazi wa Kakuma, kaunti ya Turkana nchini Kenya kwa kutambua changamoto za maendeleo zinazokabili jamii zinazohifadhi wakimbizi kufuatia ujio wa wakimbizi. 

Huyo ni Michael Emuria kutoka kaunti ya Turkana magharibi eneo la Kakuma na yeye ni mfanyabiashara mdogo kabisa katika eneo hilo na ni mmiliki wa kampuni ya ujenzi na uwasilishaji wa bidhaa. Tayari yeye amepata mafunzo muhumi ya ukuzaji biashara kutoka kwa ILO. “Mwaka jana wakati tulipata ajira kutoka kwa ILO kupitia taasisi ya Kenya ya barabara na teknolojia ya ujenzi KHIBT tulijenga barabara kutoka a1 hadi kituo cha Luma. Tulipata mafunzo kwa wiki tatu kutoka kwa ILO na KHIBT na tulifundishwa ni namna gani tunaweza kukarabati barabara kwa kutumia nguvu kazi ya watu hapa badala ya kutumia mashine.” 

Aidha walipatiwa mafunzo kuhusu kufuatilia fedha kwa kufanya hesabu za biashara ili kutofautisha matumizi, faida na hasara katika biashara. “Awali wakati tulikuwa tukipata tenda na kulipwa hatukufanya hesabu ya kufahamu faida ni ipi na tulichukua malipo yote kama ni faida lakini baada ya mafunzo tulipata uelewa kwamba tunahitaji kutoa matumizi na faida na hata katika faida hiyo jinsi ya kusimami fedha zetu.” 

Lakini hali sasa imebadilikwa kwani Emuria amewekeza kiasi cha faida katika duka ambapo anasema, “tumepanua mawazo yetu na ndio maana katika kipindi cha miezi kadhaa ijayo tutakuwa na duka kubwa zaidi kwa sababu tumepewa mafunzo na tumewezeshwa ili kupanga kwa ajili ya mustakabali wetu na sio sasa tu ili wakati ILO na KHIBT wakija tena watashuhudia mabadiliko na kuona kwamba waliwezesha watu wa Turkana magharibi.”