Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hii si sahihi! Asema Mkuu wa OCHA baada ya kujionea hali halisi Turkana 

Wakazi wa kaunti ya Turkana nchini Kenya ambako kunashuhudiwa ukame na ukosefu wa uhakika wa chakula.
UN News/ Thelma Mwadzaya
Wakazi wa kaunti ya Turkana nchini Kenya ambako kunashuhudiwa ukame na ukosefu wa uhakika wa chakula.

Hii si sahihi! Asema Mkuu wa OCHA baada ya kujionea hali halisi Turkana 

Msaada wa Kibinadamu

Ulimwengu umesahau madhila ya ukame wanayopitia watu wa Turkana, mvua haijanyesha Turkana.Tumeshuhudia misimu minne ya mvua zisizotabirika. Ni kauli ya Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura, Martin Griffiths baada ya kujionea hali halisi kwenye kaunti ya Turkana nchini Kenya hii leo. 

Kenya, Somalia, na Ethiopia ni mataifa matatu ya Pembe ya Afrika yaliyokumbwa na ukame uliosababisha watu wasiopungua milioni 15 kukubwa na na uhaba mkubwa wa chakula na maji. 

Akiwa Turkana Bwana Griffiths amesema, “watu aamepoteza mifugo yao na hawana chakula wala maji. Kina mama hawa ambao ni jasiri wamelazimika kupitisha maamuzi magumu.Lomupus inahitaji juhudi na mchango wetu.” 

Utapiamlo sugu 

Takwimu zinaashiria kuwa watu milioni 3.5 nchini Kenya wanakabiliana na uhaba mkubwa wa chakula na utapia mlo sugu umewaathiri baadhi kwa zaidi ya maradufu katika kipindi cha dharura. Hilo limesababishwa na ukame mkali zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia. 

Rhoda Wesite Langai ni Mratibu wa wadi katika eneo la Lomopus na anakiri kuwa njaa imewaathiri kina mama kwani, “hata hawajisumbui kupanga uzazi kwani njaa inawaumiza.Wakitumia mbinu za uzazi wa mpango na hawana chakula watakufa,” anaelezea. 


Njaa na uzazi wa mpango 

Kulingana na utafiti,kiwango cha chakula kwenye kaunti za maeneo ya ukame na kavu kilipungua kwa kiasi kikubwa tangu katika kipindi cha miezi mitatu ya mwisho ya mwaka 2021 kwasababu ya mvua chache za msimu wa vuli. 

Hali hiyo ilisababisha uhaba mkubwa wa chakula katika miezi ya mwanzo wa 2022.Kipindi kirefu cha ukame na uhaba wa chakula kimewafanya watoto wasiopungua nusu milioni kuwa na utapia mlo sugu. 

Iyanei Kebe ni mama wa watoto wanane. Hali ya watoto watatu wa mwisho ni mbaya kiafya. Analazimika kuuza fagio za ukili ili kukidhi mahitaji ya kila siku ila soko limeharibika. 

“Watoto wamekonda kwasababu ya kukosa chakula.Serikali ya kaunti wala mashirika ya msaada hawajatufikia,” analalamika. Mwanawe wa kwanza aliye na umri wa miaka 20 alipata mimba kabla ya kuolewa na kwa sasa ana mtoto mdogo wa umri wa miezi 8. Analazimika kumnyonyesha ijapokuwa afya yake mwenyewe sio nzuri. 

Mto Turkwel kaunti ya Turkana nchini Kenya.
UN News/Thelma Mwadzaya
Mto Turkwel kaunti ya Turkana nchini Kenya.

Mto Turkwel na usalama duni 

Mto Turkwel uko umbali wa kilomita 7 hivi kutokea vijiji vya Lomuputh na Kangatotha ila wakaazi hawawezi kuhamia sehemu za ukingoni yaliko maji kwasababu ya usalama duni. 

Ili kukimu mahitaji ya maji wanalazimika kutembea mwendo huo kila siku ili kupata maji ya matumizi. Wanafunzi wanalazimika pia kubeba maji wanapokwenda shuleni ndipo waweze kupata mlo angalau mmoja kwa siku. 

Juhudi za dharura 

Mratibu wa misaada ya kibinadamu na dharura katika Umoja wa mataifa, UNOCHA,Martin Griffiths alipata fursa ya kujionea ana kwa ana hali mbaya wanayokabiliana nayo wakazi wa Turkana na kusema, “hali hii si sahihi. Mtoto ameweza kuhimili maisha na kuingia shule ya sekondari, lakini ili aweze kwenda lazima malipo, na malipo ni lazima mama auze mbuzi na mbuzi hakuna. Hili ni kosa.” 

Wanakijiji walimsihi awaletee misaada ili waubwage mzigo wa njaa na maafa ya mifugo. Ziara ya Mkuu huyu wa OCHA Martin Griffiths aliyoanza leo tarehe 12 mwezi Mei inatamatika kesho tarehe 13 Mei 2022.