Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Aliyoyashuhudia Martin Griffiths Kenya yamtisha, atoa wito wa haraka 

Wakazi wa kaunti ya Turkana nchini Kenya ambako kunashuhudiwa ukame na ukosefu wa uhakika wa chakula.
UN News/ Thelma Mwadzaya
Wakazi wa kaunti ya Turkana nchini Kenya ambako kunashuhudiwa ukame na ukosefu wa uhakika wa chakula.

Aliyoyashuhudia Martin Griffiths Kenya yamtisha, atoa wito wa haraka 

Msaada wa Kibinadamu

Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura, Martin Griffiths, akihitimisha ziara ya siku mbili nchini Kenya ambapo alijionea athari mbaya ya msimu wa nne mfululizo wa mvua bila mvua katika Pembe ya Afrika. 

Taarifa iliyotolewa jana Jumapili na OCHA jijini Nairobi, Kenya, imemnukuu Griffiths akisema, "wakati wa ziara yangu, nilikutana na watu katika kijiji cha Lomopus katika Kaunti ya Turkana, Kenya, na nikazungumza na watu waliokimbia makazi yao huko Doolow, Somalia, na pia eneo la Korehey katika Mkoa wa Somalia wa Ethiopia. Kila mmoja wa watu niliozungumza nao walikuwa wazi: shida hii inatishia maisha yao na njia yao ya maisha. Wanahitaji umakini na hatua za ulimwengu. Sasa.” 

Ukame katika eneo la Pembe ya Afrika tayari umeathiri zaidi ya watu milioni 18 kote Ethiopia, Somalia na Kenya, ikiwa ni pamoja na watu wasiopungua milioni 16.7 wanaoamka na njaa kila siku na hawajui mlo wao ujao utatoka wapi. Idadi hii inatarajiwa kuongezeka katika wiki zijazo, kwani msimu wa mvua wa sasa (ambao hudumu kutoka Machi hadi Mei) umekuwa wa chini ya wastani, na kufanya ukame huu kuwa mrefu zaidi katika Pembe ya Afrika katika takribani miongo minne. 

Katika kijiji cha Lomopus, wanajamii walimwambia Bwana Griffiths kwamba huu ndio ukame mbaya zaidi ambao wamekumbana nao katika kumbukumbu zao. Familia nyingi zimepoteza mifugo yao na zinahangaika kuishi. Wale wanaoweza kununua chakula wanagawana vifaa vyao duni na majirani zao, wakati wengi wanakula tu matunda ya mawese. Watoto katika kijiji hicho wanategemea mpango wa Serikali wa chakula shuleni kupata mlo mmoja kwa siku, kwani mara nyingi nyumbani hakuna chakula. Katika shule hiyo wanafunzi walieleza kuwa baadhi ya wanafunzi wenzao wamelazimika kuacha shule kutokana na kushindwa kulipa karo huku baadhi ya wasichana wakifukuzwa shule na wazazi wao kuolewa. 

"Tumekuwa tukipiga kengele juu ya shida hii, na tukimsihi yeyote anayeweza kuchangia, kwa miezi mingi." amesema Bwana Griffiths na kuongeza akisema kuwa anawashukuru wafadhili weo kwa ahadi zao za kusaidia kukabiliana na ukame katika Pembe ya Afrika. “Lakini ukweli ni kwamba tumepitwa na wakati: ikiwa hatutapokea ufadhili mpya mara moja ili kuongeza shughuli za kibinadamu, tunakabiliwa na matarajio ya upotezaji mkubwa wa maisha katika kipindi kijacho.” 

Katika ziara yake, mkuu huyo wa masuala ya kibinadamu pia alikutana na maafisa wa Serikali ya Kenya, ambao alijadili nao jinsi Serikali inavyokabiliana na ukame, pamoja na hitaji muhimu la kuchukua hatua za kuokoa maisha leo, ikiambatana na msaada kwa jamii zilizoathiriwa na ukame ili kukabiliana na hali hiyo na kustawi katika siku zijazo. 

Akihitimisha, Bwana Griffiths amesema, “ikiwa nina ujumbe mmoja kwa ulimwengu, ni kutosahau watu wa Lomopus na wengine kote katika ukanda ambao wanahitaji sana msaada wetu. Watu hawa ni sura ya kibinadamu ya janga la tabianchi duniani, ambao hawajafanya chochote kusababisha hali hii. Ni lazima tujitokeze na kusimama katika mshikamano nao kabla hatujachelewa.”