Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulio katika shule Ukraine, viongozi UN walaani vikali

Hivi karibuni, shule moja huko Kharkiv, kaskazini-mashariki mwa Ukraine, iliharibiwa baada ya kushambuliwa kwa makombora. Shule nyingine imeshambuliwa tarehe 7 Mei 2022
© UNICEF/Kristina Pashkina
Hivi karibuni, shule moja huko Kharkiv, kaskazini-mashariki mwa Ukraine, iliharibiwa baada ya kushambuliwa kwa makombora. Shule nyingine imeshambuliwa tarehe 7 Mei 2022

Shambulio katika shule Ukraine, viongozi UN walaani vikali

Amani na Usalama

Taarifa iliyotolewa hii leo mjini New York Marekani, imeeleza namna Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alivyosikitishwa na shambulio lililoripotiwa tarehe 7 Mei ambalo lilipiga shule huko Bilohorivka, Luhansk nchini Ukraine, ambapo watu wengi walikuwa wakitafuta makazi kutokana na mapigano yanayoendelea. 

Taarifa hiyo iliyotolewa na Stéphane Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu wa UN imeeleza shambulio hili ni ukumbusho mwingine kwamba katika vita hii, kama katika migogoro mingine mingi, ni raia wanaolipa gharama kubwa zaidi. 

Kupitia taarifa hiyo, Katibu Mkuu amerejelea wito wake kwamba raia na miundombinu ya kiraia lazima iepushwe wakati wa vita. Vita hii lazima iishe, na amani ianzishwe kwa kuzingatia Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa. 

“Umoja wa Mataifa na wadau wake wa nchini Ukraine wataendelea kusaidia wale ambao maisha yao yameharibiwa na vita.” Taarifa imeeleza. 

Watoto  

Kwa upande wake shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, limelaani vikali shambulio hilo huku kukiwa na ripoti kwamba raia, wakiwemo watoto, walikuwa waliathiriwa na shambulio hilo walikuwa wametafuta hifadhi katika chumba cha chini cha shule hiyo.  

Tweet URL

Kupitia ukurasa rasmi wa Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Catherine Russell ambaye ndiye mkuu wa shirika hilo, hii leo Jumapili ameandika akisema, "bado hatujui ni watoto wangapi wanaweza kuwa wameuawa au kujeruhiwa katika shambulio la bomu lililoripotiwa, lakini tunahofia shambulio hili limeongeza mamia ya watoto ambao tayari wamefariki dunia katika vita hii. Familia ambazo zilinaswa na shambulio hili zilipaswa kusherehekea Siku ya Mama leo huko Ukraine, sio kuomboleza kupoteza wapendwa wao.”  

Bi. Russell ameongeza kusema kuwa, "shule hazipaswi kamwe kushambuliwa au kutumiwa kwa madhumuni ya kijeshi. Kuwalenga raia na vitu vya kiraia, ikiwa ni pamoja na shule, ni ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu. Shambulio hili la hivi punde ni moja tu ya matukio mengi katika vita hiii ambapo tumeona kupuuzwa kwa wazi. maisha ya raia.” 

170 waokolewa Mariupol 

Aidha Bwana Guterres, Jumapili hii ametoa tamko la pili akikaribisha kuwasili kwa kundi jipya la zaidi ya raia 170 katika eneo la Zaporizhzhia wakitokea katika viwanda vya chuma vya Azovstal na maeneo mengine ya Mariupol. 

Operesheni iliyofanikiwa ya kuwahamisha watu iliratibiwa na UN na Kamati ya Kimataifa ya Chama cha Msalaba Mwekundu (ICRC). 

"Fikra zangu ziko pamoja na watu wote nchini Ukraine wanaoteseka katika vita hivi." Amenukuliwa Bwana Guterres katika taarifa hiyo fupi iliyotolewa jioni Jumapili saa za Marekani.  

Operesheni ya sasa inafanya kufikia watu zaidi ya 600 ambao wamehamishwa kwa usalama kutoka katika kiwanda cha chuma cha Azovstal na maeneo mengine ya Mariupol.