Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu wa umoja wa Mataifa amteua Catherine M. Russell kuwa bosi mpya wa UNICEF

Catherine M. Russell akizungumza katika Mkutano wa Kimataifa wa Ujasiriamali jijini Nairobi,
US State Department
Catherine M. Russell akizungumza katika Mkutano wa Kimataifa wa Ujasiriamali jijini Nairobi,

Katibu Mkuu wa umoja wa Mataifa amteua Catherine M. Russell kuwa bosi mpya wa UNICEF

Masuala ya UM

Kufuatia mashauriano na Bodi ya Utendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametangaza leo kumteua Catherine M. Russell raia wa Marekani kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF .

Russelle anarithi nafasi ya Henrietta H. Fore wa Marekani ambaye amestaafu uongozi wa shirika hilo.

Katibu Mkuu amemshukuru Bi Fore kwa uongozi wake wa UNICEF na jukumu muhimu la UNICEF katika masuala ya utafiti, janga la COVID-19 na elimu.

“Kutokana na uongozi wake, UNICEF sasa ni shirika lenye safu zaidi ya ubia wa sekta ya umma na binafsi inayolenga kufikiria Malengo ya Maendeleo Endelevu.” Amesema Guterres.

Bi. Russell ambaye kwa sasa anahudumu kama Msaidizi wa Rais na Mkurugenzi wa Ofisi ya Utumishi wa wafanyakazi wa Ikulu anashika nafasi hiyo ya juu ya UNICEF akiwa na miongo kadhaa ya uzoefu katika kuunda sera ya kibunifu ambazo zimewezesha jamii ambazo hazijahudumiwa ipasavyo kote ulimwenguni, kuunda programu zenye matokeo makubwa ya kuwalinda wanawake na wasichana, ikijumuisha katika majanga ya kibinadamu, kuwajenga, kuwainua na kusimamia nguvu kazi mbalimbali; na kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali na uungwaji mkono wa kisiasa kwenye maeneo mbalimbali.

Bi. Russell ambaye emehudumu sehemu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya kazi na aliyekuwa rais wa Marekani Barack Obama ana Shahada ya Kwanza ya Sanaa katika Falsafa, kutoka Chuo cha Boston na shahada ya Udaktari kutoka Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha George Washington.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta H. Fore akutana na wanafunzi wa Shule ya Roberto Suazo Córdoba, huko Tegucigalpa, Honduras
UNICEF/Bindra
Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta H. Fore akutana na wanafunzi wa Shule ya Roberto Suazo Córdoba, huko Tegucigalpa, Honduras

Pongezi kutoka UNICEF

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotumwa na UNICEF imesema wanakaribisha tangazo hilo la uteuzi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres leo kwamba Catherine M. Russell atamrithi Henrietta H. Fore kama Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore amesema hana shaka UNICEF na watoto duniani watakuwa katika mikono salama chini ya uongozi huu mpya.

"Catherine Russell ataleta utajiri wa utaalamu katika kazi ya UNICEF, na nina furaha kumkabidhi mtu mwenye ujuzi wake, uzoefu, mapenzi ya dhati kwa watoto na wanawake,"

Akaribishwa na Bodi ya UNICEF

Naye  Rytis Paulauskas, Balozi wa Lithuania katika Umoja wa Mataifa na Rais wa bodi tendaji ya UNICEF amesema “Ninamkaribisha Catherine Russell kwa uchangamfu na ninatazamia kufanya kazi naye. Atapata uungwaji mkono kikamilifu na bodi ya UNICEF katika kutekeleza jukumu hili muhimu la uongozi,”

Bi. Russell anatarajiwa kuchukua majukumu yake mapya mapema mwakani akiwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa nane wa UNICEF, na mwanamke wa nne kuongoza shirika hilo lenye watu 20,000 katika historia yake ya miaka 75.