Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto milioni 559 duniani kote wanataabika na joto kali kwa sasa, idadi itaongeza na kufikia zaidi ya bilioni 2 mwaka 2050.

Mtoto mwenye umri wa miaka 11 akijipatia ahueni ya joto kali kwa kucheza kwenye chemchem ya maji huko  Uzbekhstan
UNICEF/Pirozzi
Mtoto mwenye umri wa miaka 11 akijipatia ahueni ya joto kali kwa kucheza kwenye chemchem ya maji huko Uzbekhstan

Watoto milioni 559 duniani kote wanataabika na joto kali kwa sasa, idadi itaongeza na kufikia zaidi ya bilioni 2 mwaka 2050.

Tabianchi na mazingira

Kuelekea mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP27utakaofanyika nchini Misri barani Afrika, shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya watoto UNICEF wametoa ripoti ya kuonesha athari za mabadiliko ya tabianchi kwa watoto katika kipindi cha kuanzia sasa mpaka mwaka 2050.

Ripoti hiyo ya UNICEF iliyozinduliwa leo jijini New York Marekani imeonesha kuwa watoto milioni 559 kwa sasa wanakabiliwa na joto Kali na hali inategemewa kuwa mbaya zaidi ambapo mpaka kufikia mwaka 2050 watoto wote duniani ambao wanakadiriwa kuwa bilioni 2.02 watakuwa wameathiriwa na mawimbi tofauti ya joto kali bila kujali wapo kusini au kaskazini mwa dunia na vile vile bila kujali ongezeko la joto litakuwa katika kiwango cha wastani wa nyuzi joto 1.7 katika kipimo cha Selsiyasi au kiwango cha juu cha nyuzi joto 2.4 katika kipimo cha Selsiyasi.

Ripoti hiyo iitwayo Mwaka wa baridi zaidi katika maisha yao yote: kuwalinda watoto kutokana na athari zinazoongezeka za misimu ya joto imeangazia athari ambazo tayari zimedhihirika kwa watoto na kuonesha kuwa hata katika maeneo ambayo kuna viwango vidogo vya joto katika kipindi cha miongo mitatu athari za jua haziwezi kuepukika.

Watoto wengi zaidi wataathirika

Ripoti hiyo iliyotolewa na UNICEF ni ushirikiano baina yake na shirika jingine liitwalo The Data for Children Collaborative ambapo akizungumza kuhusu ripoti hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell amesema wakati joto linazidi kuongezeka kuna athari pia ya ongezeko la zebaki. "Tayari, mtoto 1 kati ya 3 anaishi katika nchi ambazo zinakabiliwa na hali ya joto kali na karibu mtoto 1 kati ya 4 wanakabiliwa na misimu mikubwa ya joto, na hali itazidi kuwa mbaya zaidi.”

Russell amesema watoto wengi zaidi wataathiriwa na misimu ya joto kwa muda mrefu, joto litakuwa Kali zaidi na litatokea mara kwa mara katika miaka thelathini ijayo hali inato tishia afya na ustawi wao.

Mkuu huyo wa UNICEF amesema juhudi za kupambana na mabadiliko ya tabianchi ndio zitakazo amua mustakabali wa watoto duniani “Hali ya mabadiliko yatakuwa mabaya kwa kiasi gani itategemea hatua zitakazochukuliwa sasa, serikali lazima ziweke kikomo cha joto duniani kwa haraka hadi kufikia nyuzi joto 1.5 na kupatikane ufadhili wa kukabiliana na hali hii ifikapo mwaka 2025. Hii ndiyo njia pekee ya kuokoa maisha na mustakabali wa watoto, na mustakabali wa sayari dunia.”

Jimboni Sindh nchini Pakistan, mama akijaribu kumkinga mwanae dhidi ya jua kali.
UNDP/Hira Hashmey
Jimboni Sindh nchini Pakistan, mama akijaribu kumkinga mwanae dhidi ya jua kali.

Nini kifanyike

Ripoti hiyo ya UNICEF imependekeza mambo makuu manne yanayopaswa kufanyiwa kazi kwa haraka na serikali:-

Serikali kuwalinda watoto dhidi ya uharibifu wa hali ya hewa kwa kufanya marekebisho kwenye huduma za kijamii. Kila nchi lazima ibadilishe huduma muhimu za kijamii ambazo ni maji, usafi wa mazingira na usafi (WASH), afya, elimu, lishe, ulinzi wa kijamii na ulinzi wa mtoto - ili kulinda watoto na vijana. UNICEF imesema katika mkutano wa COP27 utakao fanyika wiki chache zijazo, watoto na haki zao lazima zipewe kipaumbele katika maamuzi ya kukabiliana na hali hiyo.

Serikali lazima ziandae namna ya watoto kuishi katika ulimwengu unaobadilika-badilika. Kila nchi lazima iwape watoto na vijana elimu ya mabadiliko ya tabianchi, elimu ya kupunguza hatari ya majanga, mafunzo ya ujuzi wa kijani na fursa za kushiriki kikamilifu na kushawishi uundaji wa sera za mabadiliko ya tabianchi. COP27 lazima ione nchi zikiimarisha mwelekeo wa elimu ya tabianchi ya watoto na kutekeleza ahadi za awali za kujenga uwezo wa vijana.

Serikali lazima ziweke kipaumbele kwa watoto na vijana katika utoaji wa fedha na rasilimali za mabadiliko ya tabianchi. Nchi zilizoendelea lazima zitekeleze ahadi zao walizoweka kwenye COP26 ya kuwa watafadhili wa dola bilioni 40 kwa mwaka ifikapo 2025 kwa kiwango cha chini, ikiwa ni hatua ya kuelekea kwenye kutoa angalau dola bilioni 300 kwa mwaka kwa ajili ya kukabiliana mabadiliko ya tabianchi ifikapo mwaka 2030.

Serikali lazima zijitahidi kuzuia janga la hali ya hewa kwa kupunguza kwa kiasi kikubwa utoaji wa gesi chafuzi na kuweka lengo la viwango vya Celsiasi 1.5 hai. Uchafuzi unatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 14 katika kipindi cha muongo huu, hali inayoiweka dunia katika njia ya janga lajoto duniani. Serikali zote lazima ziangalie upya mipango na sera zao za mabadiliko ya tabianchi za kitaifa ili kuongeza matamanio na hatua zaidi za kukabiliana na janga hili. Ni lazima nchi ziwe tayari kupunguza utoaji wa hewa chafuzi kwa angalau asilimia 45 ifikapo mwaka 2030 ili kuweka joto lisizidi nyuzi joto 1.5.

Maamuzi ya kuokoa watoto yapo mikononi mwa serikali

Misimu ya joto huwadhuru watoto zaidi kwani hawawezi kudhibiti joto la mwili wao ikilinganishwa na watu wazima. Kadiri watoto wanavyokabiliwa na mawimbi ya joto, ndivyo uwezekano wa kupata matatizo ya kiafya ukijumuisha magonjwa sugu ya kupumua, pumu na magonjwa ya moyo na mishipa huongezeka.

Watoto na wale wachanga wako katika hatari kubwa zaidi ya vifo vinavyotokana na joto. Misimu ya joto inaweza pia kuathiri mazingira ya watoto, usalama wao, lishe na upatikanaji wa maji, na elimu na maisha yao ya baadaye.

Huenda huu ukawa mwaka wa baridi zaidi katika maisha yetu yote

Balozi mwema wa UNICEF ambaye pia ni mwanaharakati wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi Vanessa Nakate amesema nilazima hoja ya kuendelea kupunguza, kuzuia na kukabiliana na athari zinazoweza kuepukika za mabadiliko ya tabianchi zichukuliwe kwa haraka duniani kote ili kukabiliana na ongezeko la joto duniani.

“Hali hii mbaya ya hali ya hewa inayoshitusha ya mwaka 2022 inatupa kengele ya kuziduka usingizini kuhusu hatari inayoongezeka na inayotukabili,” alisema Vanessa Nakate, na kuongeza kuwa . “misimu ya joto kali ni mfano wa wazi. Ingawa mwaka huu umekuwa wa joto katika karibu kila kona ya dunia, huenda ukawa mwaka wa baridi zaidi katika maisha yetu yote. Simu tumeshapigiwa kwenye sayari yetu na bado viongozi wetu wa ulimwengu hawajaanza kutokwa na jasho. Chaguo pekee ni sisi kuendelea kuwasha joto - juu yao - kusahihisha njia tunayoendelea.

Balozi huyo mwema wa UNICEF amesema viongozi wa dunia lazima wafanye mambo yaliyoshauriwa katika ripoti hii watakapo kutana katika COP27 kwa ajili ya watoto kila mahali, lakini hasa watoto walio katika mazingira magumu zaidi katika maeneo yaliyoathirika zaidi.  Amewakumbusha kuzingatia ripoti hiii kwakuwa imeweka wazi kwamba misimu ya joto itakuwa mikali zaidi kuliko ambayo tayari imesukudiwa kuwa.

Vanessa Nakate (mwenye fulana nyeusi) akizunguma na Mary Aspital, msimamizi wa kituo cha kijamii cha maji cha Sopel huko Kaunti ya Turkana nchini Kenya.
© UNICEF/Translieu/Nyaberi
Vanessa Nakate (mwenye fulana nyeusi) akizunguma na Mary Aspital, msimamizi wa kituo cha kijamii cha maji cha Sopel huko Kaunti ya Turkana nchini Kenya.

Joto pamoja na hewa chafu

Watoto katika kaskazini mwa dunia hususani barani Ulaya, watakabiliwa na ongezeko kubwa zaidi la misimu mikali ya joto na ifikapo mwaka 2050, karibu nusu ya watoto wote barani Afrika na Asia watakabiliwa na hali mbaya y joto kali lililokithiri.

Hivi sasa nchi 23 ziko katika kundi la juu zaidi la kuathiriwa na joto la juu la watoto na idadi hiyo ya nchi inatarajiwa kuongezeka na kufikia nchi 33 ifikapo 2050. Nchi nyingine 36 zimewekwa katika kipengele cha kuwa na uzalishaji wa juu wa hewa chafuzi.

Nchi za Burkina Faso, Chad, Mali, Niger, Sudan, Iraq, Saudi Arabia, India na Pakistan ni miongoni mwa nchi zinazoweza kusalia katika maeneo yote mawili ya juu zaidi katika matukio yote mawili ya joto Kali na hali mbaya ya hewa chafuzi.