Sahel watoto milioni 5 watahitaji msaada mwaka huu:UNICEF 

28 Januari 2020

Karibu watoto milioni 5 watahitaji msaada wa kibinadamu mwaka huu Sahel ya Kati kutokana na machafuko yanayoendelea limeonya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF likisema idadoi hiyo ni ongezeko kubwa kutoka milioni 4.3.

Kwa mujibu wa taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo idadi hiyo inatarajiwa kupanda zaidi mwaka huu wa 2020 kutokana na ongezeko la mashambulizi dhidi ya raia wakiwemo watoto nchini Burkina Faso, Mali na Niger lakini pia utekaji, na uingizaji wa watoto jeshini unaofanywa na makundi yenye silaha.

Mkurugenzi wa UNICEF wa kanda ya Afrika Magharibi  na Kati Marie-Pierre Poirier  amesema “Tunapoiangalia hali Saheli ya Kati hatuwezi kujizuia kusikitishwa na kiwango cha machafuko yanayowakabili watoto. Wanauawa, kukatwa viungo, na kufanyiwa ukatili wa kingono, na wengine mamaia kwa maelfu wamekumbana na matukio yaliyowaathiri kisaikolojia.”

Ameongeza kuwa mashambulizi dhidi ya watoto yameongezeka mwaka uliopita mfano Mali yaliorodheshwa matukio 571 ya ukiukwaji mkubwa  dhidi ya watoto katika robo ya kwanza ya mwaka 2019 ikilinganishwa na matukio 544 kwa mwaka mzima wa 2018 au 386 kwa mwaka 2017.

Msichana akimbia nje ya shle katika jamii ya Korioume nchini Mali ambako watoto wankosa vifaa muhimu vya shule. Sehemu ya shule imeshambuliwa.
@OCHA/Eve Sabbagh
Msichana akimbia nje ya shle katika jamii ya Korioume nchini Mali ambako watoto wankosa vifaa muhimu vya shule. Sehemu ya shule imeshambuliwa.

Kwa mujibu wa UNICEF tangu kuanza kwa mwaka 2019 zaidi ya watoto 670,000 katika ukanda mzima wamelazimika kukimbia makwao kwa sababu ya vita vya silaha na kutokuwepo usalama.

watoto walioathirika na machafuko Katikati mwa Sahel wanahitaji ulinzi na msaada haraka. UNICEF inatoa wito kwa serikali , vikosi vyenye silaha, makundi yenye silaha yasiyo ya serikali na pande zingine katika mzozo kuacha mara moja kushambulia watoto majumbani kwao, mashuleni au katika vituo vya afya. UNICEF inataka kuwe na fursa salama kwa watoto wote walioathirika kwa kuzingatia mingisi ya kimataifa ya kibinadamu,. Tunazitaka pande zote kulinda na kuwezesha upatikaji wa huduma za kijamii. Hii ni muhimu sana kwa jamii na itasaidia katika kuzuia migogoro.”

UNICEF imesisitiza kuwa machafuko hayo yameathiri pia elimu kwa watoto hao, upatikanaji wa huduma muhimu na kuchangia ongezeko la utapiamlo kwa watoto wa chini ya umri wa miaka mitano, na huduma za maji pia ni haba.

UNICEF imeomba dola milioni 208 ili kusaidia kutoa huduma za kibinadamu kwa Sahel ya Kati kwa mwaka huu wa 2020.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter