Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres alaani shambulio nchini Niger

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.
UN Photo/Violaine Martin (file)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.

Guterres alaani shambulio nchini Niger

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali shambulio la kikatili huko Niger ambalo limesababisha vifo vya watu 137.

Taarifa ya Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq iliyotolewa usiku wa kuamkia leo jijini New York, Marekani imesema shambulio hilo limfanywa na watu wenye silaha wasiojulikana kwenye mkoa wa Tahoua nchini Niger tarehe 21 mwezi huu wa Machi.

“Katibu Mkuu anatuma salamu zake za rambirambi kwa familia za waliouawa pamoja na serikali na wananchi wa Niger huku akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi wa shambulio hilo,” imesema taarifa hiyo.
 
Katibu Mkuu pia ametoa wito kwa mamlaka nchini Niger kufanya jitihada zote ili kubaini na kuwafikisha mbele ya sheria watekelezaji wa shambulilo hilo huku ikiimarisha pia ulinzi wa raia.

Bwana Guterres amerejelea pia tamko lake la mshikamano na serikali na watu wa Niger katika juhudi zao za kukabiliana na kuzuia ugaidi kwenye eneo hilo sambamba na misimamo mikali yenye ghasia na uhalifu wa kupangwa.

Amesihi nchi za ukanda wa Sahel kuendeleza jitihada zao kwa ushirikiano wa karibu na taasisi za kikanda na wadau wa kimataifa ili kushughulikia vitisho vya usalama na utulivu kwenye ukanda huo wa Sahel na kwingineko.