Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampeni ya chanjo ya Ebola imeanza nchini DRC kukabili mlipuko mpya:WHO 

Timu inayofadhiliwa kwa msaada wa UNICEF kwa ajili ya kusafisha nyumba Mbandka kunakoshukiwa aliishi mtu aliyekuwa na Ebola.
© UNICEF/Mulala Josué
Timu inayofadhiliwa kwa msaada wa UNICEF kwa ajili ya kusafisha nyumba Mbandka kunakoshukiwa aliishi mtu aliyekuwa na Ebola.

Kampeni ya chanjo ya Ebola imeanza nchini DRC kukabili mlipuko mpya:WHO 

Afya

Kampeni ya chanjo dhidi ya Ebola imeanza kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, ili kukomesha kusambaa zaidi kwa mlipuko mpya wa ugonjwa huo nchini humo, ambapo tayari umeanza kuenea. 

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO leo lilisema kwamba watu sasa wamechanjwa huko Mbandaka, mji mkuu wa jimbo la Equateur magharibi. 

Kampeni hiyo ya chanjo inafuatia vifo vya watu wawili kutokana na Ebola tangu 21 Aprili.  

Zaidi ya watu 230 waliowasiliana kwa karibu na marehemu hao wametambuliwa na kufuatiliwa na timu tatu za chanjo zitafanya kazi kuwafikia walio katika hatari zaidi, limesema shirika la WHO. 

Mtazamo chanya kuhusu mlipuko huo 

"Tukiwa na chanjo zinazofaa na uzoefu wa wafanyikazi wa sekta ya afya wa DRC katika kukabiliana na Ebola, tunaweza kubadilisha haraka mkondo wa mlipuko huu na kuwa  na hali bora," amesema Dkt Matshidiso Moeti, mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika.  

Ameongeza kuwa "Tunaunga mkono nchi katika nyanja zote muhimu za kukabiliana na dharura ya Ebola ili kulinda na kuokoa maisha ya watu." 

Congo DRC imeshuhudia milipuko 14 ya Ebola tangu mwaka 1976 na sita tangu mwaka 2018. 

Kwa msaada kutoka WHO, washirika wengine na wafadhili, nchi imekuwa mtaalam katika kukabiliana na Ebola, limebainisha shirika hilo la Umoja wa Mataifa la afya. 

Msaada wa kuokoa maisha 

Takriban dozi 200 za chanjo ya rVSV-ZEBOV ya Ebola zimesafirishwa hadi Mbandaka kutoka mji wa mashariki wa Goma na dozi zaidi zitatolewa siku zijazo. 

Chanjo hiyo inatolewa kulingana na mkakati wa pete, ambapo watu waliothibitishwa kuwasiliana na mgonjwa wa ebola na waliowasiliana na watu hao, hupokea chanjo, pamoja na wahudumu wa mstari wa mbele na wafanyikazi wa afya. 

Mbali ya kampeni ya chanjo, kituo cha matibabu ya Ebola chenye vitanda 20 kimeanzishwa huko Mbandaka. Ufuatiliaji wa magonjwa na uchunguzi wa wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na Ebola tayari unaendelea kubaini maambukizi mapya, na WHO pia imetoa msaada wa vifaa pamoja na wataalamu sita wa magonjwa ya milipuko kusaidia katika kukabiliana na ugonjwa huo. 

Aina mpya 

WHO imesema mamlaka za afya za kitaifa pia ni muhimu katika juhudi hizo, ikiwa ni pamoja na taasisi ya kitaifa ya utafiti wa tiba ya jamii, ambayo imekamilisha uchambuzi wa sampuli kutoka kwa mgonjwa wa kwanza aliyethibitishwa, ambapo matokeo yanaonyesha kuwa mlipuko mpya unaonyesha aina mpya ya Ebola. 

Uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha mlipuko huo mpya na jinsi ulivyokuja kumwambukiza mtu wa kwanza aliyethibitishwa.