Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlipuko mpya wa Ebola wazuka Mbandaka DRC:WHO 

Uchunguzi wa ebola.
Photo OMS/T. Jasarevic
Uchunguzi wa ebola.

Mlipuko mpya wa Ebola wazuka Mbandaka DRC:WHO 

Afya

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC leo imetangaza mlipuko mpya wa Ebola katika jimbo la kaskazini-magharibi baada ya kisa kuthibitishwa huko Mbandaka, jiji lililo katika jimbo la Equateur.  

Huu ni mlipuko wa tatu katika jimbo hilo tangu 2018. 

Kwa mujibu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO hadi sasa, kesi moja tu imethibitishwa.  

Mgonjwa huyo, mwanamume mwenye umri wa miaka 31, alianza kupata dalili tarehe 5 Aprili na baada ya zaidi ya wiki moja ya kuugulia nyumbani, alitafuta matibabu katika kituo cha afya cha eneo hilo.  

Tarehe 21 Aprili, mgonjwa huyo alilazwa katika kituo cha matibabu ya Ebola kwa uangalizi mkubwa lakini alifariki dunia baadaye siku hiyo.  

Baada ya kutambua dalili hizo, wahudumu wa afya waliwasilisha mara moja sampuli za kupima ugonjwa wa virusi vya Ebola. 

Uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha mlipuko huo. 

Wanafunzi wa shule ya msingi wakichukuliwa vipimo kwa ajili ya kudhibiti ebola.
© UNICEF/Jonathan Shadid
Wanafunzi wa shule ya msingi wakichukuliwa vipimo kwa ajili ya kudhibiti ebola.

Hatua zinazochukuliwa 

Dkt. Matshidiso Moeti, mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika sema, "Wakati unatutupa mkono. Ugonjwa umeanza kwa wiki mbili na sasa tunafukuzana nao. Habari njema ni kwamba mamlaka za afya nchini DRC zina uzoefu zaidi kuliko mtu mwingine yeyote duniani katika kudhibiti mlipuko wa Ebola kwa haraka.” 

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inakabiliwa na mlipuko wa 18 wa Ebola tangu 1976. Mlipuko wa sasa ni wa sita tangu 2018 ulipoanza kutokea mara kwa mara katika historia ya Ebola nchini humo. Milipuko ya awali katika jimbo la Equateur ilikuwa mwaka wa 2020 na 2018, na kesi 130 na 54 zilirekodiwa mtawalia. 

Juhudi za kumaliza mlipuko wa sasa tayari zinaendelea. Mgonjwa aliyekufa alizikwa salama na kwa heshima zote , ambazo zinahusisha kurekebisha sherehe za kitamaduni za mazishi kwa njia ambayo inapunguza hatari ya kuwaambukiza waliohudhuria.  

Yeyote aliyegusana na mgonjwa pia anatambuliwa na afya yake itafuatiliwa na kituo cha afya ambapo mgonjwa alipata huduma kimesafishwa. 

Wataalamu wa WHO walio DRC wanaunga mkono mamlaka ya kitaifa kuongeza msaada katika maeneo muhimu ya kukabiliana na mlipuko ikiwa ni pamoja na kupima, kufuatilia watu walioambukizwa, kuzuia na kudhibiti maambukizi, matibabu pamoja na kufanya kazi na jamii kusaidia hatua za afya ya umma ili kuzuia maambukizi zaidi. 

Utoaji wa chanjo ya Ebola 

Kwa mujibu wa WHO chanjo dhidi ya Ebola imepangwa kuanza katika siku zijazo.  

Tayari nchi ina akiba ya chanjo ya rVSV-ZEBOV ya Ebola inayopatikana katika miji ya Goma na Kinshasa.  

Chanjo zitatumwa Mbandaka na kusimamiwa kupitia mkakati wa chanjo ya pete ambapo watu waliowasiliana na mgonjwa na wengine waliowasiliana na watu hao wote wanachanjwa ili kuzuia kuenea kwa virusi hivyo na kulinda maisha ya watu. 

"Watu wengi huko Mbandaka tayari wamechanjwa dhidi ya Ebola, chanjo ambayo inapaswa kusaidia kupunguza athari za ugonjwa huo," amesema Dkt. Moeti na kuongeza kuwa "Wale wote ambao walichanjwa wakati wa milipuko ya 2020 watapewa chanjo tena." 

Ebola ni ugonjwa mbaya, ambao unaoathiri na kusababisha vifo kwa binadamu na viumbe wengine.  

Viwango vya vifo vya kebola vimetofautiana kuanzia asilimia 25% hadi asilimia 90% katika milipuko iliyopita.  

Sasa kuna matibabu madhubuti yanayopatikana na ikiwa wagonjwa wanapokea matibabu mapema, pamoja na huduma inayohitajika, fursa zao za kuishi huboreka zaidi.