Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo wa wakulima na wafugaji Sudan Kusini wasababisha vifo vya zaidi ya watu 130 

Mapigano ya kikabila katika eneo la Jonglei nchini Sudan Kusini yamesababisha utekaji nyara na mauaji. (Maktaba))
UNMISS
Mapigano ya kikabila katika eneo la Jonglei nchini Sudan Kusini yamesababisha utekaji nyara na mauaji. (Maktaba))

Mzozo wa wakulima na wafugaji Sudan Kusini wasababisha vifo vya zaidi ya watu 130 

Amani na Usalama

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini UNMISS umechukua jukumu la kuwaleta pamoja raia na vyombo vya usalama vya serikali ili kuzungumza na kusaka amani kufuatia migogoro baina ya wakulima wakazi wa Magwi na wafugaji wanaohamahama, mapigano ambayo yamesababisha vifo vya watu 130 pamoja na kuchochea vitendo vya udhalilishaji.

Msafara wa walinda amani wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini UNMISS  ukiwa na wawakilishi wa mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa pamoja na viongozi wa serikali umewasili katika kaunti ya Magwi jimboni Equitoria Mashariki ili kutathmini na kuzungumza na wananchi kufuatia mapigano ya wanajamii wa eneo hili na wafugaji wa kuhamahama ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 130. 

 

Anyek Rose ni mwakilishi wa wanawake na anasimulia yaliyowasibu, 

“Mambo mengi mabaya yalitokea wakati wafugaji walipotuletea migogoro. Kuna  watu waliouawa, miongoni mwao ni wanawake. Sasa tuna mtoto mwenye umri wa wa miezi minne ambaye mama yake aliuawa. Pili, wanawake wamefanyiwa ukatili wa kijinsia huko vichakani, zaidi ya wanawake 20 walibakwa, na sasa waume zao wamewatelekeza. Je, Serikali inaweza kuwahudumia wanawake hawa? Ikiwa Serikali inataka sisi katika Kaunti ya Magwi tupatane na kukaa kwa amani, ni lazima wafanye jambo jema ambalo sisi tunaweza kulithibitisha.” 

Akitoa salamu za pole na rambirambi kutoka kwa Rais wa nchi hiyo, Naibu Waziri wa Mambo ya nje wa Sudan Kusini Deng Dau Deng amesema migogoro hiyo inaharibu taswira ya nchi yao. 

Amesema..... “Rais wetu ameagiza kambi zote za ng'ombe katika jimbo la  Equatoria Mashariki na Equatoria ya Kati, zirudi Jonglei na kurejea Jimbo la Lakes. Pia napenda kutoa rambirambi zetu kwa watu waliopoteza maisha, na tunasikitika kutokana na uharibifu wa mali uliotokea hapa. Wafugaji lazima warudi katika kaunti na majimbo yao.” 

Naye Hazel De Wet, Mkurugenzi wa masuala ya raia UNMISS amesema wanachofanya sasa ni kuangalia namna bora ya wananchi kuishi kwa amani. 

"Tunatafuta fursa na jinsi bora ambayo tunaweza kushirikisha jamii mbalimbali ili kuona ni hatua gani tunaweza kuchukua ili kuimarisha masuala yanayohusu ujenzi wa amani, kuruhusu wafugaji na wakulima waweze kuishi katika eneo moja kwa amani na utulivu na hivyo kuzuia matukio yoyote ya vurugu yanayoweza kutokea.”