FAO yachukua hatua kupunguza makali ya El Nino kwa wakulima na wafugaji Malawi

13 Februari 2019

Shirika la chakula na kilimo duniani,  FAO kwa usaidizi wa Belgium limeandaa mradi wa kupunguza makali ya madhara ya ukame uliosababishwa na El Nino nchini Malawi mwaka jana wa 2018.

FAO kupitia taarifa yake iliyotolewa leo huko Roma, Italia, imesema madhara ya El Nino ya mwaka jana yanaweza kuendeleza vipindi vya ukame mwaka  huu wa 2019 na hivyo kusababisha  kaya zilizo hatarini zaidi kushindwa kupata chakula cha kutosha.

“Msimu uliopita tumeshuhudia ukame na mlipuko wa viwavi jeshi, mambo ambayo kwa pamoja yalisababisha kupungua kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na wakulima na wafugaji wakauza mazao na mifugo yao kwa bei ya chini huku wengine wakijitumbukiza kwenye kazi za vibarua,” imesema FAO.

Ili kuepusha hali hiyo mradi huo wa FAO unaotokana na fedha kutoka FAO unalenga kusaidia watu 22,000 kwenye wilaya 8 kati ya 12 zilizobainishwa ambazo tayari zimekumbwa na madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

Mradi huo utapunguza hasara ambayo wanapata wakulima wakati wa uzalishaji na pia mifugo kufa na wakati huo huo kusaidia wakulima kupata maji kwa ajili ya shughuli za kilimo.

FAO kupitia mradi huo itasambaza mbegu za mazao ambayo yanastahimili ukame na pia yanakomaa haraka sambamba na  utoaji chanjo kwa mifugo ili kuepusha mlipuko wa magonjwa.

“Halikadhalika mradi utawapatia wanufaika stadi za matumizi na uhifadhi wa maji ili kuepusha kupotea kwa rasilimali hiyo,” imesema FAO huku ikisisitiza kuwa mradi utatekelezwa kwa ushirikiano na Wizara ya kilimo na umwagiliaji ya Malawi.

Malawi ni miongoni mwa nchi zilizo hatarini zaidi kukumbwa na madhara ya mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni nchi ya 105 kati ya 113 kwenye orodha ya uhakika na upatikanaji wa chakula.

Ingawa kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi kwa wakazi wa vijijini, bado vipindi vya mfululizo vya El Niño na La Niña vimesababisha zaidi ya watu milioni 8 nchini humo kutokuwa na uhakika wa chakula.

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter