Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN imetoa wito wa usitishaji mapigano ili kuwanusuru raia waliokwama Mariupol 

Wanawake wakiwa wameketi kwenye vitanda katika makazi ya muda nchini Ukraine.
© UNICEF/Viktor Moskaliuk
Wanawake wakiwa wameketi kwenye vitanda katika makazi ya muda nchini Ukraine.

UN imetoa wito wa usitishaji mapigano ili kuwanusuru raia waliokwama Mariupol 

Msaada wa Kibinadamu

Umoja wa Mataifa leo umetoa wito wa kusitisha mapigano mara moja ili kuruhusu raia wanaoripotiwa kukwama na kuzingirwa na machafuko katika mji wa Kusini mwa Ukraine wa Mariupol kuhamishwa kwa usalama. 

"Maisha ya makumi ya maelfu ya raia wakiwemo wanawake, watoto na wazee, yako hatarini huko Mariupol. Tunahitaji utulivu na usitwashi wa mapigano hivi sasa ili kuokoa maisha yao. Kadri tunavyongoja ndivyo maisha zaidi yatakavyokuwa hatarini. Ni lazima waruhusiwe kuondoka kwa usalama sasa na leo hii. Kesho inaweza kuwa tumechelewa sana." Amesema Amin Awad mratibu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mgogoro wa Ukraine 

Mapema mwezi huu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa wito wa kusitishwa mapigano kwa ajili ya kuingiza misaada ya kibinadamu wakati Wakristo wa Orthodox wanasherehekea sikukuu ya Pasaka. 

Katika siku hiyo ya Pasaka, Awad alikumbusha na kusisitiza wito wa Guterres wa kusitisha mapigano ili kuruhusu misaada ya kuokoa maisha kuingia ndani ya Mariupol na maeneo mengine yanayoshambuliwa na kuwezesha kuondoka kwa wale wanaotaka kuondoka huku kukiwa na ripoti za hali ya Mariupol kuwa mbaya zaidi. 

"Wakati wa mpangilio adimu wa kalenda ya likizo za kidini za Pasaka ya Orthodox, Pasaka ya kawaida namfungo wa Ramadhani, ni wakati wa kuzingatia ubinadamu wetu wa pamoja, kuweka migawanyiko kando na kukumbatia upendo," amesema Awad.