Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuishi katika handaki kwa mwezi mmoja Ukraine  asilani sintosahau: Alina Beskrovna 

Alina Beskrovna aliishi kwenye handaki kwa mwezi mmoja, Mariupol.
© Alina Beskrovna
Alina Beskrovna aliishi kwenye handaki kwa mwezi mmoja, Mariupol.

Kuishi katika handaki kwa mwezi mmoja Ukraine  asilani sintosahau: Alina Beskrovna 

Amani na Usalama

Vikosi vya uvamizi vya Urusi sasa vimekaribia kuharibu kabisa Mariupol, jiji la bandari kusini mwa Ukraine.

Mkaazi wa zamani wa mji huo Alina Beskrovna akizungumza na UN News, anakumbuka masaibu ya mwezi mzima akijificha katika chumba cha chini ya ardhi au handaki huko aliposhuhudia mapigano makali na uharibifu mkubwa wa mji aliokuwa akiishi, kabla ya kutoroka. 

Umoja wa Mataifa unaendelea kutoa msaada ndani ya Ukraine na katika nchi jirani kwa watu waliokimbia makazi yao kutokana na mzozo unaoendelea 

"Asubuhi ya uvamizi huo niliondoka kwenye nyumba yangu na kuishi karibu mwezi mmoja katika handaki nje kidogo ya mji wa Mariupol, hadi nilipofanikiwa kutoroka tarehe 23 Machi." 

Siku chache za kwanza nilihisi kama karamu isiyo ya kawaida ya simanzi, tukiwa pamoja na marafiki. Tulikuwa na kila kitu tulichohitaji, mpaka ulipofika wakati kila kitu kimekwisha. 

Kwanza umeme ulikatika, wakati Urusi ilipopiga makombora mfumo wa umeme wa jiji hilo. Kompyuta mpakato au Laptops na simu za rununu zilianza kuishiwa na betri. 

Kisha Warusi walilenga mfumo wa maji. Tulijaza ndoo zote tulizoweza wakati mabomba yalipokuwa yakiendelea kutoa maji, lakini tuligundua haraka kwamba ukosefu wa maji ya kunywa ungekuwa tatizo kubwa. 

Na kisha tukasikia mlipuko mkubwa, na gesi ikatoweka, hali ambayo ilimaanisha kukusanya na kuchanja kuni, na kupika kwenye moto ulio wazi nje ya lango la handaki letu. 

Watu wengine waliruka maghorofani na kupoteza maisha 

Alina Beskrovna anasema alishuhudia watu wakiruka magorofani na kupoteza maisha yao, Mariupol, Ukraine.
© Alina Beskrovna
Alina Beskrovna anasema alishuhudia watu wakiruka magorofani na kupoteza maisha yao, Mariupol, Ukraine.

Kufikia mwisho wa wiki ya pili, tulisikia milio ya risasi ikija kutoka sehemu ya kaskazini ya jiji, ikilenga wilaya za makazi zilizo karibu nasi.  

Makombora mawili yaligonga jengo la ghorofa tisa upande wa pili wa barabara, ng'ambo ya ghorofa yetu.  

Tulishuhudia ghorofa ya nne ikiteketea kwa moto na watu wakiruka hadi kufa. 

Kila kombora lilipotua karibu, nilihisi kama lilikuwa linapitia kwetu moja kwa moja.  

Tulihisi mawimbi ya mshtuko, nyufa katika ukuta wa handaki na sakafu zilipanuka kwa kila pigo moja, na tulijiuliza ikiwa msingi ya jengo letu unaweza kuhimili. 

Alina Beskrovna, kabla ya mzozo akiwa na baba yake ambaye sasa hajulikani aliko.
© Alina Beskrovna
Alina Beskrovna, kabla ya mzozo akiwa na baba yake ambaye sasa hajulikani aliko.

Sijui endapo baba yangu yu hai ama la 

Mapema katika uvamizi huo wa Urusi, kituo cha mawasiliano kilichokuwa nyuma ya moja ya vyumba vya juu vya makazi yetu kililengwa na Warusi. 

Nilijua kwa nini ilikuwa inafanya hivyo, ili kutuacha tukiwa hoi na bila tumaini kabisa, tukiwa tumevunjika moyo, na kutengwa na ulimwengu wa nje. 

Nilipoteza mawasiliano na baba yangu. Alikuwa upande wa pili wa jiji na sikuwa na uhakika kama ningemwona tena.  

Nilitumaini tu kwamba angekuja tu, kwa kuwa alijua anwani yetu, lakini hakutokea. Na bado sijui kama yuko hai ama la. Na sijui kama alipelekwa Urusi kwa nguvu. 

Uvumi ulianza kuenea juu ya jinsi jiji hilo lilivyosambaratika, jna kwamba sasa lilikuwa eneo la Urusi.  

Tulisikia hadithi za kutisha za Wachechnya wakizurura mitaani, wakiwabaka wanawake, kuua raia mahali pasipokuwa na watu, na jinsi ilivyokuwa hatari hata kujaribu kuondoka kwa sababu ya mapigano makali katika pande zote tatu za jiji. 

Kwa hivyo, hakuna mtu aliyethubutu kutoka wala kutoroka. Kwa sababu ya ukosefu wa mawasiliano na ulimwengu wa nje, ilionekana kana kwamba kulikuwa na mauaji makubwa ya watu wengi yakifanyika karibu nami, na kwamba ulimwengu haukuwa na wazo, na haungepata kamwe kiwango cha taarifa za kweli za kile kinachotokea. 

Hofu ya ubakaji 

Nilikuwa na hofu kuu mbili. Moja ilikuwa ni ubakaji ambayo hutumiwa kama silaha ya vita na jeshi la Urusi, na sote tulijua hili  na ya pili ilikuwa kupelekwa Urusi kwa nguvu au kwa kile kinachoitwa Jamhuri ya Watu wa Donetsk. 

Pia nilikuwa na wasiwasi kuhusu Mariupol kutangazwa kuwa sehemu ya Jamhuri ya Watu wa Donetsk bila tumaini lolote la kuondoka kwangu. 

Niliendelea kuwaza tu, je wataturuhusu? Je, kuna njia ya kutokea? 

Wakazi waliosalia Mariupol walikwa wakitumia choo kimoja wakati mji ulikuwa ukiendelea kushambuliwa.
© Alina Beskrovna
Wakazi waliosalia Mariupol walikwa wakitumia choo kimoja wakati mji ulikuwa ukiendelea kushambuliwa.

Fursa ya kutoroka 

Mtu yeyote ambaye hakutoka katika siku tatu au nne za kwanza, hakuweza kuondoka baadaye, kwa sababu ya mapigano kushika kasi na vikosi vya Kirusi vinavyokaribia jiji hili kutoka pande zote tatu. 

Wale ambao walijaribu kukimbia walijikuta katika uwanja wa vita  amesema  Mkazi huyo wa zamani wa Mariupol 

Wale waliojaribu kukimbia walijikuta katika uwanja wa vita-Mkazi wa Mariupol .

Tulichoweza kufanya ni kungoja upenyo unaoweza kufunguka. Karibu na wiki ya pili ya vita, uvumi ulienea kwenye Telegram ya Kirusi (jukwaa la mitandao ya kijamii), kwamba safu ya vita iliyopangwa ilikuwa inakusanyika kwenye ukumbi wa michezo, ikielekea magharibi kwenye mji wa Manhush. 

Kila mtu aliyekuwa na gari na mafuta ya kutosha, aliweka vipande vyeupe vya vitambaa kwenye vioo vyao vya pembeni kuashiria kwamba walikuwa ni raia wanaojaribu kukimbia, akaenda mahali pa kukusanya. 

Lakini hapakuwa na kitu. Iligeuka kuwa uvumi wa uwongo. 

Kufikia Machi 20, Warusi wakawa wamechukua kabisa ukanda wote waeneo karibu na bahari ya Azov, kutoka Berdyansk na Manhush, hadi nje ya mji wa Mariupol. 

Siku tatu baadaye tuliamua kuondoka licha ya kuwepo kwa taarifa za kulengwa kwa raia, kwani jiji hilo lilikuwa likizingirwa na zulia na mabomu yaliyovurumishwa kwa usahihi kabisa. 

Niliona kwa macho yangu jinsi walivyolenga majengo ya ghorofa, kana kwamba walikuwa wakicheza mchezo wa kompyuta. 

Tulikuwa tukikosa chakula na maji. Nilikuwa sijaoga kwa mwezi mmoja. 

Alina Beskrovna akipika kwa moto wa nje kufuatia kukatika kwa umeme.
© Alina Beskrovna
Alina Beskrovna akipika kwa moto wa nje kufuatia kukatika kwa umeme.

Safari ya kutisha 

Saa moja kamili asubuhi ya tarehe 23 Machi, tulianza kuelekea Zaporizhzhia. Na baada ya vituo 16 vya ukaguzi vya Urusi, safari ambayo kwa kawaida ingechukua saa tatu ilituchukua zaidi ya  saa 14 kufika. 

Uendeshaji wenyewe ulikuwa wa kutisha. Wanajeshi wa Urusi walitutafuta, wakakagua hati na kuwaweka kizuizini kila mwanamume.  

Lakini mara tu tulipofika kituo cha ukaguzi cha Ukraine karibu na lango la Zaporizhzhia, tulisikia lugha ya Kiukraine. 

Ilionekana kana kwamba tumefanikiwa, kana kwamba tulikuwa salama kiasi. 

Licha ya kuhisi kana kwamba nilikuwa nikitoka kwenye shimo hili jeusi la uharibifu na kifo, Zaporizhzhia yenyewe haikuwa salama, kulikuwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya anga. 

Lakini tulikuwa tumetoka Mariupol na hatukuweza kuamini tulikuwa hai. 

TAGS: Urusi, Ukraine, Mariupol, vita, handaki, Alina Beskrovna