Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia 101 wamehamishwa salama kutoka kwenye kiwanda cha chuma cha Azovstal Mariupol:UN

Raia kutoka Mariupol wanakimbia Azovstal eneo la Mariupol kufuatia operesheni ya kuhamishwa inayoongozwa na UN.
© UNOCHA/Kateryna Klochko
Raia kutoka Mariupol wanakimbia Azovstal eneo la Mariupol kufuatia operesheni ya kuhamishwa inayoongozwa na UN.

Raia 101 wamehamishwa salama kutoka kwenye kiwanda cha chuma cha Azovstal Mariupol:UN

Wahamiaji na Wakimbizi

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine Osnat Lubran amesema amefurahishwa na kufarijika kuthibitisha kwamba raia 101 wamefanikiwa kuondolewa kwenye kiwanda cha chuma cha Azovstal huko Mariupol Ukraine na maeneo mengine katika operesheni maalum iliyoratibiwa na Umoja wa Mataifa na kamati ya kimataifa ya chama cha msalaba mwekundu (ICRC) ya kuhamisha watu waliokuwa wamekwama Mariopul .

Amesema operesheni hiyo ilianza Ijumaa tarehe 29 Aprili na ilikubaliwa na wahusika katika mzozo huo, kufuatia mazungumzo ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres wakati wa ziara yake ya hivi karibuni huko Moscow na Kyiv.

“Shukrani kwa operesheni hiyo, wanawake, wanaume, watoto, na wazee 101 hatimaye wameweza kuondoka kwenye mahandaki yaliyokuwa kwenye kiwanda cha Azovstal na kuona mwanga baada ya miezi miwili. Watu wengine 58 walijiunga nasi katika mji wa Manhush, mji ulio viungani mwa Mariupol. Leo tumeongozana na watu 127 hadi Zaporizhzhia, takriban kilomita 230 kaskazini-magharibi mwa Mariupol, ambako wanapokea usaidizi wa awali wa kibinadamu, ikiwa ni pamoja na huduma za afya na kisaikolojia, kutoka kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa, ICRC na washirika wetu wa kibinadamu. Baadhi ya watu waliamua kutoendelea na msafara kuelekea Zaporizhzhia.”

Madhila waliyopitia ni makubwa

Mratibu huyo amesema katika siku chache zilizopita akisafiri na watu hao wanaohamishwa amewasikia akina mama, watoto na wazee wakizungumza kuhusu kiwewe cha kuishi siku baada ya siku kwenye mahandaki nakusikia makombora yakirushwa huku wakighubikwa na hofu ya kifo, wakikabiliwa na ukosefu mkubwa wa maji, chakula, na usafi wa mazingira.

“Walikuwa wakizungumzia hali ya jehanamu ambayo ilikuwa ikiwakabili tangu kuanza kwa vita hivi, wakitafuta hifadhi katika kiwanda cha chuma cha Azovstal, wengi wakitenganishwa na wanafamilia ambao bado hawajui hatima yao.”

Ameongeza kuwa ameshuhudia machozi ya furaha yakibubujika wakati wanafamilia waliokwama katika sehemu tofauti za kiwanda hicho kwa miezi miwili walipounganishwa tena.

Hadithi hizi kutoka Mariupol na maeneo mengine mengi nchini Ukrainie ni ushahidi wa ukatili wa vita hivi vya kidhalimu.

Raia wakiondoka Azovstal eneo la Mariupol, Ukraine wakati wa operesheni ya kuwahamisha.
© ICRC
Raia wakiondoka Azovstal eneo la Mariupol, Ukraine wakati wa operesheni ya kuwahamisha.

Bado kuna watu wamekwama Mariupol

Lubrani amesema pamoja na Habari Njema ya leo kufanikiwa kuwahamisha watu salama hadi Zaporizhzhia, “lakini, nina wasiwasi kwamba kunaweza kuwa na raia zaidi ambao bado wamekwama Mariupol. Tuko tayari kufanya kazi na ICRC kurejea Azovstal ili kuwahamisha, na kufanya vivyo hivyo katika maeneo mengine yote yanayokumbwa na mapigano makali na yanayoendelea kote Ukrainie. Umoja wa Mataifa utaendelea kushirikiana na wahusika kwenye mzozo kwa ajili hiyo.”

Ameongeza kuwa wamejitolea pia kushirikiana na wahusika ili kurejea Mariupol na kuleta usaidizi wa haraka wa kibinadamu kwa watu wanaoishi katika jengo lililoharibiwa ambako hakuna maji wala umeme. “Tunajua hilo linaweza kufanywa, na lazima lifanyike.”