Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais wa Ukraine ataka Baraza la Usalama liungane kwa ajili ya amani

Taswira ya ukumbi wa Baraza la Usalama la UN wakati Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy (kwenye skrini) alipohutubia  05 Aprili 2022
UN /Loey Felipe
Taswira ya ukumbi wa Baraza la Usalama la UN wakati Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy (kwenye skrini) alipohutubia 05 Aprili 2022

Rais wa Ukraine ataka Baraza la Usalama liungane kwa ajili ya amani

Amani na Usalama

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amehutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa hisia kali akielezea kwa kinagaubaga kile alichodai kuwa ni mauaji ya makusudi yaliyofanywa na  majeshi ya Urusi dhidi ya raia huko Bucha, viungani mwa mji mkuu Kyviv, hotuba ambayo ametoa huku akitaka wajumbe wa Baraza kuchagua kuhusu  hatma ya muundo wa ulinzi na usalama ulioanzishwa baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Akihutubia kwa njia ya video, Bwana Zelenskyy amefananisha kura ya turufu inayotumiwa na wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama kama silaha ya kifo.

“Tunahangaika na taifa ambalo linatumia kura turufu ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kama haki ya kufa,” ameonya Rais Zelenskyy. Iwapo itaendelea kufanya hivyo, nchi hazitategemea tena kwenye taasisi za kimataifa au sheria za kimataifa kusaka usalama, bali uthabiti wa silaha zao.

Akitanabaisha kuwa ndio kwanza amerejea kutoka Bucha, mji ambao umekombolewa, ameelezea jinsi majeshi ya Urusi yamesaka na kuua kwa makusudi mtu yeyote aliyeunga mkono Ukraine. 

Mbinu zitumiwazo na  magaidi

Ametuhumu Urusi kwa kutaka kugeuza raia wa Ukraine kuwa watumwa wanyamavu huku ikipora waziwazi kila kitu kuanzia chakula huku maiti wakivuliwa vito vyao vya dhahabu.

“Mbinu hizi hazina tofauti na zile za Da’esh isipokuwa za sasa zinatumiwa na nchi ambayo ni mjumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama. Je usalama unaweza kuwa na hakikisho wapi?” amelalama.

Amani inapaswa kutawala

Ukraine inahitaij amani, Ulaya inahitaji amani ,dunia inahitaji amani, amesisitiza Rais huyo wa Ukraine huku akikazia hoja ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mgawanyiko ndani ya Baraza ambao umekwamisha chombo hicho kuchukua hatua kunusuru Ukraine. Amesihi Baraza lichukue hatua zozote zilizo ndani  ya uwezo wake kumaliza vita hivyo.

Idadi ya raia waliouawa tangu Machi 17 imeongezeka maradufu

Mkuu wa Idara ya Umoja wa Mataifa ya Siasa na Ujenziwa Amani Rosemary DiCarlo naye pia ameeleza kuwa hali ya usalama imezorota tangu alipohutubia Baraza tarehe 17 mwezi uliopita wa Machi.

Idadi ya raia waliouawa imeongezeka zaidi ya maradufu; miji ya Ukraine inaendela kushambuliwa kwa mabomu, na makombora mazito, angani na ardhini, mamia ya maelfu ya raia bado wamenasa kwenye mazingira hatarishi.
“Uharibifu uliofanyika Maripol na miji mingine ya Ukraine ni alama za aibu kwa vita hii isiyo na msingi wowote,” amesema Bi. DiCarlo.

Baba akimuaga mtoto wake wa kiume na familia yake baada ya kuwafikisha eneo salama na kisha yeye kurejea Ukraine
© IOM/Francesco Malavolta
Baba akimuaga mtoto wake wa kiume na familia yake baada ya kuwafikisha eneo salama na kisha yeye kurejea Ukraine

Ametoa wito kwa viongozi wa Ukraine na Urusi kutafsiri kivitendo maendeleo ya mashauriano yanayoendelea akisisitiza kuwa mashambulizi ya jumla na maeneo ya makazi hayakubaliki katika sheria ya kimataifa.

Mazingira magumu yakwamisha UN kufanya kazi

Akihutubia Baraza hilo, Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa Misaada ya kibinadamu, Martin Griffiths, amesema zaidi ya robo ya raia wa Ukraine wamekimbia nchi yao.

“Mazingira magumu yanazuia juhudi zetu za kufikia raia au wao kutufikia sisi,” amesisitiza.

Katika moja ya viashiria vya dalili chanya, ametangaza kuwa siku moja iliyopita, msafara ulioondoka kituo cha 
Dnipro kuelekea Severodonetsk — mji ulio mashariki mwa Ukraine, ukiwa umebeba vyakula, nguo za kujihifadhi na baridi, vifaa vya kujisafi na dawa umewasili na vifaa vimekabidhiwa kwa chama cha Msalaba Mwekundu cha Ukraine.

‘Safari ni ndefu kuhakikisha mapigano yanakoma na watu wanahama salama

Mratibu huyo pia ameelezea mazungumzo yake yamuda mrefu na ya uhalisia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergey V. Lavrov na Naibu wake Sergey V. Vershinin, tarehe 4 mwezi huu wa Aprili, pamoja na mazungumzo mengine aliyofanya kando na Waziri wa Ulinzi wa Urusi ambaye kwa pamoja wamebadilishana mawazo kuhusu hoja ya kusitisha mashambulizi ili raia waweze kuondoka salama sambamba na misaada ifikie raia.

“Baada ya mikutano hii naamini kuwa “bado kuna safari ndefu mbele yetu, lakini lazima tuifanye safari hiyo na tutasafari,” amesema Bwana Griffiths.

Tarehe 7 mwezi huu wa Aprili anatarajia kusafiri kuelekea Ukraine kuongoza mazungumzo na maafisa waandamizi wa Ukraine kuhusu suala hilo hilo.

Maisha ya watu yamefungiwa kwenye mabegi

Mjadala ulipoanza, Mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Linda Thomas-Greenfield amesema nyuma ya picha zinazosambaa kutoka Bucha, ni maisha ya watu yaliyofungiwa kwenye mabegi na kuacha nyumba zao walizofahamu maisha yao yote.

Mwakilishi wa kudumu wa urusi kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Vassily A. Nebenzia  kwenye mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu Ukraine
UN /Manuel Elias
Mwakilishi wa kudumu wa urusi kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Vassily A. Nebenzia kwenye mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu Ukraine

Urusi yapinga madai dhidi yake

Mwakilishi wa Kudumu wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Vassily A. Nebenzia akijibu tuhuma dhidi ya serikali yake amesema, nchi  yake imeokoa watu 123,500  huko Mariupol bila msaada wa Ukraine. Zaidi ya watu 600,000 wamehamishiwa Urusi tangu operesheni hiyo ianze tarehe 24 mwezi Februari mwaka huu.

“Hatuzungumzii kulazimisha watu au kuteka watu, huu ni uamuzi wa hiari na video zilizoko kwenye mitandao ya kijamii zinathibitisha hilo,” amesisitiza.

Kwa Rais wa Ukraine, Balozi Nebenzia amesema, “Tunaweka utashi wako juu ya madai dhidi ya Urusi yasiyo na msingi ambayo yanakinzana na mashuhuda wa matukio hayo.”

Kuhusu madai ya majeshi ya Urusi huko Bucha, Balozi huyo amelaumu Ukraine na vyombo vy ahabari vya Magharibi kwa kusongesha uongo na kusema kuwa kuna video za watu wenye msimamo mkali Ukraine wakifyatulia risasi raia.

“Miili inayoonesha kwenye video zilizowasilishwa na Rais Zelenskyy hazifanani kabisa na kile kilichoripotiwa kufanyika kwenye eneo hilo kwa siku nne.”