Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto zaidi ya milioni 15 kupata chanjo ya polio Ethiopia:WHO 

Kampeni ya utoaji chanjo ya Polio
WHO
Kampeni ya utoaji chanjo ya Polio

Watoto zaidi ya milioni 15 kupata chanjo ya polio Ethiopia:WHO 

Afya

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO limesema Ethiopia inaendelea na kampeni ya duru ya pili ya chanjo ya matone ya polio  ijulikanayo kama nOPV2.  

Kampeni hiyo ya siku nne inayokamilika leo Aprili 18 inalenga kuwachanja na kuwalinda watoto zaidi ya milioni 16 wa umri wa chini ya miaka mitano dhidi ya ulemavu na vifo kutokana na mlipuko wa polio unaoendelea hivi sasa nchini humo .  

Kampeni hiyo iliyoanza tarehe 15 Aprili inafanyika nchi nzima kwenye majimbo yote isipokuwa Addis Ababa, Afar na Tigray, ambako kampeni imepangwa kufanyika wakati mwingine.  

nOPV2 ni nyezo mpya  

Kwa mujibu wa WHO chanjo ya nOPV2 ni zana mpya iliyoidhinishwa kupitia utaratibu wa orodha ya matumizi ya dharura ya dawa na tiba (EUL) ikichukua nafasi ya chanjo ya aina 2 ya virusi vya polio inayotolewa kwa njia ya matone ya (mOPV2) kulingana na ubora wake wa juu wa ulinzi uliothibitishwa dhidi ya virusi vya polio vinavyotokana na chanjo ya aina ya 2 (cVDPV2). 

"Chanjo hii mpya imeanza kutolewa katika ukanda wa Afrika ili kuhakikisha, pamoja na chanjo nyingine za polio, aina zote za polio zinatokomezwa ili watoto wanaoishi katika maeneo yenye chanjo duni wapate ulinzi wa kutosha dhidi ya maambukizi ya polio na kupooza baadaye," amesema Dkt. Boureima Hama Sambo, mwakilishi wa WHO nchini Ethiopia. 

Kampeni hii inaongozwa na kuratibiwa na taasisi ya afya ya umma ya Ethiopia (EPHI) na vituo vya operesheni ya dharura (EOCs) katika ngazi zote kwa msaada kutoka kwa washirika mbalimbali ikiwemo WHO.  

WHO imepeleka timu  

Zaidi ya wafanyakazi 100 wataalm wa kiufundi wa WHO na washauri wametumwa kusaidia kampeni hii kupitia: 

• uratibu, 

• mafunzo ya timu za kampeni, 

• kubuni na kutoa mafunzo ya vitendo kwa wahusika wote wa kampeni kuhusu utayarishaji na ufuatiliaji wa utekelezaji wa vifaa vya simu za rununu kama vile google sheet na open data kit (ODK), na 

• kuwezesha uajiri na usambazaji wa waangalizi huru na wafanya tathimini ya chanjo kwa ajili ya kuhakikisha ubora wa kampeni. 

Wafanyakazi na washauri wa WHO pia wanasimamia na kufuatilia moja kwa moja utekelezaji wa kampeni katika jamii.  

WHO pia imepeleka magari kuwezesha usafirishaji wa chanjo kwenye maeneo ya chanjo. 

Washirika katika kampeni hii ya chanjo, ni pamoja na WHO, UNICEF, Vituo vya Marekani vya kudhibiti na kuzuia magonjwa, Wakfu wa Bill na Melinda Gates, na washirika watekelezaji kama USAID wako tayari kuunga mkono kampeni hii.