Nchi za Afrika zaahidi kutokomeza aina zote za polio :WHO

26 Agosti 2021

Serikali wanachama wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa (WHO) kanda ya Afrika zimeahidi kumaliza aina zote zilizobaki za polio na kutoa kadi za alama ili kufuatilia maendeleo kuelekea kutokomeza kabisa virusi bvya ugonjwa huo. 

 Ahadi hizo zimetolewa kwenye kikao maalum kuhusu polio kilichofanyika kandoni mwa mkutano wa kamati ya 70 ya WHO kwa ajili ya Afrika. 

Wakati kanda ya Afrika ilithibitishwa kuwa huru bila ugonjwa wa polio mwaka mmoja uliopita kufuatia miaka minne bila kuwa na mgonjwa yeyote, milipuko ya virusi vya polio inayotokana na chanjo (cVDPV) inaendelea kuenea.  

cVDPV hutokea katika jamii ambapo watoto hawajapata chanjo ya kutosha ya polio.  
Visa vya polio viliongezeka mwaka jana kwa sehemu ni kwa sababu ya usumbufu wa kampeni za chanjo ya polio uliosababishwa na janga la corona au COVID-19.  

Tangu mwaka 2018, nchi 23 katika eneo hilo zimepata milipuko ya polio na zaidi ya nusu ya visa 1071 vya cVDPV vilirekodiwa barani Afrika. 

WHO inasema idadi ya wagonjwa iliongezeka mwaka jana moja ya sababu kubwa ikiwa ni kufurugwa kwa kampeni za chanjo dhidi ya polio kulikosababishwa na janga la corona au COVID-19. 

 Nyenzo na mbinu za kuzuia milipuko 

Nchi katika mkutano huo zimejadili jinsi zitakavyoanza kutekeleza Mkakati mpya wa kutokomeza polio duniani (GPEI) 2022-2026 mkakati, ambao ulizinduliwa mnamo  mwezi Juni ili kukomesha ueneaji wa CVDPVs. 

Mbinu na nyezo za kutumiwa ni pamoja na kuendeleza kasi na ubora wa mikakati ya kukabiliana na mlipuko, kama vile kupitia upelekaji wa haraka wa wafanyikazi wa upasuaji wa WHO, kuboresha matumizi ya chanjo ya polio kwa kujumuisha kampeni za polio kufikia watoto ambao hawajawahi kupata chanjo, na kupanua wigo wa utoaji wa chanjo ya matone mdomoni aina ya 2 (nOPV2), cmbinu mpya ambayo inaweza kumaliza zaidi milipuko ya aina 2 ya CVDPV iliyoenea zaidi. 

Kufikia sasa, nchi sita barani Afrika zimeanzisha chanjo hii na karibu watoto milioni 40 wamepewa chanjo na hakuna wasiwasi juu ya usalama wa chanjo hiyo uliobainika. 

 Kufuatilia mafanikio 

Mawaziri wa afya wa ukanda huo pia wamejitolea kukagua maendeleo mara kwa mara kupitia kadi za alama ya chanjo, ambayo itafuatilia utekelezaji wa wakati unaofaa wa hatua bora za kukabiliana na mlipuko wa polio, kuanzisha kwa chanjo ya matone ya polio aina ya 2 (nOPV2) kwa matumizi mapana na hali ya mpito ya kuingiza chanjo hiyo kwenye mifumo ya kitaifa ya afya katika mikakati na mbinu za kuchukua hatua. 

"Mafanikio yetu kumaliza ugonjwa wa polio katika ukanda huu yanaonyesha kile kinachowezekana tunapofanya kazi kwa pamoja na kwa uharaka", amesema mkurugenzi wa WHO wa kanda ya Afrika Matshidiso Moeti. 

Tangu Julai 2020, karibu watoto milioni 100 wa Kiafrika wamepewa chanjo dhidi ya polio. 
Wakati COVID-19 ilitishia mafanikio haya, Dk Moeti amesema kuwa inawezekana "kushinda vizuizi vya mwisho. Tuna ujuzi, lakini lazima uende sanjari na ahadi za rasilimali zitakazowezesha kufikia jamii zote ambazo hazijapata chanjo”.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter