Mwaka mmoja bila polio WHO kanda ya Afrika

24 Oktoba 2021

Ikiwa leo ni siku ya kutokomeza ugonjwa wa polio duniani, mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wamesisitiza azma yao ya kuendelea kutekeleza ahadi zao ili hatimaye ugonjwa huo usiwepo kabisa duniani hivi sasa na kwa vizazi vijavyo.
 

Taarifa ya pamoja iliyotolewa huko Hawassa nchini Ethiopia na mashirika hayo lile la afya, WHO na la kuhudumia watoto UNICEF na mdau wao Rotary imesema hatua hiyo inazingatia pia hatua ya Ethiopia kuzindua kampeni ya kitaifa ya utoaji wa chanjo ya polio kuanzia tarehe 22 hadi 25 mwezi huu wa Oktoba kwa lengo la kuhakikisha hakuna virusi vipya vya ugonjwa huo vinaibuka katika taifa hilo ambalo halina ugonjwa huo.

Hali ya polio duniani

Mwaka 1988, dunia iliazimia kutokomeza virusi vya Polio na leo hii kanda 5 kati ya 6 za WHO zimethibitishwa kutokuwa na ugonjwa huo huku virusi hivyo vikiripotiwa kuwepo katika nchi mbili tu ambazo ni ugonjwa huo umejikita ambazo ni Pakistan na Afghanistan.

Wagonjwa wawili wa polio waliripotiwa duniani katikati ya mwezi huu wa Oktoba ikilinganishwa na wagonjwa 125 katika kipindi kama hicho mwaka jana wa 2020.

Wanaume wawili wa kabila la Eñepa  nchini Venezuala wakisafirisha chanjo kuelekea kituo cha matibabu.
© UNICEF/Alejandra Pocaterra
Wanaume wawili wa kabila la Eñepa nchini Venezuala wakisafirisha chanjo kuelekea kituo cha matibabu.

Tarehe 25 mwezi Agosti mwaka 2020, kamisheni huru ya kanda ya Afrika ya kuthibitisha kutokomezwa kwa polio, ARCC ilitangaza kuwa WHO kanda ya Afrika ambayo ina nchi 47 haina tena polio pori, WPV.
Ingawa asilimia 99.9 ya polio imetokomezwa kupitia chanjo ya polio, katika baadhi ya matukio iwapo kila mtoto hajapatiwa chanjo, aina nyingine ya virusi vya polio inaweza kuibuka.

Ili kukabiliana na hilo ndio maana Ethiopia imeamua kuhakikisha hakuna virusi vingine vinaweza kuibuka na kampeni yao ya chanjo inalenga kufikia watoto milioni 17 nchini kote walio na umri wa chini ya miaka mitano. Watoa chanjo wanapita nyumba kwa nyumba.

Ujumbe wa siku ya kutokomeza polio ni “siku moja, msisitizo ni mmoja: kutokomeza polio na kutekeleza ahadi yetu ya kuwa na dunia bila polio.”

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter