Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita vya Ukraine ni mgogoro unaotuathiri wote: Guterres

Mama akiwa na mwanae katika vitongoji duni Vijaynagar, India.
© UNICEF/Prashanth Vishwanathan
Mama akiwa na mwanae katika vitongoji duni Vijaynagar, India.

Vita vya Ukraine ni mgogoro unaotuathiri wote: Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres hii leo amewasilisha muhtasari wa kwanza wa kina wa sera itakayotolewa na Kikundi cha Kukabiliana na Migogoro ya Kimataifa kuhusu Chakula, Nishati na Fedha (GCRG), ambacho alikianzisha kuchunguza madhara ya vita vya Ukraine kwa dunia.

Huu hapa ni muhtasari wa matokeo, na baadhi ya maswali muhimu yaliyojibiwa, juu ya kile ambacho GCRG wanalenga kufikia.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa muhtasari huo, Guterres alidokeza kwamba, wakati ambapo umakini mkubwa umewekwa kwenye athari za vita kwa wananchi wa Ukraine, pia vinaleta athari duniani, katika dunia ambayo tayari ilikuwa ikishuhudia ongezeko la umaskini, njaa na machafuko ya kijamii.

"Sasa tunakabiliwa na dhoruba kamilifu ambayo inatishia kuharibu uchumi wa nchi zinazoendelea", alisema Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa.

GCRG ni nini?

Kundi la Kukabiliana na Migogoro Duniani kuhusu Chakula, Nishati na Fedha au kwakifupi GCRG ni kundi la wanachama 32, linaloongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed, ambalo linajumuisha wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, benki za maendeleo na mashirika mengine ya kimataifa.

Kundi hili lilizinduliwa na Guterres tarehe 14 Machi, 2022, kufuatia wasiwasi juu ya Urusi kuivamia nchi ya Ukraine, pamoja na athari zinazoendelea za janga la coronavirus">COVID-19.

Bibi akilisha mjukuu wake wamiezi 17 nchini Sudan Kusini.
© UNICEF/Bullen Chol
Bibi akilisha mjukuu wake wamiezi 17 nchini Sudan Kusini.

Litasaidiaje?

Kundi hilo litahakikisha ushirikiano katika serikali zote, mfumo wa kimataifa na sekta mbalimbali, ili kusaidia nchi zilizo hatarini kuepusha majanga makubwa.

Hili litafikiwa kupitia uratibu na ushirikiano wa hali ya juu, hatua za haraka, na ufikiaji wa takwimu muhimu, uchambuzi na mapendekezo ya sera. Muhtasari wa kwanza wa sera umetolewa Jumatano tarehe 13 Aprili 2022.

Shamba la ngano wakati wa mavuno, Krasne, Ukraine.
© FAO/Anatolii Stepanov
Shamba la ngano wakati wa mavuno, Krasne, Ukraine.

Kwa nini ni muhimu?

Mgogoro wa Ukraine una hatari ya kuingiza hadi watu bilioni 1.7 - zaidi ya moja ya tano ya walimwengu - katika umaskini, umaskini na njaa.

Ukraine na Urusi wanatoa asilimia 30 ya ngano na shayiri duniani, moja ya tano ya mahindi yake, na zaidi ya nusu ya mafuta yake ya alizeti.

Kwa pamoja, nafaka zao ni chanzo muhimu cha chakula kwa baadhi ya watu maskini zaidi na walio hatarini zaidi, wakitoa zaidi ya theluthi moja ya ngano inayoagizwa kutoka nje na nchi 45 za Afrika na nchi zenye maendeleo duni.

Wakati huo huo, Urusi ni muuzaji mkubwa wa gesi asilia ulimwenguni, na muuzaji wa pili kwa ukubwa wa mafuta.

Vita hivyo vimeongeza changamoto ambazo nchi nyingi zinazoendelea zinakabiliwa nazo kutokana na janga la COVID-19, pamoja na mizigo ya kihistoria ya madeni na mfumuko wa bei unaoongezeka.

Tangu kuanza kwa mwaka 2022, bei ya ngano na mahindi imeongezeka kwa asilimia 30, bei ya mafuta imepanda kwa zaidi ya asilimia 60 tangu mwaka 2021, na bei ya gesi asilia na mbolea imeongezeka zaidi ya mara mbili.

Wakati huo huo, operesheni za kibinadamu za Umoja wa Mataifa zinakabiliwa na upungufu wa ufadhili: Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limeonya kwamba halina rasilimali za kutosha kulisha watu wenye njaa walio katika hali mbaya. Shirika hilo linahitaji kwa dharura dola bilioni 8 kusaidia shughuli zake nchini Yemen, Chad na Niger.

Ripoti hiyo, alisema Guterres, “inaonesha kwamba kuna uwiano wa moja kwa moja kati ya kupanda kwa bei za vyakula na ukosefu wa utulivu wa kijamii na kisiasa. Ulimwengu wetu hauwezi kumudu hii. Tunahitaji kuchukua hatua sasa”.

Mambomba ya mafuta nchini Russia.
World Bank/Gennadiy Kolodkin
Mambomba ya mafuta nchini Russia.

Muhtasari wa sera ya kwanza unapendekeza nini?

Muhtasari wa sera unasisitiza juu ya umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na mgogoro huo, ambao, inasema, "utaacha makovu makubwa na ya muda mrefu".

Ripoti hiyo inatoa wito kwa nchi zote - pamoja na sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na wahusika wengine - kutambua kwamba "asili ya mishtuko inayozidi kuwa ya kawaida ulimwenguni ni kwamba kila nchi haiwajibiki", na kwamba suluhu zinapaswa kuzingatia, hatari ya kimataifa, badala ya kitaifa.

Kwa kuzingatia kupanda kwa gharama ya chakula, mafuta na bidhaa nyinginezo, nchi zote zinahimizwa kuweka masoko yao wazi, kupinga ubadhirifu na vikwazo visivyo vya lazima vya kusafirisha bidhaa nje, na kuweka akiba kwa nchi zilizo katika hatari kubwa ya njaa.

Ripoti hiyo inatoa wito kwa taasisi za fedha za kimataifa kutoa ufadhili kwa nchi zilizo hatarini zaidi, kusaidia serikali katika nchi zinazoendelea kuwekeza katika nchi maskini zaidi na zilizo hatarini zaidi kwa kuongeza ulinzi wa kijamii, na kufanyia mageuzi mfumo wa fedha wa kimataifa ili ukosefu wa usawa upunguzwe.

Misaada ya kibinadamu, unasema muhtasari wa sera, lazima ufadhiliwe kikamilifu, na mageuzi makubwa ya mfumo wa fedha wa kimataifa yanahitajika ili, kwa maneno ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, "kuvuta nchi zinazoendelea nyuma kutoka kwenye ukingo wa kifedha".

Mgogoro huo, kulingana na jinsi ulimwengu unavyokabiliana nao, unaweza pia kugeuka kuwa fursa kwa sayari. Muhtasari wa sera unakubali kwamba, kwa muda mfupi, akiba ya kimkakati ya nishati ya mafuta ya kisukuku inahitaji kutolewa ili kuleta utulivu wa bei na kuhakikisha  kuna usambazaji wa kutosha.

Hata hivyo, utumiaji wa nishati mbadala ungesaidia kuhakikisha kuwa bei za nishati zinazopanda hivi sasa hazirudiwi tena katika siku zijazo, huku kukiharakisha maendeleo kuelekea siku zijazo safi, zenye matumizi ya kiwango cha chini ya kaboni, na nishati endelevu.

Muhtasari wa sera unaofuata utatolewa lini?

Mpango uliopo sasa ni kwa muhtasari wa sera za GCRG kutolewa kila wiki, siku ya Jumanne, lakini ratiba ya uchapishaji inaweza kubadilika, kutegemea jinsi vita vya Ukraine vitakavyokua.