Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita Ukraine: Bei za nishati, chakula zazidi kupaa 

Mji wa bandari wa Mariupol ulioshambuliwa nchini Ukraine.
IOM/Diana Novikova
Mji wa bandari wa Mariupol ulioshambuliwa nchini Ukraine.

Vita Ukraine: Bei za nishati, chakula zazidi kupaa 

Amani na Usalama

Zaidi ya siku 100 zimepita tangu Urusi kuvamia Ukraine, na hii leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametambulisha ripoti ya pili kutoka kikundi cha kuchukua hatua dhidi ya janga la dunia litokanalo la vita hivyo, GCRG na kusema madhara ya vita hiyo katika sekta ya chakula, nishati na fedha ni dhahiri shairi na yanazidi kuongezeka kila uchao.

Ripoti hiyo imewasilishwa na kikundi hicho alichounda mapema mwaka huu kutathmini madhara ya vita hiyo katika maeneo hayo matatu. 

Taswira mpya ya miezi 3 ya uvamizi Ukraine 

Miezi mitatu ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine kuna taswira mpya; “walio Ukraine kila siku wanakabiliwa na umwagaji damu na machungu. Na kwa wengine wengi duniani kote, vita inatishia kuibua wimbi la aina yake la njaa na uhohehahe, na kuacha mtibuko mkubwa wa kijamii na kiuchumi pindi itakapomalizika,” amesema Guterres. 

Amesema watu walio hatarini zaidi pamoja na nchi zinazojikokota tayari wameathirika zaidi, “lakini kumbuka, hakuna nchi au jamii ambayo haitaguwa na ongezeko la gharama za maisha litokanalo na janga hili.” 

Wafanyakazi katika kiwanda cha nafaka nchini Ukraine.
© FAO/Genya Savilov
Wafanyakazi katika kiwanda cha nafaka nchini Ukraine.

Gharama kutokana na vita Ukraine 

Bei za vyakula zinakaribia kuvunja rekodi; bei za mbolea zimeongezeka maradufu na kuibua hofu kila mahali. 

“Bila mbolea, kutaibuka uhaba wa mahindi, ngano na nafaka nyingine tegemewa, ikiwemo mchele  na hivyo kuwa na madhara makubwa kwa wakazi wa Asia na Amerika ya Kusini,” ameonya Guterres. 

Guterres amesema mwaka huu uhaba wa chakula ni kutokana na kushindwa kukipata lakini mwaka ujao inaweza kuwa uhaba wa chakula kwa kuwa hakipo kabisa. 

Bei ya nishati nayo imeongezekana kuvunja rekodi na kusababisha baadhi ya watu kukosa umeme na wengine nishati hakuna kabisa, hususan barani Afrika. 

Vita pia imesababisha kubinywa kwa utoaji wa fedha kwa nchi zinazoendelea  wakati tayari nchi hizo zilikuwa na tatizo la kushindwa kulipa madeni na tishio la kuporomoka kwa uchumi kutokana na janga la coronavirus">COVID-19, ukosefu wa uwiano katika harakati za kujikwamua  bila kusahau janga la mabadiliko ya tabianchi. 

Ujira nao umeporomoka 

Duniani kote, waajiriwa 3 kati ya 5 wanapata ujira mdogo kuliko waliolipwa kabla ya janga la COVID-19. 

Sasa ni kwamba mtu binafsi halikadhalika serikali hawana matumaini ya kuweka mizania kwenye bajeti za matumizi  yao, “matumizi ni makubwa kuliko mapato.” 

Familia zinashinikizwa kupitisha uamuzi mgumu; Ama kufunga biashara; kuuza mifugo; au kuondoa watoto wao shuleni. 

Wanawake na wasichana ndio wa mwisho kula chakula, na wa kwanza kukosa mlo pindi kunapokuweko na uhaba wa chakula. 

Nini kifanyike sasa? 

“Kuna njia moja tu ya kukomesha wimbi hili la majanga juu ya majanga,” amesema Guterres akiongeza kuwa, “uvamizi wa Urusi nchini Ukraine lazima ukome, sambamba na uharibifu na mauaji.” 

Suluhu la kisiasa lazima lipatikane kwa mujibu wa sheria za kimataifa na Katiba ya Umoja wa Mataifa. Lakini hadi hili lifanyike, tunahitaji mambo mawili. 

1. Utulivu katika masoko ya chakula na nishati duniani 

Hili ni muhimu ili kumaliza mzunguko wa ongezeko la bei na hivyo kuleta ahueni kwa nchi zinazoendelea. “Uzalishaji chakula nchini Ukraine na chakula na mbolea kutoka Urusi lazima virejeshwe kwenye masoko ya dunia licha kuwepo kwa vita.” 

Guterres amesema tayari amemtaka Katibu Mkuu wa UNCTAD Rebeca Grynspan na Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA Martin Griffiths waratibu vikosi kazi viwili vya kuwezesha uuzaji nje ya Ukraine tena kwa usalama vyakula kupitia Bahari Nyeusi na pia chakula na mbolea kutoka Urusi bila vikwazo vyovyote. 

2. Rasilimali ziweko kwa ajili ya nchi na jamii maskini 

Katibu Mkuu anasema suala la pili ni kuhakikisha serikali za nchi maskini zina uwezo wa kukopa fedha zinazohitajika ili kuendeleza uchumi wao na maisha ya wananchi wao yaweze kustawi. 

“Hakuna suluhu ya janga hili la kimatiafa bila suluhu katika janga la kiuchumi linalokumba nchi zinazoendelea,” amesema Guterres. 

Ni kwa mantiki hiyo ametaka mfumo wa fedha duniani ukabiliane na changamoto na utumie fursa zote zilizoko kusaidia jamii na nchi zilizo hatarini. 

 Ujumbe wa leo kutoka ripoti hii ni dhahiri kwamba, “lazima tuchukue hatua sasa kuokoa maisha na mbinu za watu kujipatia kipato kwa miezi na miaka ijayo,” amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa “inahitajika hatua za kimataifa kutatua janga la kimataifa na tunahitaji kuanza leo.”