Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukraine inateketea, asema Guterres huku akitangaza dola milioni 40 zaidi kutoka CERF

Huyu ni Milala, mtoto mwenye umri wa miaka 6. Mama yake aliuawa kwa bomu na sasa yeye anatibiwa majeraha kwenye hospitali ya watoto iliyoko Kyiv, Ukraine.
© UNICEF/Oleksandr Ratushniak
Huyu ni Milala, mtoto mwenye umri wa miaka 6. Mama yake aliuawa kwa bomu na sasa yeye anatibiwa majeraha kwenye hospitali ya watoto iliyoko Kyiv, Ukraine.

Ukraine inateketea, asema Guterres huku akitangaza dola milioni 40 zaidi kutoka CERF

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kwa mara nyingine tena amezungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani hii leo na kusema Ukraine inazidi kuteketea mbele ya macho ya dunia na madhara ya vita kwa wanancih  hayana kipimo.
 

“Watu wasio na hatia wakiwemo wanawake na watoto wanauawa. Baada ya  kushambuliwa na majeshi ya Urusi, barabara, viwanja vya ndege na shule vimesalia magofu’” amesema Guterres.
Katibu Mkuu amesema kadri muda unavyosoma mambo mawili yako dhahiri; Mosi; hali inazidi kuwa mbaya na pili, chochote kile kitakachotokea, vita hii haitakuwa na mshindi bali kila mtu atakuwa ameshindwa.

Umoja wa Mataifa na wadau wanaendelea na kutoa usaidizi

Umoja wa Mataifa na wadau wake wanafanya kazi kuhakikisha kuna njia salama ya kupita ili kufikisha misaada kwenye maeneo yaliyozingirwa na kwamba “hadi zaidi sasa zaidi ya watu 600,000 wamepatiwa aina mbalimbali za misaada.”

Ni kwa kutambua ongezeko la mahitaji, Katibu Mkuu ametangaza kuwa Umoja wa Mataifa kupitia mfuko wake wa usaidizi wa dharura, CERF umetoa dola milioni 40 zaidi ili kusongesha misaada ya  haraka kwa wahitaji.

Misaada kama vile maji, chakula, dawa pamoja na fedha taslimu zitapatiwa wahitaji. Ingawa ametaka pande zote ziheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu ili misaada hiyo ifikie walengwa.

Mama mzazi akiwa amelala kando ya kitanda cha mtoto wake mchanga kwenye wadi ya muda ya wazazi kwenye mji mkuu wa Ukraine, Kyiv
© UNICEF/Oleksandr Ratushniak
Mama mzazi akiwa amelala kando ya kitanda cha mtoto wake mchanga kwenye wadi ya muda ya wazazi kwenye mji mkuu wa Ukraine, Kyiv

Kwa wasafirishaji haramu na wauaji vita ni fursa

Guterres ametaka kila hatua zichukuliwe ili kunusuru makundi yaliyo hatarini kama vile wanawake na watoto kutumbukia kwenye midomo ya wauaji na wasafirishaji  haramu akisema, “kwa wauaji na wasafirishaji haramu vita si janga bali ni fursa. Nitaendelea kupazia sauti adha wanayopata wananchi wa Ukraine kama ninavyofanya tena leo hii.”

Madhara ya vita Ukraine yanavuka mipaka

Katibu Mkuu ametanabaisha kuwa madhara ya vita nchini Ukraine yanavuka mipaka na waathirika wakuu ni nchi maskini pamoja na zile zinazotegemea bidhaa kutoka Ukraine na Urusi.

“Tegemeo la chanzo cha chakula limepigwa bomu. Urusi na Ukraine zinachangia zaidi ya nusu ya mafuta ya alizeti na takribani asilimia 30 ya unga wa ngano unaotumika duniani kote,” amesema Guterres.

Ukraine peke yake inatoa zaidi ya nusu ya unga wa ngano unaosambazwa na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP.

Tweet URL

Bei za chakula, mafuta na mbolea zinaongezeka kwa kasi kubwa. Minyororo ya usambazaji wa bidhaa imevurugwa na gharama za usafirishaji na kuchelewesha bidhaa zinazoagizwa kutoka nje pindi zinapopatikana nazo zimefikia kiwango cha juu kuwahi kufikiwa.

Ngano inayotegemewa kutoka Ukraine na Urusi sasa hatihati

Nchi 45 za Afrika na nyingine zinazoendelea huagiza theluthi moja ya ngano kutoka Ukraine au Urusi, na 18 kati ya hizo zinaagiza takribani asilimia 50.

Nchi hizo ni pamoja na Burkina Faso, Misri, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Lebanon, Libya, Sudan na Yemen.

“Lazima tuchukue hatua zozote zinazowezekana kuepusha kimbunga cha njaa na kusambaratika kwa mfumo wa chakula duniani,” amesisitiza Katibu Mkuu.

Guterres amesihi viongozi wa dunia kujizuia kupeleka fedha zaidi katika bajeti za silaha na badala yake zielekeze kwenye misaada rasmi ya maendeleo na hatua kwa tabianchi wakati huu ambapo mataifa maskini yanahaha kupata fedha kujikwamua kutoka madhara ya janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19.

Janga hili amesema lazima likome na katu “hatujachelewa kutumia diplomasia na mazungumzo. Tunahitaji amani, amani kwa ajili ya wanachi wa Ukraine.