Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nani apewe nani anyimwe chakula: Uamuzi mgumu kwa mashirika ya UN 

UNHCR na wadau wamehamisha wakimbizi kutoka Sudan na Sudan Kusini hadi mahali salama Ethiopia Benishangul ukanda wa Gumuz.
© UNHCR/Adelina Gomez Monteagud
UNHCR na wadau wamehamisha wakimbizi kutoka Sudan na Sudan Kusini hadi mahali salama Ethiopia Benishangul ukanda wa Gumuz.

Nani apewe nani anyimwe chakula: Uamuzi mgumu kwa mashirika ya UN 

Wahamiaji na Wakimbizi

Mamilioni ya familia za wakimbizi katika eneo la Mashariki mwa Afrika ziko hatarini kutumbukia kwenye njaa kali wakati huu ambapo mgao wa chakula unapungua kutokana na rasilimali za misaada ya kibinadamu kuzidiwa uwezo kwa sababu za mizozo lukuki, madhara ya tabianchi, janga la COVID-19 na ongezeko la bei ya chakula na mafuta, yamesema mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa, lile la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na mpango wa chakula duniani, WFP. 

Kupitia taarifa ya pamoja iliyotolewa leo Geneva, Uswisi, mashirika hayo yamesema, licha ya juhudi za kuhakikisha chakula kilichopo kinapatiwa familia kwa misingi ya kipaumbele cha uhitaji, idadi ya wakimbizi wenye uhitaji inaongezeka, sambamba na pengo la rasilimali zilizopo na kile kinachohitajika. 

Wakimbizi hao wako katika nchi za Burundi, Djibouti, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Sudan, Tanzania na Uganda. 

Katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, idadi ya wakimbizi Mashariki mwa Afrika imeongezeka mara tatu kutoka milioni 1.82 mwaka 2012 hadi takribani milioni 5 leo hii, ikiwemo wakimbizi wapya 300,000 mwaka jana pekee. 

Changamoto ni kuamua nani umpatia chakula nani umnyime 

WFP inasema ongezeko la idadi ya wakimbizi isiyoendana na chakula kinachopatiakna kinaliacha shirika hilo na uamuzi mgumu wan ani apatiwe msaada wa chakula na nani anyimwe. “Leo hii asilimi a70 ya wakimbizi wenye uhitaji hawapokei mgao kamili wa chakula kutokana na ukata,” amesema Clementine Nkweta-Salami, Mkurugenzi wa UNHCR kwa kanda ya Mashariki, Pembe ya Afrika na Maziwa Makuu. 

Amesema watoto wengi zaidi wenye umri wa chini ya miaka 5 wanakumbwa na viwango vya juu vya udumavu na ukuaji usiondana na umri wao kwa kuwa hawana lishe bora na virutubisho vinavyotakiwa wakati wanakua. 

“Familia hazijui mlo ufuatao unatokan awapi na wanakumbwa na deni kubwa, wanauza mali zao na hata kuwaondoa watoto wao shulen ili washiriki katika kazi. Hii inaongeza hatari ya ukatili wa majumbani. Kuwaondoa watu kwenye hatari hii inapaswa mahitaji yao ya chakula yaweze kukidhiwa.” 

“Ukweli wa kusikitisha ni kwamba eneo la Mashariki mwa Afrika linakumbwa na mahitaji ya aina yake ya kibinadamu, yakichochea na mabadiliko ya tabianchi, mizozo, ukosefu wa utulivu na ongezeko la bei za vyakula na nishati ya mafuta,” amesema Michael Dunform, Mkurugenzi wa WFP kanda ya Mashariki mwa Afrika. 

Amesema ongezeko la mahitaji kwenye ukanda huo linaakisi kile kinachoonekana pia duniani kote, “hivyo tunaomba dunia isiipe kisogo eneo hili na hususan jamii zilizo hatarini zaidi za wakimbizi ambazo zina fursa finyu ya mbinu za kujipatia kipato na tegemeo lao kuu ni WFP ili ziweze kuishi. 

WFP kwa kuanzia kipindi cha mwezi huu wa Aprili hadi Septemba mwaka huu wa 2022, inahitaji dola milioni 226.5 kukidhi mgao kamilifu wa chakula kwa wakimbizi katika nchi zilizoko Mashariki mwa Afrika.