Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mnufaika wa mpango wa UNHCR asimulia safari yake kutoka DRC, Tanzania hadi Marekani

Aliyekuwa mkimbizi kutoka DRC, Lubunga Mwendanababo, sasa ni raia wa Marekani.
UN News/Assumpta Massoi
Aliyekuwa mkimbizi kutoka DRC, Lubunga Mwendanababo, sasa ni raia wa Marekani.

Mnufaika wa mpango wa UNHCR asimulia safari yake kutoka DRC, Tanzania hadi Marekani

Wahamiaji na Wakimbizi

Katika mwendelezo wetu wa kupitia taarifa ambazo zilikuwa na uzito wa juu kwa mwaka huu wa 2018, tunakurejesha kwa Lubunga Mwendanababo, mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambaye baada ya kuishi ukimbizi Tanzania, sasa amepata uraia wa Marekani ikiwa ni manufaa ya mpango wa shirika la Umoja wa Mataifa UNHCR la kuwapatia wakimbizi hifadhi kwenye nchi ya tatu. Grace Kaneiya anakurejesha kwenye taarifa hiyo ya tarehe 13 Novemba mwaka 2018.

Hii ni sauti ya Lubunga mwendanababo, mkimbizi kutoka DRC, ambaye aliishi katika kambi ya Nyargusu nchini Tanzania.

 Kijana huyu ambaye alikimbia DRC miaka ya tisini akiwa na umri wa miaka mitano katika mahojiano maalum nami jijini New York, Marekani mwezi uliopita wa Novemba nilimuuliza kile anachokumbuka katika safari yake ya kutoka DRC hadi Tanzania.
 
“Tuliingia kwenye boti tukaenda mapka Tanzania, tukaishi pale tulikuwa tunalala kwenye hema, baada ya pale tukajenga nyumba ya matofali, chakula tulikuwa tunapokea pale ila kuni tulikuwa tunatafuta wenyewe na tulipofika walitupatia nguo na viatu.”

Mzawa huyu wa DRC licha ya kwamba sasa yuko Marekani ambapo amemaliza shahada ya kwanza na sasa anafanya kazi bado analilia nchi yake.

“Inasikitisha sana na moyo wangu unauma, kwa sababu mimi ni mkongomani ninapoangalia habari kwamba kuna watu wameuwawa, watoto wanatumikiswah jeshini, wanawake wanabakwa, inaniumiza sana lakini ninaimani kuwa DRC itapata amani.”

Sasa hivi Mwendanababo ana ndoto za kusoma hadi shahada ya uzamili na anasema elimu imekuwa msingi muhimu katika maisha yake.

“Nilikuwa na matumaini ya kuwa kutakuwa na maisha baada ya vita na sikukata tamaa, niliamini kuwa shule ni msingi wa maisha na wazazi wangu kwa kuwa wamesoma walinisukuma kuendelea na masomo licha ya kuwa ukimbizini.”

Hata hivyo ukosefu wa amani DRC bado ni kidonda moyoni kwa Lubunga.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.