Nimeazimia kuendelea na masomo yangu hadi Chuo Kikuu kama Mungu ataruhusu-Mkimbizi Gift Maliamungu

8 Oktoba 2019

Gift mtoto aliyejikuta peke yake nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC baada ya kuyakimbia mapigano nchini Sudan Kusini, amefanya vizuri katika mtihani wa darasa la sita baada ya kuibuka na alama za juu katika mashindano ya tahajia za maneno lakini matarajio yake ya kuendelea na masomo ya juu yanaweza kupotea kwa kuwa hakuna nafasi za kutosha kwa wakimbizi.

Ni kijana mdogo mkimbizi kutoka Sudan Kusini ambaye machafuko nchini mwake yamemfanya ajikute ukimbizini nchi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. Hapa anajitambulisha kuwa anaitwa Maliamungu Gift.

Wakimbizi watoto walioporwa utoto wao wanaweza kuurejesha utoto wao kupitia elimu. Lakini hakuna shule au rasilimali za kutosha. 

Hata hivyo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limeanzisha mpango wa kukuza uandikishaji kwa masomo ya sekondari hiyo ikimaanisha watoto kama Gift wanayo nafasi nzuri ya kuendeleza masomo yao.

Kwa mujibu wa UNHCR, ni asilimia 8 tu ya wakimbizi walioko nchini DRC ambao wanamudu kuifikia elimu ya sekondari.

UNHCR inawasaidia kuwasajili katika mfumo wa shule wa taifa lakini kwa walio wengi, mustakabali wao una kiza kinene. Gift anasema anataka akikua awe mwalimu kwa kuwa anataka kusaidia watu na anaeleza kuwa vita husababisha watu wengi kuteseka,

(Sauti ya Gift)

“Tulipofika, watoto wengine walisema hawakuweza kwenda shule kwa sababu hawazungumzi kifaransa. Nilijiambia lazima niweze na sitakata tamaa.”

Gift ambaye sasa anasoma katika shule ya msingi Biringi nchini DRC, anasema shuleni haendi kucheza, anautumia muda wake wote kujisomea na anapokuwa darasani anakuwa mchangamfu.

Pia anaeleza kuwa kufikia saa moja asubuhi anakuwa shuleni na wanasoma hadi saa sita na dakika hamsini. Kisha anaenda nyumbani kula na kupumzika kwa saa moja. Baada ya hapo anajisomea kwa muda wote wa siku uliosalia na usiku anatumia taa ya sola aliyoiunda mwenyewe.

(Sauti ya Gift)

“Nililazimika kutengeneza taa hii inayotumia mionzi ya jua kwa kuwa usiku siwezi kujisomea. Siyo taa bora lakini nimeiunda na inafanya kazi.”

Gift anasoma kwa bidii lakini anahofia mstakabali wake,

(Sauti ya Gift)

“Ninajua kuandika, ilikuwa rahisi kwangu kujifunza haraka na kuandika. Ninaposoma inakuwa rahisi kwangu kuelewa. Ndiyo maana ninaendelea vyema hapa Congo. Nimeazimia kuendelea na masomo yangu hadi chuo kikuu kama Mungu ataruhusu na kama kuna hela ninataka kuikamilisha elimu yangu. Sitakata tamaa nitamaliza masomo yangu. Hamu yangu ni kila mtoto kwenda shule kama mimi. Siyo haki kwa watoto wengine kwenda shule wakati wengine hawaendi. Kama kuna namna, ningependa watoto wote waende shule.”

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud